Candid Scope
JF-Expert Member
- Nov 8, 2010
- 11,890
- 6,896
Picha: Askari wa Jimbo la Macau wakiwadhibiti machangudoa waliokamatwa katika oparesheni maalumu.
Wakati wanawake kwa wanaume wengi huenda barani Asia, hasa China kununua bidhaa kwa ajili ya kuja kuzichuuza, hali sasa ni tofauti kwa kuwa kuna wasichana ambao huenda huko kwa ahadi za ajira, lakini huishia kufanya ukahaba kwenye madanguro, gazeti hili linaweza kukuthibitishia.
Wasichana hao hutafutwa na mawakala wa hapa nchini ambao kazi yao huwa ni kutafuta wasichana wazuri na baadaye kuwashawishi kwa kuwaeleza fursa za ajira za hotelini zilizo barani Asia. Msichana akikubali, wakala huchukua jukumu la kumtafutia viza ya kuingia China na baadaye kuwasiliana na mwenyeji wake, maarufu kama Lady Boss, ambaye hutuma tiketi ya ndege kwa ajili ya kumsafirisha ‘mwajiriwa' mpya.
Hata hivyo, hali hubadilika mara wafikapo huko kwa kuwa ‘mwajiri' huyo humpokonya hati ya kusafiria na baadaye kumpa maelekezo kuwa atatakiwa kulipa Dola 200 kila siku ambazo atakuwa akizipata kwa kufanya umalaya kwenye klabu na maeneo ya biashara.
Tayari wasichana kadhaa wa Kitanzania wamenaswa katika mtego huo na kujikuta wakilazimika kuuza miili yao ili wamudu ada ya Dola 200 pamoja na fedha za kujikimu, akiwemo Munira Mathias mwenye umri wa miaka 23 ambaye alimudu kuvaa ujasiri wa kuweka bayana uovu huo katika mazungumzo yake na gazeti hili.
Binti huyo Mtanzania aliyesafiri kwa saa 18 kwenda Guangzou, China alitakiwa kupumzika kwa saa mbili tu kabla ya kupelekwa kuanza ‘kazi' ambayo hakuitarajia. "Baada ya kupumzika kwa saa mbili tu, nilipelekwa kwenye klabu," anasema Munira wakati akisimulia mkasa wake. "Sikuwa na kazi nyingine zaidi ya kucheza muziki na wanaume ambao licha ya kwamba sikuwahi kuwaona, walinichangamkia kama vile wananifahamu."
Munira aliondoka Januari mwaka huu kwenda China ambako aliahidiwa kuwa angeajiriwa hotelini, lakini alikutana na ‘ajira' ya ukahaba, huku akilazimika kuwalipa ‘waajiri' wake Dola za Marekani 200 kila siku. Binti huyo, ambaye alifanikiwa kuchomoka mikononi mwa waajiri hao baada ya viza yake kuisha, alisema kwa siku 91 alizokaa China, alipata mateso ambayo hatayasahau ikiwamo kupigwa, kubakwa na kundi la wanaume raia wa Nigeria, pia kulazimika kutoa mimba aliyoipata kwa kubakwa.
"Nilifika Guangzhou kama saa 9.00 alasiri za China na kulikuwa na baridi sana," anasema Munira akisimulia jinsi alivyokanyaga kwa mara ya kwanza ardhi ya nchi hiyo akiwa na matumaini ya kuanza maisha mapya. "Wakati huo nilikuwa nikijaribu kupata mawasiliano na mwenyeji wangu ambaye niliagizwa kutoka Magomeni, Dar es Salaam.
Alisema alipotoka Dar es Salaam aliambiwa angepokewa na mtu anayeitwa Jacky ambaye hakumkuta kwa kuwa alikuwa safarini Malaysia, lakini alikuwa ameacha maagizo apokewe na mwanamke mwingine. "Nilielekezwa nikodi taksi hadi kwenye hoteli inayoitwa Nairobian. Kutoka hapo uwanja wa ndege hadi kwenye hiyo hoteli ni sawa na umbali wa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam hadi Bagamoyo," anasema Munira.
Anasema alitakiwa kulipa Yuan 200 (Sh60,000) na alipofika katika hoteli hiyo alipokewa, akaoga na kupewa chakula. "Nilipomaliza kula nilipumzika kwa saa mbili hivi. Jacky alikuwa amesharudi na alinifuata chumbani na kuniambia natakiwa kwenda saluni. Hivyo tuliondoka pamoja hadi kwenye jengo kubwa lenye maduka makubwa linaloitwa Tin- shu," anasimulia Munira.
