UPENDO UDUMISHWENI
Beti nimetunga, sikio ziwakune,
Kwa hiyari mmepanga, muoane muoane,
Kibwebwe mmejifunga, pamoja mshikamane,
Upendo udumishweni, i ngao ya familia.
2.
Ndoa ni uvumilivu, hili mwapaswa tambua,
Mjue mbichi na mbivu, vinaweza kutokea,
Mwenye wivu na anaiharibu ndoa,
Upendo udumishweni, i ngao ya familia.
3.
Mkawe mfano bora, kwenu hawo majirani,
Waige zenu ishara, zitumie maishani,
Kitabia mking'ara, wao kwenu taigeni,
Upendo udumishweni, i ngao ya familia.
4.
Watoto kibahatika, muwafunze yalo mema,
Waombeeni baraka, waje wawe na heshima,
Wote shuleni peleka, wakajifunze kusoma,
Upendo udumishweni, i ngao ya familia.
5.
Kauli nzuri tumia, mke kwa wako mmeo,
Sauti ya kupepea, iwe kwako mkazio,
Kiburi takuumbua, utaishia kilio,
Upendo udumishweni, i ngao ya familia.
6.
Mume nawe vile vile, mke ni faraja yako,
Uache mambo ya kale, kupiga kwa teke lako,
Mpe kanga na mchele, huko ndiko apendako,
Upendo udumishweni, i ngao ya familia.
7.
Msilete chokochoko, mawifi nawaambia,
Silete mvurugiko, ndoa kuitia doa,
Yamekushinda ya kwako, ya wifi unadandia,
Upendo udumishweni, i ngao ya familia.
8.
Mwovu atapata hamu, wanandoa kiachana,
Ndoa yenu itadumu, pamoja kishikamana,
Upendo udumishweni, i ngao ya familia.
9.
Mwenza wa ndani mepata, wa nje wa kazi gani,
Huko maradhi tapata, majuto hayo ya nini,
Ujumbe huu fuata, mshinde ya duniani,
Upendo udumishweni, i ngao ya familia.
10.
Shime metoa nasaha, mwapaswa kuzingatia,
Ombaneni msamaha, kati yenu kikosea,
Ndoa iwe ya furaha, mkono nawapungia,
Upendo udumishweni, i ngao ya familia.
Denny Jeremias kitumbika
Mtunzi wa mashairi na ngano za Kiafrika
Mufindi Tanzania 13.4.2016