Simu inayoua taratibu!

IAmShedeOne

JF-Expert Member
Joined
Jul 2, 2015
Posts
202
Reaction score
385
SUMU INAYOUA TARATIBU


Shumbana ni msichana mrembo aliyeolewa na kijana mtanashati mwenye kipato cha wastani. Walichukuana kimahaba tamthili ya njiwa manga. Licha ya umri wake kuwa mdogo, Shumbana alionekana kuyamudu vema majukumu yake ya nyumbani. Changamoto kubwa kwake iliyoanza kumsukasuka ni mama mkwe wake.

Tangu kuolewa kwake, Shumbana aliishi na mama mkwe wake katika nyumba moja. Na ikatokea mara kadhaa, Shumbana akikwaruzana na mkwewe kwa kupishana mitazamo juu ya namna mambo yalivyopaswa kufanyika ndani ya nyumba. Kila mmoja aliamini anayo mamlaka ya kuratibu shughuli za ndani. Mizozo ilichipua na kutengeneza uadui mkubwa baina yao - wakawa chui na paka.

Maisha ya ndoa yalimwia ugumu sana, Shumbana. Hakufurahia kabisa kuwa mke katika nyumba anayopangiwa namna ya kuishi na mama mkwe. Alipoona siku hadi siku hali inazidi kwenda arijojo, aliamua kumshitakia mumewe. lakini mume, alikuwa upande wa mama yake kwa kila jambo - hivyo Shumbana kukosa mhimili.

Uvumilivu ukamshinda Shumbana. Akaamua kuikacha nyumbani na kurudi kwao. Akiwa nyumbani kwao, alimshitakia baba yake kadhia nzima kuhusu mkwewe. Kwa kuwa bado alikuwa akimpenda sana mumewe, Shumbana alitoa rai akitaradhi msaada kwa baba yake: "Baba, njia pekee itakayonifanya nidumu kwenye ndoa yangu ni kumuondoa yule mama duniani. Naomba unipe sumu itakayomuua haraka ili mimi na mume wangu tuishi kwa amani."

Rai hiyo ilimshitua sana baba Shumbana, lakini hakuidhihirisha kwa bintiye. Ni kweli, baba Shumbana ni daktari bingwa wa masuala ya kutoa sumu mwilini, anazijua sumu za kila aina - na namna zinavyofanya kazi. Baada ya kutafakari, baba alimnasihi binti yake, "Haupaswi kufanya hivyo, Shumbana. Kwanza ni kinyume na maamrisho ya dini pamoja na utu; pili ujue tukifanya hivyo, lazima tutakamatwa."

Kwa ghadhabu na papara, Shumbana alijibu, "Kwahiyo baba unafurahia adha na manyanyaso ninavyopata kwa yule mama? Kama hutaki kunisaidia bora useme tu. Nani atakayejua kama tumempa sumu mpaka aje kutukamata?"

"Si hivyo binti yangu, siwezi asilani kufurahia taabu yoyote inayokuandama. Lakini kumbuka mumeo anajua wazi kwamba umeondoka kwa sababu ya matatizo na mama yake - naye ameshachagua upande wa mama yake. Ikitokea ukarudi, na mama yake akafariki, bila shaka atachunguza na kugundua ukweli. Na hapo ndipo tutakapotiwa nguvuni sote."

Pamoja na nasaha hizo, bado Shumbana alibaki na msimamo uleule. Basi, ili kumridhisha binti yake, baba aliafiki. Alimkabidhi pakiti ya sumu, kisha akamwambua, "Zingatia sana maelekezo yangu. Kwanza, usimwekee sumu yote kwa wakati mmoja - kila siku uwe unamwekea walau kijiko kimoja tu katika chakula chake, hii itamdhoofisha ndani kwa ndani kwa taratibu, na ndani ya miezi mitano mpaka sita atakufa. Hivyo basi, kwakuwa umeshajua kwamba atakufa, hautakiwi kuonekana una chuki naye; yakupasa ukaishi naye kwa amani na upendo, ukawe mkarimu kwake, umhudumie kwa nidhamu hata kama yeye ataendelea kukukwaza, ili atakapokufa usihisiwe kwa chochote!"

Shumbana alirejea nyumbani akiwa na furaha na matarajio mapya. Kama alivyoelekezwa, akaanza kumwekea sumu kwenye chakula kila siku, huku akizidisha ukarimu na upole. Kila alichokisema na kukitaka mama mkwe, Shumbana alitii kwa heshima na taadhima - lake moyoni.

Baada ya wiki chache tu, tabia ya mama mkwe ikaanza kubadilika. Hakua tena akimshurutisha Shumbana, badala yake alipenda kutumia muda mwingi kuketi naye na kupiga soga. Na kadiri siku zilivyozidi kusonga mbele, ndivyo mama mkwe alivyozidisha urafiki na Shumbana kiasi cha kumpa baraka zake zote kama mzazi.

Miezi ilianza kuyoyoma huku Shumbana akiendelea kumtilia sumu kidogo kidogo mkwewe kwenye chakula. Lakini hali ya masikizano ndani ya nyumba ilizidi kuimarika. Ikawa mama mkwe hawezi kula peke yake mpaka awe na Shumbana, hawezi kwenda kulala mpaka ameagana na Shumbana, na hata Shumbana anapogombana na mumewe basi mkwe humtetea yeye. Yale magomvi yao ya awali yakabaki kwenye 'jumba la makumbusho ya simulizi za kale'.

Upendo mpya uliochipua baina yao, ulianza kumtesa Shumbana kila alipofikiria sumu aliyokuwa akimlisha mkwewe kwa takribani miezi mitano sasa. Aliumia sana kila alipojua kwamba, siku za mwisho za uhai wa mkwewe zilikuwa zimekaribia. Hakukubali tena kumpoteza mkwewe lakini angefanyaje ilhali amekwisha kumlisha sumu!


Katika hali ya kutapatapa, Shumbana alirejea nyumbani kwa baba yake kumwomba ampe dawa ya kuondosha ile sumu mwilni mwa mkwe wake. Alimwambia baba yake, "Mkwe wangu amekuwa mtu muhimu sana, ananijali na kunipigania, sihitaji tena kumpoteza. Tafadhali baba, naomba unipe dawa ya kumtolea ile sumu mwilini."

Baba alitabasamu huku akisema, "Sumu?! Sumu gani tena? Mimi sikukupa sumu binti yangu, nilikupa dawa ya kumeng'enya chakula ili mlaji aweze kuwa na afya madhubuti. Nilijua kwamba endapo utamsikiliza mkweo na kumtii kwa kila atakalokuagiza, machukizo yatatoweka baina yenu na upendo utaanza kuchipua kama uyoga. Niliamini kwamba, mabadiliko ya tabia ya mkweo yasingaliweza kutokea endapo usingelianza wewe kubadilika - na huo ndo msingi wa mabadiliko katika kila nyanja duniani. Kabla ya kuibadili jamii au mtu, kwanza ubadilike wewe. Pia giza (chuki) haliondoshwi kwa giza, bali kwa mwanga (upendo)"

***

Maundu Mwingizi (Mwanabalagha)
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…