Nimekuwa nikiwasikiliza wadau wengi wakiwalaumu wachezaji wetu kwa kishindwa kucheza Ulaya. Wanaoongoza kwa lawama hizi ni waandishi wa habari. Lakini wachezaji ni kundi dogo sana (ingawa lililo muhimu sana) la wadau wote wa mpira duniani. Ili nchi ifanikiwe, ni lazima viungo vyote vya mnyororo huu viwe madhubuti na vilivyolainika: viongozi, waamuzi, waandishi, wapenzi, washabiki, madaktari, waalimu, wadhamini mawakala, n.k. Kabla hatujajiuliza ni wachezaji wangapi wameshaenda kucheza soka ya kulipwa kwenye Ligi zilizokomaa, tunapaswa kujiuliza ni wangapi kati ya wadau waliobakia nao wameshapata ajira kwenye mataifa hayo? Talib Hilal aliyeko Oman? Huko nako wachezaji kadhaa walikwishacheza. Jamhuri Kihwelu alipokwenda Yemen? Abdi Kassim yuko mbele zaidi ya hapo. Mawakala wanaosemekana wako ughaibuni? Kwa rekodi zao, ni madaraja ya akina Henry Joseph aliyeamua kurejea nyumbani baada ya kubangaoza hukohuko. Charles Hilary, Mwamoyo Hamza na wengineo? Wako huko wakiwa watangazaji wa jumla, mahsusi kwa idhaa za Kiswahili, sio wachambuzi wa kimataifa wa soka. TBL na udhamini aw Barcelona? Labda. Na ndio angalau wanaoisukuma hiyo Taifa Stars yetu. Sasa kama visima vyenyewe vimekauka, utategemeyaje maji mtungini?