Moyo wangu nilikupa, tena nikakuridhia
leo hii wanilipa , unyonge bila hatia
penzi umeshalitupa, kwengine waelekea
mimi waniacha kapa, bila kunihurumia
Ahsante nashukuru, nami nimeyakubali
madhali sikukudhuru, nenda potelea mbali
mola nitamdhukuru, anipe wangu asali
yaILAHI YA KAHARU, nipe moyo nihimili.
Nalia ninaumia, leo hii sina hali
wajua nateketea, penzi letu kulijali
mwenzangu wafurahia, umenitwisha jabali
nami nimelipokea, nifanye mie jahili.
Dunia yazunguka, waswahili wamesema
wewe utanikumbuka, si hiyari ni lazima
kwa wema nilikuweka, kwa maradhi na uzima
leo hii watoweka , kwa mabaya wanisema
Nenda "usotabirika", iko siku nitapona
kweli nimefadhaika, kwani nilipenda sana
leo umefarijika, mwenzio ninasonona
kuna siku nitacheka, tena sio mbali sana.