Watanzania lukuki
Katika jengo hilo alishangaa kuwaona Watanzania wengi, wakiwamo wanawake kadhaa ambao aliwahi kukutana nao Magomeni wakati akifuatilia safari yake. Munira anasema miongoni mwa watu aliowaona ni binti mmoja ambaye wanafahamiana ambaye alistaajabu kumwona sehemu hiyo. "Aliniuliza kwa mshangao, ‘mbona umekuja huku? Umekuja kufanya nini?' Wakaanza kunishangaa. Yule msichana akaniambia ‘huku msala ndugu yangu, umekuja kufanya nini?" alimnukuu na kuongeza kuwa kabla hawajamaliza mazungumzo yao, mwenyeji wake alitokea hivyo waliyakatisha.
Anasema waliingia saluni ambako aliwakuta Watanzania na Wakenya wakifanya kazi humo na wakati yeye akiendelea kusukwa nywele kwa umaridadi, Jacky alikwenda kumnunulia nguo na viatu dukani. "Baada ya hapo niliambiwa nivae nguo niende klabu kwa sababu huo ni msimu wa sikukuu za mwaka mpya wa Kichina," alisema Munira.
Anasema alishangaa kuambiwa aende klabu usiku huo wakati alikuwa amechoka kwa safari ndefu. "Kilichokuwa kinanipa moyo usiku ule ni kuwa niliwaona wasichana wa Magomeni, lakini nilihisi wameambiwa wasiwe karibu na mimi." Anasema alipoingia klabu, pia alishangaa zaidi kukutana na Watanzania wengi wa rika tofauti ambao baadhi yao aliwatambua kwa sura na pia kulikuwa na raia wengi wa Nigeria.
"Kiasi fulani nilifarijika kuwaona Watanzania na nilijisikia kukua kiakili baada ya kuwaona Wanigeria ambao nilizoea kuwaona kwenye filamu peke yake," anasema. Hata hivyo, alishangaa kuona pale klabu alichangamkiwa na watu wengi, lakini hakutaka kudadisi zaidi bali alidhani ndiyo hali halisi au alikuwa na bahati ya kupendwa. "Baada ya kumaliza kucheza muziki kwenye klabu hiyo, walipelekwa kwenye klabu nyingine ya asubuhi.
"Tuliporudi hotelini, nilijitupa kitandani na kulala kwa sababu ya uchovu mwingi. Miguu ilikuwa imevimba kwa sababu nilikuwa nimevalishwa viatu virefu na kucheza muziki mfululizo. Nikalala bila ya hata kuoga," anasema.
Mwanzo wa mateso
Baada ya saa moja kupita na akiwa amelala fofofo mchana ule, mara aliamshwa na Jacky, ambaye alimwamuru amkabidhi pasipoti yake. "Nikampa, pasipoti yangu nilikuwa nimeiambatanisha na tiketi na kila kitu. Akanishangaza kuniambia kuwa kuanzia siku hiyo niwe nampelekea Dola 200 mezani kila siku. Nilishangaa na nikaanza kulia," anasema.
Kwa hasira na mshtuko alioupata, Munira anasema alitoka nje na kuanza kulia na wenzake walipomuuliza kinachomliza, aliwaeleza. Waliamua kumwambia ukweli kwamba hata wao walipelekwa kwa miadi ya kupata ajira za hoteli, lakini hawafanyi hivyo. "Waliniambia kuwa nao walirubuniwa na wakanyang'anywa hati za kusafiria kama mimi na wakaishia kuambiwa wafanye biashara ya kuuza miili ili watafute fedha," anasema Munira.
Munira anasema alichanganyikiwa, hasa pale alipoambiwa na wenzake kwamba kazi kubwa ni kwenda klabu kujiuza au kuzurura eneo la Chambu Chambu. Chambu Chambu ni soko la bidhaa ambako wasichana hujifanya wananunua vitu, lakini kimsingi huwa wanakwenda kutafuta wateja wa ngono. "Kule wanaume wameshajijengea picha kuwa wanawake wa Kitanzania wapo kwa ajili ya kujiuza, basi wakikuona tu wanakufuata na mnaongea biashara, mnakwenda kumalizana," anasimulia.
