Ndg habari za jioni!
Tangu Tanzania ilipoingia kwenye ubinafishaji mpaka sasa manufaa yamekuwa madogo sana. Si kweli kwamba hatukunufaika hata kidogo bali manufaa yetu yamekuwa madogo sana kiasi kwamba nchi imendelea kuwa masikini wakati rasilimali zetu zikiondoka.
Sababu hasa kubwa ya sisi kunyonywa kwa mtizamo wangu ni makosa yaliyofanywa na taasisi mbili kuu hapa nchini. Kwanza ni watumishi wa serikali waliaminiwa na umma kubariki unyonyaji huu kwa kujua au kwa kutokujua. Lakini pia chama cha mapinduzi (ccm) kushindwa kabisa kuona kwamba sisi tunanyonywa hivyo kushindwa kuisahihisha serikali zake kwa kipindi hicho. Kiasi kwamba kila kilichofanywa na serikali chama kiliona ni haki na sawa kabisa. Wako watu ndani ya chama huenda hawakuyapenda haya ila hawakuwa na uwezo wa kusema kwa kuogopa ama kuonekana wapinzani wa ndani ya chama au wapinzani wa serikali. Kwakweli hawa pamoja na yote tunapaswa kuwalaumu pia kwa kusaliti maslahi ya nchi kwa kulinda kuonekana wabaya ndani ya chama au kuonekana kuipinga serikali ya chama chao.
Heshima za dhati ziende kwa muona mbali mheshimiwa TL ambaye kaweka historia iliyotukuka kwa kupaza sauti kupinga sera na sheria zetu za uwekezaji ambazo ndizo zilikuwa mwanya wa sisi kunyonywa. Hapa kwakweli alistahili na nadhani bado anastahili pongezi kwa uzalendo wake wa muda wote, nadhani wale wanasiasa vijana waige mfano huu wa kuwa tayari kukosoa serikali au hata chama chako kwa mabaya yanayofanyika. Tatizo kubwa ni kwamba jumuia za vyama hapa nchini, kama uvccm, uwt, wazazi (ccm) ni vikundi ambavyo kazi yao kubwa ni kuikingia serikali kifua na hawana uthubutu wa kukemea mabaya ndani ya chama chao na serikali yao. Lakini hata BAVICHA, BAWACHA, AU NGOME YA VIJANA NA WAZEE WA ACT hawawezi kukosoa mambo yanayofanyika ndani ya vyama vyao hadharani bali wanaona tu makosa ya vyama vingine na makosa ya serikali. ( kama kuna kitu jumuia hizi zinatakiwa kukeamea ni makosa ndani ya vyama vyao kwanza kisha ndipo wavuke mipaka hasa kwa upinzani. Kwa vikundi vya ccm kazi kubwa iwe ni kukosoa chama na serikali kwanza kabla ya kuwashambulia cdm, act na cuf.
Heshima nyingi sana ziende kwa Mheshimiwa Rais wa awamu ya tano ndg JPM kwa kuwa na utashi wa kisiasa (political will) ya kushughulikia suala hili. Kwakweli pamoja na malalamiko mengi yaliyokuwepo viongozi waliotangulia walikosa utashi wa kisiasa kushughulikia suala hili, japo rundo la tume ziliundwa na matokeo yaliwekwa wazi. Kwangu binafsi na kama taifa tunapaswa kumpongeza Rais kwa nia yake kushughulikia suala hili ili walau tuanze kufaidi rasilimali zetu.
Baada ya utangulizi huo nimekuwa nikipata shida sana kutafakari juu ya meneno "TUKO KWENYE VITA VYA KIUCHUMI" ukweli ni kwamba tuko kwenye vita kubwa dhidi ya hawa wawekezaji wetu ila kidiplomasia neno vita vya kiuchumi nafikiri ni nzito sana. Hofu yangu ni kwamba pamoja na kwamba hawa watu wanatupunja pakubwa lakini ni wawekezaji , lakini pia wawekezaji wote duniani walio muhimu ni wa kutoka kwenye hizi nchi za ulaya, Marekani na kwasasa china. Sasa tunaposema tuko kwenye vita vya kiuchumi ambayo ni kweli, mtu anaweza kujiuliza je, tuko kwenye vita dhidi ya nani? jibu laweza kuwa wawekezaji wanyonyaji (mfano wa accacia and the like). Sasa hii haiwezi kuogopesha wawekezaji wengine kuja Tanzania kwa kuogopa neno hili "vita vya kiuchumi dhidi ya walengwa ambao kwakweli ni wawekezaji wanyonyaji"?.
NB: Kama kijana niliyepata elimu kidogo nilikuwa najaribu kuwaza impact ya neno hilo dhidi ya sera yetu ya kuvutia wawekezaji. Naomba michango yetu iegemee zaidi kujadili kama maneno hayo yana madhara au hayana. unaweza kutoa sababu kama yana madhara kwanini na kama hayana ni kwanini. Hakuna haja ya kumkebehi mtu, matusi au kutumia lugha ya kuudhi. Kumbuka ukomavu ni kuheshimu fikra za wengine hata kama hukubaliani nazo.
Kindikwili masasi Ntwara.