Bob Marley's 69th Birthday

AL SHARPTON

JF-Expert Member
Feb 6, 2014
2,797
952
Today would have been Bob Marley's 69th birthday.
Marley was born in St. Ann Parish, Jamaica on Feb. 6, 1945. His Jamaican roots remained a cornerstone of Marley's personal identity and musical style, selling over 20 million records throughout his career. Marley began his career in music as part of The Wailers, a group which helped to shape the reggae genre as they released some of the earliest albums of its kind. In the mid–'70s, Bob Marley launched his solo career, quickly becoming a cultural icon, largely due to the popularity of his album "Exodus."
Marley's Rastafarian lifestyle and reggae–crossover music are as culturally iconic now as they were during his 36 years of life. The musician died of melanoma in 1981.
Happy birthday, Bob Marley! The sun is shining.

bob-marley-wallpaper-900x500-1384549156.jpg

Historia yake fupi
Historia hii fupi ya msanii huyo katika uhai wake ambaye kwa hakika alikuwa mpiganaji wa Gheto ,inaandikwa na Steve Jonas.

Mara nyingi umekuwa ukisikia ama kuwaona baadhi ya watu wapigania Uhuru na maskani yao kuweka msituni. Lakini Bob Marley ambaye kwa jina lake halisi aliitwa Robert Nesta Marley, alikuwa mpigania Uhuru na haki ambapo kampeni zake aliziendesha akiwa mjini wala si msituni.

Alikuwa mtoto mpenzi wa Gheto,alipigana kwa kutumia sauti yake na nyuzi za gitaa lake.Mikogo ya sauti yake ilivuma kote Duniani akafurahisha,akaamsha ,akasuta na akahimiza.

Alikuwa jabari wa Regae kama alivyokuwa mpinga uonevu,lakini mpiganaji huyu wa mjini,Robert Nesta Marley( Berhane Selasie) au kama wote tulivyozoea kumwita kwa jina la Bob Marley,alitokea shamba .Bob alizaliwa bondeni katika kijiji cha Nine Miles.

Sina maana kwamba bondeni huko tuliko kuzoea sisi ,Afrika ya kusini la hasha,ni bonde ambalo liko kwenye jimbo la St.Ann's nchini Jamaica ,alizaliwa February 5 mwaka 1945 na alifariki akiwa na umri wa miaka 36 tu,lakini si haba ndani ya miaka hiyo Bob alitoa mchango wake mkubwa katika ulimwengu wa muziki.


Bob ambaye alikuwa akipigania Uhuru na haki katika staili ya midundo ya Regae,baba yake alikuwa ni afisa wa Jeshi kikosi cha maji nchini Uingereza ambaye alifariki wakati Bob angali tumboni mwa mama yake Bibi Cedella Booker mwanamke wa kiafrika.

Mama yake Bob alikuwa mwimbaji mahiri wa kwaya kanisani Bob aliupitisha udogo wake huko shamba kwenye mazingira ya wakulima wa ndizi na minazi ,akinywa madafu,akiwakamua ng'ombe maziwa na mbuzi pia aliogelea kwenye vijito na Bahari.

Bibi Cedella Booker hakutaka mwanaye aishie kutanga tanga na kuzurura.Aliogopa mwanaye kuharibika kama ilivyo kwa watoto wa familia zingine zenye tabaka la chini, alitamani sana mwanaye ajifunze kazi yoyote ya ufundi ambayo ingeweza ingeweza kumudu maisha yake hapo baadae.

Bob akaanza kujifunza ufundi wa kuchomelea (welding) katika ufundi huo Bob alikuwa akishirikiana na kijana Desmond Dekker,waliketi katika benchi huku wakifanya kazi pia cheche zikiruka huku na huko kutoka katika lile benchi.

Bob na Desmond walikuwa ni vibarua waliolipwa ujira wa siku ,huku wakiendelea na shughuli za uchomeleaji,vijana hawa walifundisha nyimbo na mara nyingi walipokuwa kazini hapo walionekana kutingwa na kazi lakini waliendelea kuimba na kuchapa kazi.

Siku moja kipande cha chuma chenye moto kilirukia jichoni kwa Desmond.Hapo mambo ndipo yalianza kubadilika,Desmond aliamua kurudi nyumbani na kwa kuwa alikuwa na ujira wa kutwa ,hivyo hakuwa na kipato cha na wakati huo akiendelea kuuguza jicho lake akaamua kuanza kile kilichokuwa kwenye damu yake (muziki).

Desmond Dekker baada ya muda akatoa kibao chake cha muziki kilichoitwa ‘Honour Thy Father and Thy Mother' akimaanisha ‘waheshimu Baba na Mama'wimbo huu ulipendwa sana na katika mafanikio hayo ilikuwa ni kijana huyo kusaidiwa na studio za Beverleys.

Mambo yalipo mnyookea katika muziki,Desmond alimshawishi Bob ajaribu kuupa wasaa zaidi muziki.Bob alikubaliana na ushauri wa Desmond na walikwenda kwenye studio za Beverleys. Huko Bob akakutana na Jimmy Cliff mwana muziki mashuhuri.

Cliff mbali ya umaarufu aliokuwa nao wa kimuziki hasa katika sinema ya ‘The Harder They Come',alikuwa na moyo wa huruma na kupenda kusaidia akamsaidia Bobo kwa vifaa na ushauri mpaka hapo Bob alipofanikiwa kuipua wa kwanza wa ‘Judge Not'.

Wakati huo Robert Nesta Marley alikuwa na umri wa miaka 15 tu,wakati huo huo mama yake tayari alikwisha hamia Marekani(U.S) alimwacha Bob akijifunza ‘welding'.

Baadae Bob alipokuwa akiishi Gheto huko Trench Town kwenye nyumba ya baba yake Bonny Livingstone ikiwa ni muda mfupi tu tangu alipounda urafiki na Bonny,kijana mmoja mwembamba mrefu,mcheshi mwenye maneno mengi,Peter Tosh alionekana akipitapita mitaani akiwa na Gitaa lake.

