Mzee nasalimia, wa Kijijini hujambo?
La mgambo likilia, ninajua lina jambo!
Mbiu nimeisikia, sio leo ni kitambo
Unataka kumjua, huyu ndege mwenye mambo
Ndege huyu ni KASUKU!
Ndege huyu ni Kasuku, jina nimelibaini
Si Bata wala si Kuku, hawa ndege wa shambani
Wala si yule Chiriku, wa sauti ya kughani
Itafika ile siku, atanaswa mtegoni
Ndege huyu ni KASUKU!
Nashangaa wa Kijiji, humjui ndege huyu!
Kama unamhitaji, 'usizunguke mbuyu'
Kwenye mti huo haji, amedandia mkuyu
Nawe sipande Bajaji, panda mti wa mkuyu
Ndege huyu ni KASUKU!
Wa Kijiji msifika, sasa unayo safari
Nenda msitu na nyika, jina ukilikariri
Wewe unajua fika, Msafiri ni kafiri!
Ndege huyu ni KASUKU!
Nenda siku na mapema, Kasuku 'kiita jina
Atakuja akihema, unataka nini Bwana
Huyu ni ndege wa zama, alifugwa kiungwana
Pema usijapo pema, kipema si pema tena!
Ndege huyu ni KASUKU!
Katu sibebe manati, ndege atakupuuza
Mithili ya Goliati, Daudi alimbeza
Wala sipige magoti, ndege kumbembeleza
Taja jina kwa sauti, KASUKU twende kucheza
Ndege huyu ni KASUKU!
Beba la mchuma Tenga, ndege kumhifadhia
Asije akakuchenga, msituni kurejea
Tembea 'kiringaringa, nyumbani 'naporejea
Ukishukuru wahenga, kwa dua kukuombea
Ndege huyu ni KASUKU!
Nyumbani ukiwasili, Tenga ulitue pindi
Katengeneze kufuli, kwa wale stadi mafundi
Tenga ulifunge kweli, na ndege mpe mahindi
Funguo katupe mbali, mle bahari ya Hindi
Ndege huyu ni KASUKU!
Acha na kucheka cheka, na huyu ndege Kasuku
Kuiga yake silika, atacheka kila siku
Ndege anahangaika, huenda huko na huku
Umesha 'piga mweleka, Karata umempiku
Ndege huyu ni KASUKU!
Fumbo fumbia mjinga, mwerevu huling'amua
Waliyasema wahenga, wa zama za Mwinyimvua
Ndiyo mana najiunga, la mgambo kupigia
Mwakaribishwa malenga, ulingoni kuingia
Ndege huyu ni KASUKU!
Namuita Andanenga, 'Sauti ya Kiza' Rufiji
Tumepuliza kipenga, mimi na Mwanakijiji
Mpira kupiga chenga, baadaye tunywe uji
Katu hatutawatenga, wa vijiji na wa miji
Ndege huyu ni KASUKU!
Na malenga wa Mvita, Juma Bhalo wa zamani
Nakuita kwenye vita, uje hapa Barazani
Najua utajikita, mashairi kuyaghani
Kati ya Popo na Bata, utambue ndege nani
Ndege huyu ni KASUKU!
Beti nazikamilisha, beti hizi za kudumu
Jibu nimewasilisha, Mmeipata elimu
Anayetaka kubisha, anitumie salamu
Hakuna kisichoisha, iliyobaki karamu
Ndege huyu ni KASUKU!
Hapa sasa ninakoma, sitaki kuitwa Kenge!
Nataka kwenda kusoma, mimi si Kalumekenge
Salamu zao Musoma, na wenyeji wa Rulenge
Wa Dar na wa Kigoma, na wa Kusini Mahenge
Ndege huyu ni KASUKU!
Na: Mrimu wa Herakuli (Jitu la miraba minne)