Wasichana wenzake wa Kitanzania walimwambia kuwa hayo ndiyo maisha yenyewe, hivyo aliporejea ndani, mwenyeji wake (Jacky) alimwambia ajiandae kuanza kazi mara moja na Munira akawa hana budi kufuata maelekezo.
Baada ya hapo aliingia bafuni akaoga, kisha akaenda eneo la Chambu Chambu kutafuta wateja. "Nikakubaliana na hali halisi nikawa nafanya kazi kama nilivyoambiwa. Niliona nikubali lakini akili kichwani mwangu ilikuwa nifanye mbinu ili nirudi nyumbani," anasema
eep: eep: eep:
Minira abakwa na Wanaijeria
Munira baada ya kuamrishwa na ‘bosi' wake kufanya kazi hiyo, alielekezwa na wenzake kwenda eneo la soko liitwalo Chambu Chambu ambako wanawake Watanzania wanafahamika kuwa maarufu kwa biashara ya ukahaba. Binti huyo mwenye umri wa miaka 23 anasema usiku wa kwanza alipokwenda sokoni Chambu Chambu, wenzake walimkimbia, hivyo alichanganyikiwa na kuanza kuwapigia simu wenyeji wake kwani hakujua la kufanya. "Nilimpigia simu Jacky na yeye alinijibu, ‘acha ujinga, tafuta hela uniletee mimi." Anasema katika mazingira hayo alianza kulia na wakati akilia, alikutana na mwanaume wa Kinigeria, ambaye alimhoji maswali kadhaa.Minira abakwa na Wanaijeria
Mnigeria yule alisema anaifahamu hoteli anayoishi Munira, lakini alimtaka wazungumze kwanza biashara kisha ampeleke na Munira alikubali. "Nilizungumza naye biashara na tukakubaliana twende kwenye hoteli niliyofikia, baada ya kufanya mapenzi akanilipa Dola 100, baadaye nilidakwa na mwenyeji wangu akinitaka nimpe fedha zote nilizopata," anasema. Alipomkabidhi fedha hizo, aliamrishwa kurudi tena sokoni kutafuta kiasi kingine cha fedha hadi atimize dola 200. Wakati huo bado ulikuwa ni mchana. "Baada ya kumalizana na Mnigeria yule, nilienda kulala, lakini sikulala sana kabla mwenyeji wangu hajaniamsha na kuniambia lazima nitimize Dola 100 iliyobaki, hivyo nikanyanyuka na kwenda tena sokoni," anasema.
Munira akawa hali wala halali vizuri akifanya kazi ya kujiuza mwili wake, kazi ambayo hata kiasi kidogo alichopata alitakiwa kugawana na mwenyeji wake kwa kumpatia Dola 200 kwa siku. "Nilikuwa nachoka, hasa kwa kudaiwa, wakati mwingine nikiwa kwenye siku zangu najiuliza nitafanyaje ili nipate fedha za kulipa deni? Niliondoka hapa nikiwa na afya, lakini nilipofika huko baada ya muda mfupi niliisha, yaani niliisha," anasema.
Ukatili wa aina yake
Anasimulia kwamba, siku moja saa 10.00 usiku akiwa klabu, alijisikia vibaya akatoka nje, akiwa huko alikutana na mwanamume ambaye walikubaliana wakastarehe kwa ujira fulani. Munira alikubali, lakini alijua kabisa kuwa anakwenda sehemu ambayo haifahamu kabisa. Baadaye aligundua kuwa eneo hilo linaitwa Nan-hai na linaongoza kwa matukio mengi ya uhalifu. Anasema walikubaliana na mwanamume huyo wa Kinigeria na alikaribishwa na kuingia ndani katika nyumba yenye vyumba vinne, alipomuuliza iwapo anaishi peke yake, mwanamume huyo alimhakikishia kuwa anaishi peke yake. "Nikamwambia nataka kiasi fulani, tukakubaliana niende Nan-hai, sehemu yenye matukio ya ajabu. Ni nyumba nzuri kwa kweli, nikaingia ndani, nikaoga," anasema.