Alikuwa akipiga na kuimba,akicheka na kutania,akitukana na kuchokoza na ubishi kama jadi yake.Watu hawa watatu ndio walioanzisha kundi zima la The Wailers.Waanzilishi hao ni BonnyLivingstone,Bob Marley na Peter Tosh.Mwanzoni walijiita The Wailing Wailers.

Baada ya vigogo hao kupatana vyema huko Kingstone katika Gheto la Trench Town,ndipo mwimbaji mwingine alijiunga aliyeitwa Junior Braith Waite lakini hakuweza kukaa sana kutokana na wazazi wake kuhamia Marekani ambako ilibidi aongozane nao.

Kulikuwepo pia wasichana wawili ambao ni Rita ambaye baadae alikuja kuolewa na Bob Marley na Beverley Kelso.Lakini akina dada hawa hawakudumu sana japo walikuwa waimbaji wazuri sana,huko mbele Rita akiwa The I Threes alikuja kuendelea kuimba na Marley.

Huku wakidhaminiwa na Beverleys Records.Bob,Bonny na Tosh wakayapanda majukwaa ya Kingstone wakiimba nyimbo zenye mtazamo wa kibiblia pamoja na nyimbo za mapenzi kama vile wimbo wa ‘Do It Twice'waliimba nyimbo za kuchangamsha na kuliwaza vijana wa Gheto.



Waliwaliwaza vijana wa Gheto kwa sababu ya kukosa kazi huku wakizongwa na Polisi,pia waliimba nyimbo za kuulaani utumwa ambao mtu mweusi alikabiliwa nao kwa muda mrefu sana hali ambayo ilionyesha kama vile mtu mweusi hana haki yake hapa Duniani.

Kujulikana kwa vijana hawa kuliongezeka zaidi hasa pale walipo chukuliwa na ‘Studio one' ya jamaa aliyeitwa Coxsone Dodd,huyu jamaa alikuwa maarufu sana hasa katika utengenezaji wa Santuri,lakini mambo hayakuwa mazuri kwa wapiganaji hao kuhusiana na kipato.

Coxsone Dodd hakuwa na nia ya kupanua vipaji vya Bob ,Tosh na Bonny kwani alitaka wamtumikie ,awanyonye, awakamue kasha wabaki hohehahe kimuziki au kwa namna nyingine wasingeweza kupigania haki za wengine huku wao wenyewe wakinyimwa haki zao kimuziki.

Mnamo mwaka 1966,Wailers waliipua kibao kama vile Put It On,Rude Boy, I'm still waiting na Rule them Rudie ambazo zilimwingizia kipato kikubwa Coxsone Dodd,ilfika sikukuu ya Krismasi ambapo vijana hao walidai haki yao ili wakafurahi na wenzi wao Trench Town,Gheto.

Dodd akawapa Paund 60,Bob hakuweza kuvumilia akazichukua pesa hizo na kumtupia usoni Dodd kasha akaanza safari ya kumfuata mama yake Marekani huko akaendelea kutunga nyimbo kama vile wimbo uitwao ‘Bend Down Low'.

Akiwa huko Marekani Bob akapata kibarua katika kiwanda cha kutengeneza magari aina ya Cryster kilichopo mjini Delaware,lakini huko Amerika hakukaa sana aliamua kuondoka nchini humo baada ya kupata barua .

Barua aliyoipata Bob ilimtaka akapigane vita huko Vietnam,wazo hilo Bob hakuafikiana nalo huku akijiuliza ni kwa nini aende kupigana vita au kushiriki katika suala la mauaji ya watu wasio na makosa ,akarudi Jamaica.


Ulimwengu wa kibepari bado uliendelea kumtupa huku na kule ,aligundua kuwa kila mahali wanataka kumtumia au kukitumia kipaji chake cha muziki ili wajitajirishe wao au kumtumia kama kibarua mchomeaji kasha kumlipa ujira mdogo ama kutumia ujana wake katika vita huko Vietnam kwa manufaa ya mabeberu.

Watu hawa wanajifanya ni marafiki kumbe wanataka kumtumia tu kama ilivyokuwa kwa Coxsone Dodd ambaye alijifanya rafiki kipenzi wa Bob hata kufikia hatua ya kumsaidia Bob chumba cha kulala nyuma ya Studio One lakini Bob alipodai haki yake alipewa paund 60 tu ambazo Dodd alitupiwa usoni kwa hasira.
‘Watoto,
Mwanadamu anamdhurumu mwanadamu mwenzie,
Mpaka unashindwa kujua yupi umwamini,
Adui yako mkubwa anaweza kuwa rafikio mkubwa ,
Na rafikio mkubwa anaweza kuwa adui yako mkubwa,
Wengine watakula na kunywa nawe,
Kumbe nyuma yako wanakuhujumu,
Ni rafiki tu ajuae siri yako,
Hivyo ni yeye tu awezaye kuitoa ,
Mwache aivae kofia Yule ambaye inamtosha,

Maneno hayo yanaonyesha hali halisi Bob alivyo itambua jamii ya Kibepari na ndipo alipoamua kuifikishia ujumbe huu Dunia nzima kupitia kibao chake cha ‘Who The Cape Fit'katika Santuri ya Rastaman Vibration.

Basi,Bob mambo yake yaliendelea kusua sua huko Jamaica kwa sababu hakuwa na pesa wala mtaji kwani walio kuwa na uwezo huo walikuwa Chui ndani ya ngozi ya Kondoo,wanafiki na makupe.

Wailers wakaendelea na Regae katika hali ya nguvu na kushindana na umasikini na unyonyaji,mwaka 1969 Lee Perry Scratch ambaye zamani alikuwa akimfanyia kazi Coxsone Dodd,akawa ameeanzisha Studio yake mwenyewe iliyoitwa Upsetter .

