Ngozi ya mapenzi

Nicodemas Tambo Mwikozi

JF-Expert Member
Joined
Aug 13, 2016
Posts
663
Reaction score
1,047
Husika na kichwa cha habari hapo juu.

Baada ya kusikia mwingine tena kapigwa na kitu kingine chenye ncha kali na kupoteza maisha, nilijikuta nikirudisha kumbukumbu zangu juu ya ngozi; ngozi za ng'ombe, ngozi za binadamu, ngozi za mimea nk.

Kila chenye uhai Mwenyezi Mungu alikipatia ngozi. Ngozi ni ulinzi lakini pia ndiyo inayotoa muonekano wa nje wenye kuvutia.

Kila binadamu ana ngozi. Kwenye ngozi ndiko tunakopata rangi. Bila ngozi tungekimbiana, isitoshe tusingejitofautisha kati ya mweusi na mweupe. Ngozi ndiyo imebeba uzuri wa nje wa mwanadamu. Na zaidi sana ngozi inafanya vilivyo ndani ya mwili viwe na viendelee kuwa salama.

Ukichunwa ngozi hata kwa kutumia ganzi, kisha wakakuruhusu utembee barabarani, kuna mambo mawili yatatokea. Kwanza watu wote watakukimbia. Pili bacteria na virusi watakukimbilia na kukushambulia, baada ya muda mfupi utakufa.

Hata mnyama pia, anavutia kwa ngozi yake, lakini pia hawezi kuishi endapo utamchuna ngozi na kumuacha aendelee kula majani. Ngozi ni ngome ya ulinzi wa kila kiumbe hai.

Hata mti una ngozi yake. Tunayaita magome. Ukibandua magome, mti utakuwa na muonekano wa kushangaza, na siku chache baadae utakufa.

Hata matunda yanakuwa salama ndani ya ngozi zake. Tunaita maganda. Kuna maganda ya machungwa, ndizi, miwa nk. Hebu lifikirie parachichi bila ganda, lingekuwa na taswira gani? Matunda hayawezi kuwa salama kwa matumizi ya binadamu wala kwa uhai wake yenyewe kama utayaondoa maganda. Hakika yatapoteza thamani yake na kufa.

Mapenzi pia ni kiumbe hai. Mapenzi huzaliwa, hukomaa na hufa. Ili yaendelee kuwa salama yanahitaji ngozi. Ili yaendelee kuvutia na kupendeza yanahitaji ngozi pia. Ngozi ya mapenzi ni UPENDO.

Kuna tofauti kati ya MAPENZI na UPENDO. Tafsiri ya mapenzi ntamuachia dada yangu Neema Paulo anisaide. Lakini upendo ni kitu kingine kabisa.

Tofauti nyepesi kati ya mapenzi na upendo, ni kuwa mapenzi ni hisia kali kwa mtu mwingine kwaajili ya maslahi binafsi ya kuridhisha nafsi yako mwenyewe, wakati upendo ni hisia njema kwaajili ya maslahi mapana ya mtu mwingine.

Sifa kuu ya mapenzi ni ubinafsi na kutogawanyika kwa mbili. Mapenzi ni namba witiri.

Lakini sifa za upendo zimeenda mbali zaidi.

*Upendo hauhesabu mabaya
*Upendo hufadhili
*Upendo hautakabari (kujivuna)
*Upendo huvumilia yote
*Upendo hauna husuda (wivu)
*Upendo huamini yote (uaminifu)
*Upendo haulipi kisasi
*Upendo husamehe bila masharti

Kwa tafsiri hiyo utagundua kuwa upendo ni ile hali ya kujitoa kwako kwaajili ya furaha, mafanikio na uzima wa mtu mwingine.

Malipo ya upendo ni furaha na amani ya kweli katika moyo wako mwenyewe.

Malipo ya mapenzi kwa upande mwingine yanaweza kuwa pesa, ngono, au bakshishi.

Mwanamke au mwanaume anaweza kukupeda kimapenzi kwasababu tu ya pesa zako kwake, au kwa sababu ya utamu na utundu wa sanaa yako katika ngono tu; na wala asiwe na upendo juu yako. Upendo wake wa dhati unaweza kuwa kwa mtu mwingine tofauti, ambaye hayuko tayari kumpoteza kwa gharama yoyote. Mtu aliyeyagusa maisha yake kwa namna ya tofauti.

Mapenzi yanaweza yakanoga kwasababu za utamu wa pesa na ngono pekee lakini upendo usiwepo.

Upendo ni zaidi ya ngono na pesa. Ni zaidi ya zawadi na takrima. Upendo ni hisia inayogusa sehemu ya ndani kabisa ya moyo na nafsi ya binadamu.

Kwa karibu wiki mbili hizi yamefuatana matukio ya watu kuuana kikatili kwasababu za mapenzi. Tena wengi wao ni wanandoa. Na hayo ni baadhi tu ya matukio yaliyotangazwa, kuna mengi zaidi yasiyotangazwa. Tatizo liko wapi? Kwanini mapenzi yaliyokuwa matamu ghafla tu yanageuka shubiri?

Nimerudi na huu ufunuo wa NGOZI.

Mapenzi(ndoa) yanapaswa kufunikwa kwa ngozi imara ya Upendo, ili yaweze kuwa salama na yenye kuvutia.

Mapenzi bila upendo ni sawa na kumchuna ng'ombe ngozi na kumuacha aendelee kula majani safi ya kijani kibichi. Hawezi kufika popote....

MUNGU ATUFANYIE WEPESI
 
Mkuu ulipotelea wapi?
Sijakuona humu jukwaani mda mrefu
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…