CCM, Chadema kubanana bungeni Jumatano | Send to a friend |
Saturday, 11 June 2011 20:37 |
Ally Mkoreha, Dodoma WAKATI mjadala kuhusu bajeti ya serikali katika mwaka wa fedha wa 2011/12, ukitarajiwa kuwa mkali ndani ya Bunge, kufuatia hatua ya awali ya Kambi Rasmi ya Upinzani, kupinga bajeti hiyo kwa maelezo kuwa haikutoa unafuu wa maisha ya wananchi wa kawaida, wabunge wa CCM wamesema wamejipanga kuitetea kikamilifu. Habari zilisema wabunge wa chama hicho kinachoongoza serikali, walikutana juzi katika kikao cha kamati yao ambayo Mwenyekiti wake ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.Katika mkutano huo wabunge hao waliweka mikakati jinsi ya kutetea bajeti hiyo, iliyowasilishwa bungeni Jumatano iliyopita na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo. Katika hotuba yake, Mkulo alisema bajeti hiyo imelenga kuwapunguzia wananchi, makali ya maisha na kwamba, ndiyo maana serikali imeondoa tozo mbalimbali za mafuta na kufuta kodi kwenye pembejeo za kilimo. Alisema kupanda kwa bei ya mafuta, ni moja ya mambo yaliyosababisha ugumu wa maisha miongoni mwa wananchi. Hata hivyo siku moja baada ya kuwasilishwa kwa bajeti hiyo, kambi ya upinzani kupitia kwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, iliibuka na kuiponda kuwa ni bajeti hewa haikulenga kuwasaidia walalahoi kama ilivyoelezwa na serikali. Hatua hiyo ilisababisha Waziri Mkulo kuibuka mjini hapa na kuwaeleza waandishi wa habari kuwa, Zitto amepotosha umma kujitafutia umaarufu wa kisiasa. Hali hiyo inaashiria kuwapo kwa mvutano kati ya wabunge wa CCM na wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inayoongozwa na Chadema katika mjadala kuhusu bajeti itakayojadiliwa kuanzia Juni 1 5 hadi 21, mwaka huu. Wakizungumza na Mwananchi jana kwa masharti ya kutotajwa, baadhi ya wabunge wa CCM walithibitisha habari kuhusu kuwapo kwa kikao cha kamati yao na kwamba, kilikuwa na lengo la kuweka msimamo wa pamoja kuhusu kutetea bajeti. "Ni kweli jana (juzi) tulikuwa na kikao cha Kamati ya Wabunge wote wa CCM, kuweka msimamo wa pamoja kutetea bajeti yetu. Tumejipanga vilivyo kuwakabili wapinzani wetu na tuna uhakika kwa kuwashinda katika mjadala huo kwa sababu bajeti yetu ni safi na wao wanaikubali ingawa kwa tabia yao, wanaipinga, alisema mmoja wa wabunge hao. Lakini akizungumzia majigambo hayo ya wabunge wa CCM, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, alisema: Wabunge wa CCM watashinda kwa kupiga meza na kuzomea, ni mabingwa katika hayo lakini siyo hoja, kila mtu anajua hilo. |
Hivi wabunge wetu wana mpango gani na sisi wananchi? Kwao vyama ni muhimu kuliko maisha bora kwa wapiga kura? Ndio maana nasema alaaniwe aliyepindisha hukumu ya Mgombea binafsi