Upsetter ikishirikiana na kampuni ya Trojan Records ya Uingereza na kutoa Albam za Wailers Rasta Revolution Herbsman.Wailers wakawa wamewasha moto na kuushitua Ulimwengu,sasa masikio yakawa yameelekezwa huko Jamaica na Regae ikaanza kuingia kwenye damu za watu wa nje ya Jamaica.

Wailers wakiwa na studio ya Lee Perry Scratch (Upsetter),Bob ,Peter na Bonny wakakutana na ndugu wawili ,hao walikuwa watoto wa mzee Barett ambao ni Carlton Barett(Carly) na Aston Barett (Family Man),Carly alikuwa mpiga ngoma (Drums) na Family Man alikuwa akipiga Gitaa zito.

Katika nguvu hiyo mpya Bob ,Peter na Bonny waliandika nyimbo za kuziimba ,Carly na Aston wakakamata vyombo vyao kwa hakika wote walikuwa na uwezo wa kuimba na wote walikuwa na uwezo wa kupiga vyombo,siku za harakati hizo zikaendelea .

Baade Bob Marley alipokutana na Chris Black Well,ambaye alikuwa mtengenezaji Santuri,Black Well alikuwa mzungu aliyetokea kwenye familia ya kitajiri tena ya kikoloni nay a kibaguzi,alijichanganya na wafanya kazi weusi huko Uingereza akajifunza Lugha na tabia zao akawazoea na wakamzoea.

Kampuni yake ya kutengeneza Santuri hakuianzisha kifahari na kitajiri katika vitongoji vya Mabepari bali alianzisha kwenye kitongoji chenye makazi ya watu weusi.

Chris aliyatazama macho maangavu ya Bob,akautazama mwili wake mdogo ulio shupaa, akaisikiliza sauti yake iliyo jaa hisia ,hamasa na azma…'Bob anatetea kitu chenye uzito mkubwa '.Alisema Chris Black Well. ‘Na The Wailers ni kundi kubwa kisanaa ,naamini ni watu wanaostahili kupata msaada ,muziki wao unauzito kuliko wa Rock'.Alisema Chris.

Hayakuwa maneno matupu ,Chris aliwapatia The Wailers vifaa vipya tena vya kisasa ambavyo hapakuwa na Bend yoyote ya Jamaica ambayo iliwahi kumiliki au kuvitumia vyombo vya aina ile.Wakaamua kutengeneza Albam za Stereo.

Uuzaji na usambazaji wa Black Well ulikuwa mzuri sana .Wailers wakapiga Regae nzuri ,na Island Records yaani kampuni ya Black Well ikarekodi na kuuza Albam vema ingawa yeye Chris hakuwa mwanamuziki (mpigaji).

Hakika alitoa mchango mkubwa kuuza na kuusambaza muziki wa Regae Duniani kote hata kuwepo kwa gumzo kubwa kuhusiana na kundi zima la The Wailers,pia hatuwezi kuzungumzia The Wailers bila kumtaja Chris Black Well.Aliwapa kila kifaa walichokitaka hata studio aliwaachia .

Studio hiyo waliitumia walivyo taka ,wakati wowote,akawatengenezea Santuri za stereo,akazisambaza vizuri kote .Albam ya ‘Catch a Fire' ilitolewa mwaka 1973 ikiwa ni moja ya kazi za Island Records na kila mpenda Regae aliifurahia Albam hiyo.

Mnamo mwishoni mwa mwaka 1973,baada ya ziara ya The Wailers kutoka London ,Bunny Wailer alionyesha wazi kuwa hakuwa tayari kuendelea na The W ailers.Naye Yule kijana mrefu ,mbishi,aliyejiamini sana Peter Tosh asiye kubali kudhalilishwa pia alionyesha nia kama ya Bunny.

Redio,Matangazo,Magazeti ya Kibepari hayakutaka kabisa kukubali mafanikio ya The Wailers kwamba yalitokana na bidii za pamoja za wahusika wote,bali vyombo vyote hivyo viliamini kwamba kila kitu kilifanyika na Bob Marley na hao wengine walifanywa kama vijana wake tu kitendo ambacho kiliwaudhi Bunny na Tosh,hizo zilikuwa hisia ,mbinu za mabepari ili kuhakikisha wanawatenganisha.

Hata kama Bob alikuwa kiongozi ,wenzie pia walikuwa na umuhimu mkubwa na walifanya kazi kubwa .Bunny na Tosh walikuwa si waimbaji wazuri tu bali pia walikuwa watunzi wazuri wa nyimbo na upigaji wa kama Carly na Aston haikustahili kudhalilishwa .

Bunny akaamua kuwa mkulima ,akashika shamba katika sehemu iitwayo Bull Bay,akiwa na ndoto moja ,kuzalisha chakula kingi iwezekanavyo,ikiwezekana cha kuweza kuilisha Jamaica nzima.Lakini hakuacha muziki,baada ya muda akaipua albam ya Black Heart Man.

Katika wimbo huo ,Bunny kuna maneno anayasema akidai kwamba ‘walimuua Lumumba kwa kupigania haki zake ,lakini hawawezi kumzuia Rasta'.Naye Peter hakuacha muziki wala hakufa kimuziki kama baadhi ya magazeti ya kibepari yalivyo tabiri.

Yalidai kuwa kiburi cha Tosh baada ya kujitenga kilimfanya amuonee wivu Robert Nesta Marley.Ili kukata ngebe hizo za wanafiki,Tosh alipakua Albam ya Legalise It na Equal Rights.Wakaanza kusema Tosh si mwanamuziki ila ni mvuta Bangi aliye changanyikiwa anaye pigania haki za Ganja (Ndumu).

