Magesa Inyasi, mwenye ulemavu wa macho na mkazi wa Musoma Mjini mkoani Mara amejipatia umaarufu mkoani hapo kutokana na kipaji chake cha kipekee cha kutunga nyimbo za papo kwa papo kulingana na matukio ya kijamii, kidini na kitaifa, huku akitumia mdomo na vidole vyake kuiga midundo ya vyombo vya muziki.
Mbali na kuimba nyimbo za dini, Inyasi pia huimba nyimbo za kupongeza maharusi, kuwatia moyo wafiwa na kuhamasisha jamii katika matukio mbalimbali.
Jana Mei Mosi, 2025, mwandishi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) amekutana naye mkoani humo na kumtaka aimbe kuhusu uchaguzi. Bila kusita, alitunga na kuimba wimbo unaowataka Watanzania kuchagua viongozi watakaolinda na kudumisha amani ya nchi.