Baadaye Munira aligundua kuwa yule mwanamume anaishi na wenzake, wakati wanafanya tendo la ngono, alishangaa mwanamume mwingine anaingia chumbani na wote mmoja baada ya mwingine walimwingilia. "Kwa kuwa nilikuwa nakataa kufanya walichotaka, walinipiga sana na ikabidi nikubali, hawakuniachia waliendelea kunibaka hadi kesho yake Saa 1.00 jioni, niliumia sana," anasema. Walimnyang'anya fedha alizokuwa nazo na walipomuachia, mmoja kati ya wanaume wale alimpa Munira Yuan 100 na kumwambia hiyo ni nauli yake. "Sikuelewa alikuwa na huruma au dharau?" anasema Munira.
Munira anasema kuwa alichukua gari na kumpigia simu rafiki yake, ambaye alimpokea na walipoingia ndani alimsimulia kisanga kilichomkuta na kwa pamoja wakaanza kulia. "Rafiki yangu alinipeleka hospitali ambako nilipigwa ultra- sound na x-ray, ikaonyesha jinsi nilivyoharibiwa kwa kiasi kikubwa." "Nikachomwa sindano za mishipa na kutundikiwa dripu, nilichomwa pia sindano za kuzuia maambukizi ya Virusi vya Ukimwi," anasema.
Akiwa hospitalini hapo, Munira alikutana na mwanamume mmoja Mnigeria ambaye walizoeana kwa muda aliokuwa hapo Guangzhou. Mwanamume huyo alipenda kumwambia Munira kuwa anafanana na mke wake. Hata hivyo, Munira hawakumwambia Mnigeria huyo nini anachoumwa na badala yake walimdanganya kuwa anaumwa malaria. "Alikubali akanisaidia kulipa bili ya hospitali, akaninunulia chakula na kunipa fedha nyingine ya ziada," anasema.
Kutokana na mateso hayo, aliamua kumpigia simu Josephine wa Magomeni (aliyemfanyia mipango ya kwenda huko) kumwuliza kuhusu kazi yake, lakini Josephine alimtia moyo kuwa eti hoteli nyingi zimefungwa hadi msimu ujao. "Kumbe kile nilichoambiwa na wenzangu kwamba kazi ni ukahaba, kikawa ndiyo hicho, niliamua kumwachia Mungu," anasema.
Atuma picha
Akiwa hospitali, Munira alijipiga picha akiwa na majeraha aliyokuwa nayo na kuitumaWhatsApp kwa baadhi ya watu ambao katika kutumiana ujumbe huo, hatimaye taarifa zilimfikia mwenyeji wake, Jacky. "Aliponipigia simu hakuchukua hatua nyingine zaidi ya kuniuliza nipo wapi. Nikamwambia nipo hospitali, basi akakata simu na wala hakutaka kujua zaidi kilichonisibu," anasema.
Aliporudi hotelini, Jacky alimwambia hataki kusikia suala lolote na wala hajali kama alikuwa anaumwa zaidi ya kutaka Dola 200 kila siku iendayo kwa Mungu. Mwanadada huyo anasema kutokana na mateso hayo, alikonda kiasi kwamba, ulipofika wakati wa kuongeza muda wake wa viza, (alikuwa ana viza ya mwezi mmoja), sura yake ilibadilika na ilitofautiana na picha iliyokwekwa kwenye viza. Kwa bahati nzuri aliongezewa muda wa kuishi China kwa siku 14 zaidi ili ajitayarishe kutafuta kibali cha kuishi.
"Nilishangaa kusikia kwamba natakiwa niweke hela ya viza, kiasi cha Dola 300 na kiasi kingine Dola 200 za kumlipa mwenyeji wangu, wakati aliahidiwa kuwa atalipiwa kila kitu ikiwamo visa na malazi," anasema. Wakati huohuo, alitakiwa kulipia hoteli, ajinunulie chakula, atafute fedha ya viza, zile Dola 200 za kumpa mwenyeji wake nazo zikabaki pale pale.
Viza inakwisha
Wakati hayo yanaendelea muda ulikuwa unapita na wiki mbili za nyongeza ya viza yake zilikuwa zinayoyoma. Anasema ilikuwa ni bahati nzuri kwake kwani mteja wake mwingine pia mwenye asili ya Nigeria alimsaidia na kumpa fedha za kuongeza muda wa kuishi hapo Guangzhou. Hata hivyo, alipokwenda kuongeza muda wa viza yake, alikutana na changamoto mpya pale maofisa uhamiaji, walipomwambia kwamba hawezi kupata kwani sura yake halisi ilikuwa inatofautiana kwa kiasi kikubwa na picha iliyopo kwenye viza, hivyo walimnyima kibali. Wakati huo, muda wa viza yake ilikwisha kabisa na sasa alikuwa akiishi katika nchi hiyo kinyume cha sheria.