Upuuzi huo haukufika popote kwani watu walizipokea vizuri tu hizo Albam zake na zikapendwa sana .Adui zake hawakufurahi sana walipo msikia akiimba na kutukuza Rasta,kutetea wakandamizwaji,kutetea Afrika ya kusini na kupinga ubaguzi wa rangi .

Baada ya Peter na Bunny kuondoka 1974,Bob alianza kutafuta wanamuziki wengine,akampata Al Andason Rasta ambaye alikaa sana Marekani(New York),akampata Junior Marvin (Rasta bitoz),mtanashati na maridadi lakini mwenye bidii na moyo usio kata tama.

Tena akapatikana Tyrone Downie kijana ambaye kwa muda mrefu alikuwa anawahusudu sana The Wailers,wakajiunga pia wale I Threes,wanawake weusi watatu waliokuwa na sauti nzuri ambao ni Rita Marley,Juddy Mowatt na Marcia Griffiths walimsaidia Marly katika uimbaji.Juddy alitoa Albam ya Black Woman.

Naye Rita Marley alionyesha umahiri wake kwa kuipua albam iliyoitwa ‘Who Feels It Knows It'.Vilevile mwanadada Marcia alithibitisha dhahiri kwamba yeye ni mwimbaji bora huenda kuwazidi hao wenzie Juddy na Rita, alishirikiana vyema na Bob katika santuri yake iitwayo ‘Young Giftted and Black'.

Kwa hakika walijituma sana katika kuboresha muziki wa Regae na ndilo lililo kuwa kundi jipya lililounda nguvu ya The Wailers ambalo lilitoa albam iliyowatia moyo ma-Rasta iliyoitwa ‘Natty Dread' ambayo iliwajaza hamasa vijana weusi wa Ulaya na Duniani kote.

Katika albam hiyo hakika kuna ujumbe uliokomaa kimuziki,muziki ulionyooka,muziki wenye kilio na azma,muziki ulioonyesha kujiamini na majivuno ya mtu ya mtu anaye jua afanyalo.unaonesha matatizo kadhaa ya Rasta huko Jamaica ambako sheria kadhaa ziliwapiga vita.

Ukaonyesha shida na raha za maisha ya njini,akawataka watu weusi wajiulize walikotoka na asili yao ya kitamaduni.Ulizungumzia mahaba, mapinduzi umasikini,kutaharuki na kuazimia,uchungu na hasira.Itegee sikio kama nyimbo ya No Woman No Cry,Natty Dread na Talking Blues'.

Ilifika wakati Fulani Bob na Wailers walivamiwa na kushambuliwa kwa risasi,kila watu wengi walihisi kuwa walishambuliwa kwa sababu ya mawazo yao hasa yaliyotokana na albam yao ya Natty Dread.

Jamaica ilikuwa ni nchi yenye upinzani mkali wa kisiasa.Vyama viwili vikubwa vya kisiasa nchini humo wakati huo vilikuwa ni Jamaica Labour Part(JPL) kilichoongozwa na Edward Seaga na chama cha Peoples'National Part kilichoongozwa na Michael Manley.Ghasia za kisiasa zilitokea mara kwa mara na C.I.A kama kawaida yake haikosi kuingilia kwa maficho.

Mnamo mwaka 1976, The Wailers walifikiria wafanye onyesho ambalo mada yake kubwa ingekuwa kuwaunganisha watu wa Jamaica,kuwasihi waache uhasama na ghasia ,wafungue macho.Serikali ya Michael Manley ambayo ndiyo ilikuwa madarakani ikakubali.Bob alihitaji kufanya onyesho la AMANI.

Jioni moja siku tatu kabla ya onyesho hilo,watu wenye bunduki waliwashambulia The Wailers ambao walikuwa wanafanya mazoezi ya muziki ,ghafla wakasikia milio ya bunduki mlango ukafunguliwa huku mitutu ikitangulia na kutoa milipuko kadhaa.Bob Marley na Rita Marley walijeruhiwa.

Watu wale watano wenye bunduki wakakimbia,Polisi wa Jamaica walishindwa kabisa kuwakamata.Sababu ya hayo mashambulizi haikujulikana lakini hilo halikuwa kikwazo kwa Bob na The Wailers kusitisha onesho hilo na baada ya onesho hilo Bob akaondoka zake kuelekea Miami, Marekani.

Claudie Massop ambaye alikuwa mfanya biashara mweusi ambaye alikuwa mtu mashuhuri jijini Kingston alimsihi Bob arudi Jamaica.Massop aliheshimiwa sana kwenye magheto na alichukuliwa na watu weusi kama kiongozi wa magheto,kilichomuuma sana Claudie Massop ni kuona jinsi vijana walivyokuwa wakipigana hovyo.

Walipigana na kuuana kwenye ushabiki wa vyama vya siasa ambavyo vilikuwa havijawez kutatua matatizo yao.Massop aliona vijana hao wanamalizana bure huku wanao faidi wakiwa ni wanasiasa.Massop alikutana na wanamuziki wengi na kuongea nao.

Alikuwa na lengo kla Bob la kufanya onyesho kubwa jioni ambalo kusudi lake lilikuwa kupinga uhasama uliokuwa umeenea katika jamii.Massop alimchukulia Bob kama mdogo wake hata Bob alimchukulia Massop kama kaka yake hivyo Bob asingeweza kukosa kwenye maonyesho yaliyoandaliwa na Massop,walipendana sana na kuheshimiana.

Wanamuziki wa Jamaica kama vile Jacob Miller na Peter Tosh walikuwepo.Lakini Bunny hakuhudhuria ,yalikuwa maonyesho makubwa yaliyofanikiwa sana, yakaumeza moyo wa kila mtu.Ilikuwa ni vita ya wanmziki wa Gheto dhidi ya uhasama wa siasa na hujuma za C.I.A.

