ACT Wazalendo kimepokea malalamiko ya Watumiaji wa Bandari ya Malindi Zanzibar kuhusu kupanda kwa gharama za utoaji mizigo

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,989
ALLIANCE FOR CHANGE AND TRANSPARENCY (ACT WAZALENDO)

OFISI YA KATIBU MKUU

(PartysSecretaryGeneralOffice)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI​

Chama Cha ACT Wazalendo kimepokea kwa uzito wake malalamiko ya Watumiaji wa Bandari ya Malindi Zanzibar kuhusu kupanda kwa gharama za utoaji mizigo mara tu baada Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Dk. Hussein Mwinyi kukabidhi shughuli za Bandari hiyo ya Malindi kwa Kampuni ya African Global Logistics (AGL) kutoka nchini Ufaransa.

Itakumbukwa kwamba Chama cha ACT Wazalendo kupitia mikutano mbali mbali ya hadhara tulizungumzia na kupinga hatua ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Dk Hussein Mwinyi kubinafsisha Bandari ya Malindi Zanzibar kwa Kampuni ya African Global Logistics (AGL) kwani jambo hili lilionesha kila dalili ya kujaa harufu ya rushwa na ufisadi uliokubuhu.

Baada ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Dk Hussein Mwinyi kupuuza hoja zetu na za wananchi wa Zanzibar na kuamua kuendelea na msimamo wao wa kuikodisha bandari hiyo kwa kampuni ya African Global Logistics (AGL) kutoka Ufaransa katika kuendesha shughuli za Bandari ya Malindi katika suala la Utoaji na Upakuaji wa Mizigo, tayari wafanyabiashara, mawakala wa utoaji mizigo, wafanyakazi, wasafirishaji na watu wengine wanaotumia huduma za bandari wametoa malalamiko ya kupanda kwa gharama za utoaji na upakiaji mizigo bandarini hapo na gharama nyinginezo bila ya kuarifiwa wao kama wadau muhimu wa Bandari hiyo.

Chama Cha ACT Wazalendo tunaona ni wazi kwamba hofu zilizokuwa zimetanda miongoni mwa watu juu ya nia ovu ya ukodishaji wa Bandari hiyo sasa zinathibitika kuwa na uhalisia. Ni wazi kwamba ukodishwaji wa Bandari ya Malindi Zanzibar kwa kampuni ya African Global Logistics (AGL) kutoka Ufaransa haukuwa na nia njema bali ilikuwa ni kitendo cha kifisadi cha watu wachache kujilimbikizia mali kupitia mgongo wa Wazanzibari walio wanyonge na kufisidi mali zao.

Chama cha ACT Wazalendo tunaitaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Dk Hussein Mwinyi itoke hadharani na ijibu masuali yafuatayo:-

Ni kwa nini Ubinafsishaji huu wa Bandari ulifanywa kwa njia ya Siri?

Je, ni lini tenda ya ubinafsishwaji wa Bandari ya Zanzibar ilitangazwa, ni kampuni zipi nyengine ziliomba, ni utaratibu upi na vigezo vipi vilitumika mpaka kufikia kupelekea African Global Logistics (AGL) kukabidhiwa uendeshaji wa Bandari ya Malindi Zanzibar?

Kama suala lililopelekea Bandari ya Malindi kukodishwa ni kuongeza ufanisi na kupunguza gharama na urasimu, inakuwaje mara tu baada ya Kampuni ya African Global Logistics (AGL) ya Ufaransa kukabidhiwa uendesahaji wa Bandari imeongeza gharama za utoaji na upakuaji wa mizigo katika bandari hiyo kwa kiwango kikubwa sana, kuanzisha tozo kubwa kama zile za kuingiza magari yanayokwenda kuchukua na kupeleka mizigo bandarini na kuongeza urasimu?

