Mgodi wa Resolute uliopo Wilayani Nzega Mkoani Tabora jana tarehe 12 Desemba, 2014, ulikabidhi eneo la Mgodi kwa Chuo cha Madini Dodoma katika hafla fupi iliyofanyika na kuhudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, anayeshughulikia madini Stephen Masele.
Wengine walioshuhudia ni, Mkuu wa Wilaya ya Nzega aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Bituni Msangi, Viongozi Waandamizi wa Wilaya ya Nzega, Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi Ally Samaje, Kamati ya Kitaifa ya uchimbaji, Uongozi wa Juu wa kampuni ya Resolute na wananchi. Naibu Waziri Masele alieleza kuwa, tukio la kukabidhiwa eneo hilo la Mgodi kwa Chuo ni tukio ambalo limefungua ukurasa mwingine kutokana na kwamba Chuo cha Madini Dodoma kitaiwezesha Tanzania kuzalisha wataalamu zaidi waliobobea katika tasnia hiyo ambao mchango wao kwa taifa unahitajika katika kuendeleza sekta ya madini.
Tunataka wanafunzi wasome kwa vitendo, hii itawezesha kupata wataalamu waliobobea. Ni nafasi kwa wanafunzi na Chuo cha Madini kuitumia fursa hii vizuri. Najua kuna mawazo mchanganyiko ya kupoteza mapato kwa Halmashauri na mengine ya kupata Chuo lakini, kufunga mgodi ni sehemu ya Sheria ya madini, aliongeza Masele.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nzega Bintuni Msangi, akizungumza katika halfa hiyo, alieleza kuwa, Mgodi wa Resolute una historia ya kuwa mgodi wa kwanza nchini kuzalisha madini ya dhahabu na kuogeza kuwa, ndani ya kipindi cha miaka 12 cha uhai wa mgodi huo umeweza kuchangia kiasi cha shilingi bilioni 290 za Kitanzania ikiwa ni kodi mbalimbali zilizotolewa na mgodi huo kama mrahaba.
Aliongeza kuwa, Halmashauri iliweza kupata kiasi cha shilingi bilioni 6 ikiwa ni kodi na kiasi cha Tsh bilioni 6 kilitumiwa na mgodi huo kuwezesha za kijamii ikiwemo ujenzi wa zahanati, shule, upatikanaji wa huduma safi ya maji katika eneo linalozunguka mgodi huo.