Kilele cha sherehe hizo kilikuwa pale Bob aliposhikanishwa mikono na Edward Seaga pamoja na Michael Manley ambao walikuwa ni viongozi wa vyama vya siasa nchini Jamaica,vyama vya JPL na PNP.Wiki chache baadae baada ya maonyesho hayo Massop akapigwa risasi na kufariki.

Hakuwa na kosa ,hakuwa na silaha ,polisi iliwachukua siku nyingi sana kumpata muuaji aliyekuwa miongoni mwao wenyewe na jambo hilo halikuwafurahisha watu wa Jamaica hata kidogo.Jitihada za Claudie zilikuwa zimekubaliwa na kuheshimiwa na kila mtu,kuuawa kwake kuliwastua wajamaica wengi.

Walijiuliza sana ni polisi gani aliye muua Brother Massop na alikuwa ana mtumikia nani? Lakini yawezekana huyo askari ndiye aliye wajeruhi Bob na Rita Marley walipokuwa wakifanya mazoezi na wenzao wa kundi la The Wailers.

Kiundani zaidi Robert Nesta Marley alikuwa na kipaji pia alipendwa na wengi ,si mashabiki tu bali kwa baadhi ya wanamziki wenzie ambao ni mashuhuri katika ulimwengu wa muziki,walimkubali na kumheshimu kama vile Jimmy Cliff.

Mnamo mwaka 1972 John Nash alipiga na hata kurekodi nyimbo za Bob Marley ambazo ni Stir It UP,Guava Jelly na Nice Time,vile vile alimfanyia mpango wa kurekodi regae on bload way katika studio za CBS.1974 mwanamziki mashuhuri wa mtindo wa rock Eric Clatton,alipiga wimbo wa Marley ‘I'Shot The Sherriff'.

Naye mwana mziki asiye ona Stevie Wonder katika uwanja wa Taifa wa Kingston,walijumuika na Bob kutumbuiza .Mnamo mwaka 1980 Stevie alirekodi ‘Master blaster' iliyojulikana na kupendwa sana, msingi wa ‘Master blaster' ulikuwa wimbo wa Bob,Jamming Commoderes huko Madson Square Gardens,New York.

Mbali ya kuongea juu ya kipaji cha Bob Marley katika muziki,sasa tuangalie utamaduni wa Rasta ambazo hata Marley alikuwa nazo na zilimpendeza sana ,Rasta ni kitu chenye uzito na undani zaidi ya baadhi ya watu wafikiriavyo,Rasta waweza kusema ni mfumo Fulani wa maisha


Baadhi ya vijana kuwa Rasta ni ile hali ya kutokunyoa nywele na badala yake kuzisuka na kuzisokota tu ili ziwe ndefu.Lakini Rasta haishii hapo,Rasta ni utamaduni unaokumbatia mila ,desturi,din,itikadi na siasa.Kwa ujumla wake utamaduni wa Rastafari ni ni utamaduni wa uasi.

Ni utamaduni uliochipuka katika jamii ya watu weusi na machotara ambao daima walijikuta wakinyanyaswa na kudharauliwa.Hususani huko Carriabean walianza kujiuliza wao ni akina nani hasa,asili yao ni wapi, walitoka au walitokea wapi, kwa vipi, sasa wana hali gani na wafanye nini ili maisha yao yawe bora na ya neema zaidi.

Katika imani za kirasta kuna vipengele vinavyo osha hamu ya mtu mweusi (aliye nje ya Afrika) kurudi Afrika ikiwa mtu unanyanyaswa daima mahala ulipo,ikiwa kila uendapo na kila upitapo unadhulumiwa,unatukanwa na kubaguliwa,ikiwa watawala wanakufanya ujihisi hutakiwi,wazo la "wapi ulikotoka" linajengeka kirahisi na kushika mizizi.

Unatamani ulikotoka kwa sababu unajenga hali Fulani ya uasi na jeuri,unaitukuza asili yako.Hivyo ndivyo cheche ilivyojenga mawazo ya "going back to my root"inachipuka katika jamii ya watu weusi wala si jamii ya weupe huko Marekani.Mweupe hana anachokikosa.

Kweli,hana anachokikosa cha kumfanya atamani Ulaya alikotoka,amekuta kuna ustawi huku kuliko huko kwenye asili yake.Alilie nini basi? Na ndio maana hujawahi kumsikia kaburu akililia "Roots"(asili) yake.

Kimila na kidini,biblia ina nafasi kubwa katika maisha ya Rasta kwa sheria ,Rasta anapaswa kusoma walau sura moja ya biblia kila siku,wanaamini kuwa biblia inaupinga mfumo wa sasa duniani ambao ni wa kinyonyaji,wanaouita mfumo wa BABY LONE.

Wanaamini kuwa yeyote anayefuata Biblia lazima awe mpigania haki za mtu mweusi mpigania haki,usawa na uhuru na mpinga unyonyaji anaye wakubali Rasta.Na ndio maana imani ya Rastafariani inamshambulia sana Papa,kiongozi wa madhehebu ya Kikatoliki kwa kumwita mwongo ,mnafiki na ni nguzo ya mfumo wa Babylone.

Rasta wanaamini kuwa chimbuko lao na asili yao ni Afrika hususa huko Sheshamane nchini Ethiopia,Rasta huwa na hamu kubwa sana ya kukanyaga ardhi ya Sheshamane katika Bara la Afrika .Bob Marley alitembelea Sheshamane mnamo mwaka 1978 ambako alikutana na Rasta wenzake.

Baada ya hapo alirudi wa sherehe za Uhuru wa Zimbabwe.Vilevile Rasta wanacho chakula maalumu ambacho kinaitwa ITAL .Ni chakula kitokanacho na mimea sio wanyama (vegetarian) na hakiungwi chumvi.

Rasta hatakiwi kukata nywele na akina mama hutakiwa kuzifunika ili zisionekana hadharani,wanazo sheria na kanuni kali kuhusu wanawake.Matharani mwanamke alie katika siku za hedhi hatakiwi kuguswa na wanaume wala hatakiwi kupika chakula .

