MAUAJI WANAWAKE 7 GESTI, DAR YATIKISIKA
- Posted by GLOBAL on May 3, 2011 at 8:00am
Na Makongoro Oging'
Jiji la Dar es Salaam lipo katika mtikisiko mkubwa kufuatia kuibuka kwa wimbi kubwa la mauaji ya wanawake katika nyumba za kulala wageni (gesti), Uwazi halijaacha kitu.
Hali hiyo imejitokeza siku chache baada ya kuongezeka kwa vitendo hivyo ambapo mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la Rafaela Joseph (28), mkazi wa Kurasini jijini Dar kukutwa ameuawa chumba namba nane, kwenye gesti moja iliyopo Keko Machungwa.
Habari za kipolisi zinasema kuwa, mwanaume mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Ayubu anashikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Kilwa Road jijini Dar kwa mahojiano zaidi kufuatia vifo hivyo.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa, huku jeshi hilo likiwa limejipanga kukabiliana na wimbi hilo la mauaji, pia limefanikiwa kumtia mbaroni mtuhumiwa mwingine aliyetajwa kwa jina la Paskal Nesto akiwa na maiti chumbani.
Nesto alitiwa mbaroni wilayani Kinondoni baada ya kuhisiwa kuhusika na tukio hilo.
Katika hali ya kushangaza, ndani ya kipindi cha miezi mitatu jijini Dar, tayari wanawake saba wameuawa, mmoja wao akikutwa amenyofolewa sehemu zake za siri, hali inayoashiria kuwa mtandao huo ni mkubwa na kuna ushirikina ndani yake.
Mauaji ya mwisho ni ya Rafaela ambaye anatajwa kuwa ni mwanafunzi wa Chuo cha Uuguzi cha Princess cha jijini Dar es Salaam. Yeye baada ya kuuawa, muuaji alimkunja na kumficha chini ya uvungu wa kitanda katika chumba walichopanga.
Maiti ya msichana huyo ilikutwa ikiwa na damu sehemu mbalimbali za mwili kama masikioni.
Gazeti hili lilizungumza na mmoja wa ndugu zake, Victor Uisso ambaye alikuwa na haya ya kusema: "Kifo cha mama mdogo Rafaela ni cha kusikitisha sana. Tulielezwa kuwa, saa 12:00 jioni, Jumatatu iliyopita alimtaarifu rafiki yake (hakutajwa jina) kuwa aliitwa na mwanaume aliyemtaja kwa jina la Ayub ili akachukue fedha.
"Alipokwenda hakurudi, ilipofika saa moja walimpigia simu lakini ikawa inaita tu bila kupokelewa, baadaye ikazima.
"Jumanne saa 3:00 asubuhi mpangaji mwenzangu akanieleza kwamba, kuna binti amekutwa amekufa gesti. Tulikwenda, tukakuta mwili umechukuliwa na polisi kwenda Hospitali ya Temeke. Tulipofika kule tukakuta ni yeye.
"Sisi hapa nyumbani huyo Ayubu tulikuwa hatumtambui kama alikuwa na uhusiano na Rafaela bali tulimjua rafiki yake mwingine wa kiume na ndiye alikuwa karibu naye kwani alishafika nyumbani mara kwa mara, " alisema Uisso.
Taarifa zilizopatikana kutoka kwa rafiki wa kike zinasema kuwa, Siku ya Pasaka akiwa na marehemu walikwenda kukutana na Ayubu ambapo walikaa naye kwa muda mrefu.
Akasema baadaye Ayubu alimpa marehemu shilingi 5,000 za sikukuu na kumwahidi kumuongezea nyingine kesho yake (Jumatatu).
Akasema, Jumatatu baada ya kuwasiliana kwa njia ya simu ya kiganjani, marehemu alikwenda tena kwa Ayubu lakini hakurudi wala kuonekana hadi ilipopatikana maiti yake.
Vyanzo vingine vya habari vinadai kuwa, kipindi cha nyuma Ayubu alikuwa akifika karibu na maeneo aliyokuwa akiishi Rafaela. Alikuwa akiwaambia watu kwamba marehemu alichukua shilingi 200,000 zake na simu ya mkononi. Alikuwa akitishia kumsomea Albadiri au kumfanyia jambo baya.
Mjumbe wa Nyumba Kumi wa eneo la tukio, Christian Michael aliliambia gazeti hili kuwa, alishuhudia mwili wa binti huyo ukiwa katika hali mbaya na baada ya muda ulichukuliwa na polisi.
Baadhi ya wananchi ambao wanaishi jirani na gesti yalikotokea mauaji hayo waliiomba serikali kutoruhusu nyumba za kulala wageni kuwa karibu na makazi ya watu kwa kuwa walevi wanapoingia humo na wapenzi wao, hupiga kelele na kubughudhi majirani hasa wenye watoto wadogo.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, David Misime alipohojiwa kuhusiana na tukio hilo alikiri na akasema mtu mmoja ambaye hakupenda kumtaja jina ametiwa mbaroni kwa uchunguzi.
Matukio mbalimbali ya mauaji ya wanawake:
Februari 23 mwaka huu, Amina Ramadhan aliyekuwa mwanafunzi wa Ubungo Islamic High School aliuawa na mwanaume katika Gesti ya Mkombozi, iliyopo Mkwajuni, Kinondoni.
Machi 9 mwaka huu, Elizabeth Swai aliuawa Kawe, Gesti ya My Fair Club, chumba namba 310. Mwanaume aliyeingia naye hapo aliandika jina la Prosper Sichale katika kitabu cha wageni.
Machi 26 mwaka huu, Zubeda Rashid aliuawa katika Gesti ya Lil Wizo Rest, Mbezi ya Kimara, chumba namba mbili. Marehemu alisikika akipiga kelele kabla ya kukata roho.
Mlinzi alipokwenda alikuta ameshakufa huku akiwa na mwanaume aliyekuwa uchi aliyekwenda naye gesti hiyo ambaye alikamatwa na polisi walioongozwa na Mkuu wao, Mwita Mrefu. Mwanaume huyo alipohojiwa na polisi alisema anaitwa Prosper Simon lakini katika kitabu cha wageni aliandika Paschal Westo.
Aprili 23 mwaka huu, Asha Shamila, mkazi wa Vingunguti, Dar alikutwa amekufa katika Gesti ya Mkombozi, Buguruni kwa Mnyamani.
Machi, mwaka huu mwanamke mwingine ambaye jina lake halikutambulika, alikutwa ameuawa katika chumba namba 108, Gesti ya Four A iliyopo Tandika Transformer. Sehemu zake za siri zilikatwa.
Machi 2, mwaka huu, Hadija alikutwa amekufa katika Gesti ya Ngekewa, Tandika chumba namba sita.
Haijajulikana sababu za wanawake hao kuuawa na uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa, vifo vyao vinahusishwa na mapenzi au mambo ya kishirikina.
Wiki iliyopita Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova aliitisha mkutano wa makamanda wote katika ‘zoni' yake ili kujadili suala hilo la mauji na aliwatahadharisha kuwa makini na mtandao wa wanaume wanaowarubuni wanawake kisha kuwaua.
Kwa picha nenda
hapa
.........
....AND THE SERIAL KILLING CONTINUES!....