Jana katika tovuti hii, binti huyo ambaye tulimpa jina bandia la Munira Mathias kutokana na sababu za kitaaluma, alieleza kwamba baada ya mateso mengi, viza yake ya kuishi China iliisha muda wake na alikuwa akiendela kuwapo katika mji wa Guangzhou kinyume cha sheria.
Wakati anasumbuka na masuala ya viza, alihisi kuwa na hali isiyokuwa ya kawaida, aliamua kununua kipimo cha ujauzito cha bei nafuu. Kwa bahati mbaya aligundua kuwa alikuwa mjamzito ambao anahisi kuupata siku alipobakwa na Wanigeria wanne.
Munira anasema suala la yeye kushika ujauzito lilileta shida zaidi, kwani mwenyeji wake, Jacky alimweka kikao na kumsuta kwa hilo bila kujali kuwa alibakwa. Mmoja wa wanawake hao ambao walikuwa wakifahamika kama ‘Boss Lady' alimshauri kuwa atamtafutia mwanaume ambaye atamsaidia kutafuta daktari ili watoe mimba hiyo.
Alipofika kwa daktari, alipewa vidonge tisa ambavyo alitakiwa kulipia Yuan za China 600 (zaidi ya Sh100,000). Hakuwa na fedha hivyo alitakiwa kuendelea kujiuza licha ya kuwa hakuwa amepona ili apate fedha hizo. "Baada ya muda nilipata fedha hizo na nilipewa vidonge, ambavyo hata hivyo haviharibu mimba kwa wakati huohuo bali taratibu sana," anasema Munira.
Muda wa kuishi Guangzhou ulikuwa umekwisha na Munira hakuwa amepata viza, ilimbidi aondoke. Lakini mwenyeji wake alimwambia ni lazima atafute fedha ya kulipia viza usiku uleule. Akimaanisha akajiuze usiku huo na kupata fedha kwa ajili hiyo. Munira alilazimika kuingia mitaani usiku ule kusaka wateja kwa ajili ya kupata fedha za kwenda kuchukua viza hiyo Macau, jimbo jingine maarufu nchini China.
Mwenyeji wake alimwambia wakati anaondoka asubuhi siku inayofuata, asiondoke bila kumuaga. Aliporejea usiku wa manane alijiandaa kwa ajili ya safari ya asubuhi yake, licha ya kwamba hakuwa amepata fedha za kutosha. Kulipopambazuka alikwenda kumuaga mwenyeji wake kama alivyoambiwa, lakini alishangazwa na kitendo cha mwenyeji huyo kumnyang'anya baadhi ya vitu kama nguo na viatu alivyomnunulia wakati alipofika nchini humo.
Wakati akiondoka alisindikizwa na Mtanzania, msamaria mwema, ambaye alimpa Dola 400 za Marekani kama akiba na nauli ya Yuan 50, hivyo kuongezea katika fedha alizokuwa amepata usiku ule.
Macau ni ‘Boda la JK'
Munira alichukua treni ya kuelekea Macau, mpakani lakini aliambiwa akiwa huko anatakiwa atoke kwa saa 12 kila baada ya miezi mitatu ili atakaporudi, aanze kuhesabiwa tena siku za kuishi.
Macau ni jimbo ambalo Watanzania wanapata msamaha wa kukaa kwa siku 90 bila viza, hivyo mara nyingi siku zinapokaribia kuisha, Watanzania katika jimbo hilo huondoka kwa saa 12, kisha kurejea kama wageni ambao huanza kuhesabiwa siku zao upya. Kutokana na urahisi huo wa kimaisha, Macau umebatizwa jina na Watanzania ambao wanauita ‘Boda la Kikwete', wakimaanisha kwamba maisha yao katika jimbo hilo ni kwa hisani ya makubaliano baina ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete na Serikali ya China.