Imani ya Rastafara inaruhusu ,inaendekeza na kutukuza uvutaji wa Bangi (Ganja).Rasta wanaamini kuwa ganja au bangi inasaidia kusafisha akili,kutafakari na kuchambua mambo.Rasta hawaamini kama kuna kifo ,wanaamini kuwa mtu hafi bali anahama tu. ‘Mungu hawezi kukunyang'anya zawadi kubwa ya uhai aliyokupa yeye mwenyewe'.Wanasema Rasta.

Katika imani ya Rastafara ,hayati mfalme Haile Selassie wa E thiopia alikuwa Jah Rastafara ambaye kwa tofasiri ya moja kwa moja ni ‘Umbo' la Mungu Duniani (Picha ya Mungu Duniani).

Kijadi Rasta walikuwa ni watu wanaotengwa tengwa sana katika jamii ya Jamaica.Hii inatokana na sheria zao ngumu,imani zao za kidini zilizo wasuta wanafiki,mtazamo wao wa kisiasa ulio wapinga watawala wanasiasa na mabepari pia wakoloni na tabia yao ya kuvuta Bangi waliitukuza mno.

Walipigania sana Ganja ihalalishwe,wamekuwa wakiitwa ‘wachafu' ,watu wenye nyoyo nyeusi nk.Lakini hapana anaye ukataa ukweli kuwa umeupanua na kuudumisha utamaduni wa waliowengi nchini Jamaica.Wala hapana ukweli .

Sanaa hiyo ambayo bila shaka huko Caribean pia wanajivunia na hakika wameifanya Jamaica ijulikane kote kote.Wameibeba Regae na kuisambaza Dunia nzima .Na muhimu kuliko yote hapana anaye pinga ,awe adui au rafiki kuwa Rasta wamekuwa wakipigania haki na uhuru pasipo kuchoka.

Pia alikuwepo Marcus Garvey ambaye ni mmoja wa Rastafari waliokuza sana urasta na ndiye aliyependekeza sare inayotumika kwa marastafari,yeye kuliko Rasta yeyote,ndiye aliye endeleza imani na hamu yao ya kuirudia asili yao ama kimwili au kinadharia .

Marcus Garvey,mjamaica aliyezaliwa huko St.Ann's ambako Bob alizaliwa pia,alikuwa mtetezi mkubwa wa haki na usawa Duniani.Aliona kuwa mtu mweusi anadharauliwa na kuonewa ,ananyanyaswa na kudhurumiwa ,Garvey alimpigania sana mtu wa hali hiyo.

Aliuchukia ukoloni na alipigana kwa kila hali aliyoweza kuupinga .Imani yake ilikuwa kwamba siku mojakama ingebidi, mtu mweusi angechukua silaha na kujikomboa. Mwaka 1922 wakati wakoloni wa kiingereza walipo wachinja ovyo waafrika huko Kenya.

Marcus garvey alimpelekea simu waziri mkuu wa uingereza simu hiyo inakumbukwa sana.Katika simu hiyo ya tarehe 20 March 1922 Garvey,kwa niaba ya watu weusi milioni mia nne.Garvey alikuwa kiongozi katika Universal Negro Improvement Association.

Alimweleza waziri mkuu wa uingereza aliyeitwa David Lloyd George kuwa serikali yake ilikuwa ikifanya vitendo vya kinyama huko Kenya ambavyo kila mnegro alivilaani,wazalendo wa Kenya walikuwa wakiuawa hovyo katika nchi yao wenyewe baada ya kudai haki zao kama binadamu.

‘Ni siasa gain hiyo? Alihoji Marcus Garvey katika simu hiyo. ‘Inazidi kuongeza lundo la dhuruma za kihistoria ambazo mtu mweusi ametendewa naye siku moja atamka kikweli si kwa fimbo,rungu na mawe tu bali kwa silaha bora za kileo'.Alieleza kwenye simu hiyo.

Haya.Mambo hayo! Ebu turudi tena upande wa Bob Marley. Japo Bob alichukizwa na siasa nchini mwake na kuwalaani wanasiasa hasa kutokana na matendo hayo,yeye mwenyewe alikuwa mwanasiasa mkubwa .Uchambuzi unaonyesha kuwa alichokilaani Bob kilikuwa mfumo wa maisha ya uonevu.

Mfumo huo huo ulitawala si Jamaica tu,bali sehemu nyingi duniani alisema anawachukia wanasiasa kwa sababu aliwaona wanapanda majukwaani huku wakiwaongopea wananchi .Aliuchukia unyonyaji aliouchukia ukandamizaji wa kiuchumi na kiutamaduni.

Bob aliuchukia sana ulaghai na ndio sababu ambazo zilimfanya akorofishane na mameneja wengi wa studio kadhaa kwa sababu walitaka kujinufaisha kupitia mgongo wa Bob hali ambayo ilimfanya atoe kibaop cha BAD CARD kilichomsuta Coxsone Dodd na Don Taylon.

‘Don alikuwa mjanja sana …mi sipendi watu lagjhai,kwa nini asiambiwe ukweli kuwa anataka vitu fulani kwangu'.Alisema Bob alipohojiwa

Bob hakuwa mpenda makuu ,alijali sana upatikanaji wa maakuli,malazi,mavazi na usafiri.Bob,baada ya kupata hayo ambayo aliyaona ni ya msingi,bila kutamba wala kujitangaza kitamaduni bila kumkomboa kiuchumi ni kupiga ngoma msituni.

Sawa na kwamba ikiwa ni sehemu kubwa ya jamii ya kike itaendelea kuwa chini ukilinganisha na wanaume,nafasi nyingi zaidi za kazi na kujiendeleza kimaisha zitaendelea kuwatendea wanaume,ikiwa mfumo wa maisha utaendelea kuwa ule wa mama ‘kuhudumiwa' na baba.

