NI YUPI MKE BORA-By Ally Bakari Almasoud-(Mchanyato);mwalimumchanyato@gmail.com
Kwa utunzi wangu huno,Mchanyato natorora
Nia mnipe maono,ni yupi ni mke bora?
Alowahi fanya ngono,au aliye bikira?
Kati ya hawa wawili,ni yupi ni mke bora?.
Siyataki mabishano,nijibuni yenye sura
Niambieni maneno,kwa hoja zenye stara
mwenzenu nina agano,natafuta mke bora
Kati ya hawa wawili,ni yupi ni mke bora?.
Nipeni yunu maono,nisije pata hasara
Kwa umbo wote wanono,wazuri pia kwa sura
Kama wana mapatano,wafananavyo ishara
Kati ya hawa wawili,ni yupi ni mke bora?.
Huyu alofanya ngono,ni kwa njia ya stara
Ndoa ikawa ndoano,karibu kumpa dhara
Akaitupa mkono,mumewe hakuwa bora
Kati ya hawa wawili,ni yupi ni mke bora?.
Usijeleta miguno,mmoja kweli bikira
Huyu binti ni mfano,kwa kuwa yupo imara
Hakuwahi fanya ngono,wala kupata stara
Kati ya hawa wawili,ni yupi ni mke bora?.
Chonde sikiza vinono,mwenzako nacha hasara
Ninenayo si kigano,bali ninayo dhamira
Sitaki mke viuno,natafuta mke bora
Kati ya hawa wawili,ni yupi ni mke bora?.
Ikiwa uwezekano,nazisubiori bishara
Niyafanye mapatano,nipate mke kisura
Mak'e aliye mnono,tena aliye m'bora
kati ya hawa wawili,ni yupi ni mke bora
-Mchanyato-