Wakiwa Macau, Watanzania huenda kuchukua viza nchi jirani ya Malaysia, kinyume na hapo hubaki Macau, wakisubiri majaliwa ya kupata viza au kurudi nyumbani. "Nilipofika Macau nilipata shida, Wachina hawajui Kiingereza, nazunguka na begi langu, kumbuka bado sijapona baada ya kufanyiwa ule unyama," anasema.
Anasema alifanikiwa kuvuka mpaka wa Macau kutoka Guangzhou, ingawa alipata shida kupita katika viunzi vya uhamiaji kutokana na sheria za China. Akiwa hoi kwa kuchoka, alikutana na raia wa Somalia ambaye alimsaidia kujaza fomu, lakini hata hivyo hakuweza kumsubiri, hivyo Munira alibaki peke yake.
"Nilipofika katika kiunzi cha mwisho cha uhamiaji, nilihojiwa sana, maofisa uhamiaji walidai kuwa sura yangu ya sasa haifanani na iliyopo kwenye hati ya kusafiria, hivyo wakawa na wasiwasi na mimi," anasema. Munira anasema maofisa hao walimuuliza maswali mengi kama namba ya pasipoti, umri, majina matatu, mambo ambayo aliyajibu kwa ufasaha, lakini bado hawakuridhika na wakampeleka kwenye chumba maalumu cha polisi kwa mahojiano.
Huko, walimwambia afumue nywele alizokuwa amesukia na kumhoji kwa zaidi ya saa moja kabla ya kumruhusu. Anasema ni kweli sura yake halisi ilikuwa imebadilika baada ya kukonda sana, kutokana na mateso aliyokuwa anayapata. "Mwisho wa siku waliniachia, nikachukue teksi, lakini ilinipoteza. Bahati nzuri mbele kabisa nikakutana na msichana raia wa Urusi, alichukua namba yangu na akanielekeza sehemu niliyotakiwa kwenda, huo ukawa mwanzo wa urafiki wetu," anasema.
Mjini Macau
Anasema alipofika eneo aliloelekezwa, katika hoteli kubwa iitwayo St Marol, aliwakuta wasichana wengi zaidi ya 200 wa Kitanzania ambao viza zao zilikuwa zimeisha muda.
Walikuwa ni wengi na wote walikuwa wanajiuza.
"Mji huo ni kama Zanzibar hivi. Ni pazuri na ni mji wa gharama sana kila kitu ni gharama, hata hivyo wateja hawakuwa wengi kama Guangzhou," anasema. Katika hoteli hiyo ya St Marol, wasichana 15 hadi 20 katika eneo hilo, huchangia gharama za chumba. Alishuhudia wasichana wadogo kuliko yeye, ambao walimlalamikia wakidai kuwa nao wanaishi maisha ya kujiuza ili wapate fedha kinachowakwamisha ni kukosa fedha za nauli ya kuwarudisha nchini.
Munira aliamua kuwasaidia, hivyo alishauriana na mmoja wao aitwaye Candy kwamba warekodi sauti kwenye simu wakieleza adha wanazopata, kisha wazitume Tanzania kupitia WhatsApp ili wapate msaada wa kurudi nyumbani.
Anasema ujumbe ule wa sauti ulisambaa karibu kwa Watanzania wote wanaoishi Macau, China, Guangzhou na Hong Kong na kwamba wezao wa Macau waligundua kwamba sauti hiyo ni ya mmoja wa wasichana wanaoishi kwenye hoteli hiyo ndipo walipoamua kwenda kuwasuta Munira na Candy chumbani kwako.
"Kundi la wasichana wa Kitanzania zaidi ya 100 walifika kwenye chumba chetu, wakaanza kutusuta kwa nini tuliamua kutuma ujumbe wa sauti kama ule." "Walitaka kunipiga wakidai kuwa nawaharibia maisha yao kwani wanapata pesa za kujenga nyumba na kununua magari kwa kazi hiyo," anasema.
Anasema yeye na Candy walipoona hali imekuwa mbaya, waliamua kukimbia. Munira kwa hofu, alibahatika kubeba hati ya kusafiria, tiketi na kadi ya manjano, akiacha nguo na baadhi ya mali zake. Hata hivyo, walipofika njiani, Candy alibadili uamuzi na kuamua kurudi hotelini. "Nilimshukuru Mungu kwa kunipa akili ya kuchukua vitu vitatu muhimu, nikampigia simu rafiki yangu Mrusi, ambaye alikuja kunisaidia na kunipeleka kuishi kwake.