Na baba ‘kuhudumia', ni uwongo kusema usawa utapatikana na hata kama kila mwanamke Duniani atahitimu shahada ya juu ya upigaji kelele.Ukombozi wa mwanamke ,kimsingi ni suala la kiuchumi na sio hisia au mila .Mfano ni huko Bara la Hindi mila za huko zinaruhusu wasichana ‘kuoa'.

Yaani wasichana wa huko ndio wanao paswa kughalamia shughuli za harusi na ndiye anayetoa mahali, lakini kwa kuwa kiuchumi huyo mama anakuwa chini ya mumewe na aghalabu kumtegemea mumewe, huko ‘kuoa' kunaisha siku hiyo hiyo.

Baada ya hapo mwanamke anaanza maisha ya wasi wasi kutokana na kuendeshwa na bwana na wakweze.Kesi za wanawake walio na wanaume kujiua huko ni nyingi kuliko sehemu yoyote duniani.

Na wala ukombozi haumanishi kuwa bwana ni mchimbaji mgodi na bibi mpiga mashine wabadilishane haumaanishi kuwa mwanamke awe na msuli kama mwanaume au mwanaume awe laini kama mwanamke, kama baadhi ya ‘watetezi' wanavyodai bila kujijua.

Marley aliwapenda wanawake ,na hasa wanawake wa tabaka la chini ,la wakulima na wafanya kazi wa kipato cha chini ,wanawake wa tabaka hili aliwafahamu yeye zaidi,walikuwa hasa wanawake weusi.Ndio maana katika wimbo wake wa No Woman No Cry tunaona wazi msimamo wa kisiasa wa Marley .Haimbi tu kuhusu mwanamke yeyote,anaimbia mwanamke wa tabaka lake,mwanamke mweusi.Basi anazungumzia habari za kuni,habari za ugali …hivi ni vitu anavyojua mama wa tabaka la chini.

Kijijini au katika ghetto,na sio mama wa kibepari Los Angels au Tokyo,kasha anawaambia hao Sisthren(kina dada) akisema ‘every thing is going to be alright'akiwapa moyo na matumaini kuwa mambo yatakuja kuwa mazuri.

Ana wajaza hamasa na kuwaonyesha utamu wa maisha na uhai.Anaonyesha mapenzi na heshima zake kwao,katika wimbo wa ‘No Woman No Cry' na ‘John was a good man'zinaonyesha heshima na mapenzi makubwa kwa wanawake.

Sihayo tu ambayo Bob aliiyafanya wakati wa uhai ,wake alikuwa anajihusiha pia na michezo kama vile mpira miguu walipokuwa ziara ya ulaya ,Bob alikuwa na Bendeji mguuni lakini hakuonyesha wasiwasi tokana na jeraha alilolipata siku alipocheza mpira wa miguu.

Marley alipokuwa jukwaani alirukaruka jukwaani huku na huko kama mtu asiye na jeraha mwilini pake alifanya mazoezi ya viungo kama kawaida alikimbia kutoka studio na kuingia uwanjani kusakata kabumbu na mara kadhaa alionekana akikimbia mchaka mchaka.
Uvumi wa kutisha ukazuka kwamba mguu wa Bob Marley ulikuwa ukioza na ingebidi ukatwe.Baadae wakathibitisha kuwa wasingehitaji kuukata ,Marley angeendelea kuwa yule yule mwenye mwili mkakamavu,mcheshi ,mchangamfu,mchezaji ,mwanamuziki aliyeyumba na kutamba na kurukaruka jukwaa zima kama kawaida yake siku zote.

Lakini ku8mbe kulikuwa na ukweli wa kutisha mno,kansa ya Melanoma ambayo iliendelea kumla ikiyaharibu maini na mapafu yake hadi alipoanguka wakati akikimbia mchaka mchaka (jogging) katika Central Park ,baada ya kupiga katika The Comodores katika midson Sqare Gardens New York.

Bob Marley akalazwa katika hospitali iliyoitwa Sloan Carttering Hospital ya jijini New York.Uchunguzi mkubwa ukafanywa na matokeo ya uchunguzi huo yalithibitisha ukweli wa kusikitisha kuhusu afya ya Bob Marley.

Baada ya hapo Bob ‘akatoweka'.Uvumi ukaenea kuwa amekwenda zake huko SHESHAMANE nchini Ethiopia,huko Sheshame ni sehemu maalumu kwaajili ya wenye imani zqa Kirasta.Bado tunakumbuka kuwa Marley aliwahi kwenda huko mnamo mwaka 1978.

Lakini Marley hakuwa Ethiopia .Alikuwa amekwenda huko Bad Wiese,Ujerumani Magharibi ambako alilazwa kwaajili ya matibabu katika hospitali mashuhuri kwa magonjwa ya Kansa (Sun shine House Cancer Clinic) .Hapo alikuwapo daktari mashuhuri wa maradhi kama ya Bob.

Daktari huyo alikuwa anaitwa Josef Issels ambaye alikuwa akimpa matibabu ya hali ya juu ikiwa ni pamoja na kumpatia mgonjwa vyakula maalumu na matibabu ya mionzi.

Kwanza ,Bob alipofika hospitalini hapo tayari alikuwa na uvimbe katika ubongo na alikuwa hawezi kutembea,alikuwa hoi bin taabani.Lakini wiki chache tu baadae ,alikuwa anaweza si kusimama tu bali hata kutembea tembea na kuonana na watu.

Lakini kansa ilimjia vibaya .Siku zilipita bila kupona .Nafuu aliyowahi kuipata haikuwa ya kupona,wala haikuwa njia ya kuelekea kwenye afya njema.

Hali ikazidi kuzorota,ukafikia wakati ambao yeye mwenyewe na daktari wake wakatambua kuwa alikuwa mtu wa kutoka.Alipotambua kuwa mauti yake yamekaribia ,Bob akaamua kufunga safari ya kurejea Jamaica ili akafie huko.