Mwekezaji huyu wa African Global Logistics (AGL) kawekeza nini zaidi ya kuja kuwakamua wananchi wa Zanzibar na kufisidi uchumi wao? Kwa nini Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Dk. Hussein Mwinyi imetumia fedha za walipa kodi wananchi wa Zanzibar dola za kimarekani milioni 6 kumfungia mwekezaji mfumo wa e-Ports bandarini na kutumia kiasi chengine cha shilingi bilioni 16.5 kumuwekea mwekezaji vifaa vya kisasa vya upakiaji na upakuaji wa mizigo bandarini muda mfupi tu kabla ya kumkabidhi bandari hiyo? Huyu mwekezaji kawekeza nini zaidi ya kuja kuvuna faida kwa mradi aliokuwa hakuwekeza kitu?

Kwa kumuwekea mifumo na vifaa vyote hivyo kwa gharama hizo kubwa tulizozitaja, Wakubwa wa Serikali na washirika wao wana maslahi gani katika mradi huu usiokuwa na maslahi na wananchi wa Zanzibar?

Chama cha ACT Wazalendo tunalichukulia tendo hili la kupandishwa kwa gharama za Uendeshaji wa Bandari ya Mizigo ya Malindi Zanzibar ni tendo baya, ovu na ambalo linakwenda kuengeza gharama za maisha na kuwaongezea umasikini wananchi wa Zanzibar kutokana na mambo yafuatayo:-

Kufanya kupungua kwa mizigo inayoingia bandarini hususan bidhaa za chakula, kutokana na kupandishwa huko kwa gharama za Upakiaji na Upakuaji wa Mizigo hiyo.

Kufanya bidhaa kadhaa kuadimika hasa bidhaa zinazotoka nje ya Zanzibar na kupelekea mfumko wa bei.

Wafanyabiashara kuongeza gharama za bidhaa wanazoingiza kutokana na kufidia gharama iliyoongezeka Bandarini.

Kuyafanya maisha ya wananchi masikini wa Zanzibar kuzidi kuwa magumu kutokana na kupanda kwa gharama za bidhaa zitakazosababishwa na kupanda kwa gharama za bandarini.

Chama Cha ACT Wazalendo tunaitaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Dk. Hussein Mwinyi kufanya mambo yafuatayo ili kuondosha usumbufu na kadhia hii iliyoanza kujitokeza mara baada ya kuikabidhi Bandari ya Malindi Zanzibar kwa kampuni ya African Global Logistics (AGL) kutoka nchini Ufaransa:-

Tunaitaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Dk Hussein Mwinyi mara moja kusitisha Bei mpya za Utoaji na Upakiaji wa Mizigo na uingizwaji wa gari bandarini zilizotangaazwa na kampuni ya African Global Logistics (AGL).

Tunaitaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Dk Hussein Mwinyi kuitisha kikao na wadau wote wa masuala ya usafirishaji na uingizaji wa Mizigo Bandarini, Wafanyabiashara na kampuni ya African Global Logistics (AGL) kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili na kurudisha viwango vya gharama zilizokuwa zikilipwa hapo kabla ya tarehe 18 Septemba, 2023 pale mwekezaji alipokabidhiwa bandari.

Ikiwa hatua hizo zitashindikana, tunaitaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Dk Hussein Mwinyi kuvunja Mkataba na kampuni ya African Global Logistics (AGL) na kurudisha uendeshaji wa Bandari ya Malindi kwa Shirika la Bandari la Zanzibar.

Hitimisho:

Chama Cha ACT Wazalendo tunaamini kwamba Bandari ni Uchumi na kwa kiasi kikubwa Wazanzibari hususan wafanyabiashara wanategemea Bandari ya Malindi ya Zanzibar kwa kupakia na kupakua bidhaa zao; hivyo basi hatutakubali kuona Uchumi wa Zanzibar unauliwa kwa manufaa ya watu wachache.

Katibu wa Habari, Uenezi, Mawasiliano na Umma,

Chama cha ACT-Wazalendo

21/09/2023
 
Kumekucha Kigoma Ujiji 😂😂🐼🔥🔥

Unaikumbuka shuka kumeshakucha

Gavana Nassir: Hatutakubali Bandari ya Mombasa ibinafsishwe Kifala fala 😂😂😂🔥
 
Back
Top Bottom