Maskini ,kinyume na alivyopanga Bob,ili afike Jamaica akiwa hai ,badala yake alifika huko akiwa ni marehemu kwani alifariki akiwa katika hospitali moja ya Florida tarehe 11 mwezi Mei mwaka 1981.

Itakumbukwa kwamba katika uhai wake Bob,viongozi wa mfumo wa Babylone daima walipingana na Marley.Walimpiga vita na kuinunia Regae.Wakati akiwa taabani kitandani walimtambua,ni wakati huu ukweli ulipoibuka na kushinda.

Wakamtambua rasmi ,wakampatia nishani ya heshima ya Order of Merit .Hii ilikuwa kabla ya kifo chake,ilikuwa mwezi machi 1981.Kabla ya kufariki Marley alikuwa amekubaliwa katika kanisa Orthodox Church la Ethiopia-The Ethiopian Orthodeox Church kasha akapewa jina la Berhane Sellasie.

Mwili wa Bob Marley ukapelekwa Kingstone kwa ndege kutoka Miami.Ibada ya kumuaga ilfanyika katika lugha nne ambazo ni lugha ya taifa ya Ethiopia iitwayo Amharic na Geez ambayo ni lugha ya zamani ya kidini huko Ethiopia.

Zingine zilikuwa ni lugha za kiafrika na kiingereza,viongozi wa kisiasa akiwemo waziri mkuu wa Jamaica Edward Seaga walitoa heshima zao .Wanasiasa ni watu ambao Bob katika uhai wake alikuwa amewakemea na kuwasuta mara nyingi sana.

Marehemu akapelekwa katika medani ya taifa (National Arena) sehemu kubwa ambayo awali iljengwa kwaajili ya michezo ya Common Wealth,hapo maelfu ya watu walikusanyika kumuaga shujaa wao,polisi walijaa tele wenye mfumo wa ki-babylone ambao hawakupata kuwa marafiki wa Bob Marley.

Agharabu polisi hao waliwatawanya vijana waliojawa hisia na uchungu kwa gesi ya machozi.Haikuwa rahisi kupata utulivu na nidhamu waliotaka polisi,nao kama kawaida ya askari wa mfumo huo wakatumia nguvu.

Muziki wa Bob ukasikika kwenye kanda huku watu wakipita pembeni mwa jeneza lililohifadhi mwili wa marehemu Bob wakitoa heshima zao za mwisho kwa mwanamuziki huyo mpiganaji wa ghetto.Halafu The Wailers wakapiga muziki wa kidini na Microphone ilishikwa na Bibi Cedeller Booker.

Bibi huyo ndiye mama mzazi wa Bob aliimba kwa sauti iliyotetemeka iliyopanda na kushuka .Ziggy na Steve ambao ni watoto wa Bob wakaamka jukwaani,wakaimba nyimbo walizo kuwa wamefunzwa na baba yao, ‘1 Threes walikuwapo pia ,waliimba kwa simanzi.

Halafu safari ikaanza kuelekea Nine Miles kijijini aliko zaliwa Marley katika jimbo la Ann's.Peter Tosh na Bunny Wailer hawakuhudhuria ,Bunny ni mtu asiye amini sherehe za mazishi na ukweli ni kwamba rasta hawakichukulii kifo kama ilivyo jamii isiyo ya kirasta.

Bunny ni mtu anaye ping asana maombolezo ya msiba ,haileweki kwa nini Peter hakuhudhuria lakini Don Taylor ambaye alikuwa meneja wa The Wailers hatimaye kukorofishana nao alihudhuria na alifanya kazi kubwa ya kuifariji jamii ya marehemu tena akatoa na msaada aliouweza.

Rita Marley walipofika huko Nine Miles alisema ‘hapa ndipo mahali nilipopitishia miaka sita nikiwa na Bob na hapa ndipo nilipo zaa mtoo wetu wa kwanza aitwaye Ziggy.

Barabara kuu itokayo mjini Kngstone ilikuwa ikiitwa Washington Boulevard ndiyo iliyotumika kuusafirisha mwili wa hayati Robert Nesta Marley,ilikuwa haipitiki,watu walisongamana,msululu wa magari ulikuwa na urefu wa kilomita kadhaa.

Safari ikaenda taratibu huku vipaza sauti vilivyokuwa kwenye magari vikitoa sauti za muziki wa Bob Marley.Barabara hiyo sasa imepewa rasmi jina la Bob Marley Boulevard badala ya Washington Boulevard.

Huko kijijini kwao alikozikwa , kaburi lilipewa nafasi nzuri na mahali pa pekee ambapo katika uhai wake Marley alipendelea kuketi na Rita huku wakijadili mambo mbali mbali usiku huku wakisikiliza muziki na kuangazwa na mbaramwezi au wakizitazama nyota.

Takribani mita mia moja kutoka eneo hilo,ndipo alipozaliwa Bibi Cedeller Booker.Shujaa Robert Nesta Marley(Barhane Sellesie) mwasisi wa soul,The Trench Town Experience,mwana wa Ragae vilevile mpiganaji kutoka Gheto akapumzishwa.
 
Alikuwa ni mtu!!!!!
Aliyeandika kwa maisha na.maisha yalimfanya aandike!!!!

May his soul rest in peace!!!!
 
tutamkumbuka daima nyimbo zake zina Message nzuri sana kama
Emancipate yourselves from mental slavery, none but ourselves can free our minds
 
Rub, rub, rubby-doo-day; Rum-pum-pum a-rum-pum-pum-pum! Dready got a job to do And he's got to fulfill that mission To see his hurt is their greatest ambition, yeah! But-a we will survive in this world of competition, 'Cause no matter what they do Natty keep on comin'through, And no matter what they...
 
Back
Top Bottom