Mhegera anatuhumiwa kufanya tukio hilo Julai 23 kwa kumpiga risasi baba mkwe wake, Adrian Mpande kwa hisia kuwa ndiye chanzo cha kuvunjika kwa ndoa yake miaka 10 iliyopita.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa Mpande ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Bagamoyo (CCM) 1980-1985 alijeruhiwa bega la kushoto kwa kupigwa risasi mbili na mtuhumiwa huyo wakati akijiandaa kuingia kanisani katika ibada.
Pia ilielezwa kuwa wakati anakamatwa, Mhegera alisikika akimlaumu Mpande kuwa ndiye chanzo cha mgogoro kwenye ndoa yake. Kadhalika, imeelezwa kuwa Elias aliwahi kufungua mashauri kadhaa ya ndoa yanayohusiana na mgawanyo wa mali, lakini alishindwa yote.
Akizungumza na Nipashe, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Muriro Jumanne alisema mtuhumiwa huyo bado anashikiliwa na polisi tangu alipokamatwa.
“Bado tunamshikilia mtuhumiwa na hatuwezi kumuachia kwa sababu majeruhi bado yuko Muhimbili, kwa sasa bado upelelezi unaendelea hadi pale tutakapokamilisha,” alisema Kamanda Murilo.
Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Neema Mwangomo, alisema majeruhi kwa sasa anaendelea vizuri na ametoka katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).
Alisema kwa sasa Mpande yuko wodi ya wagonjwa wa kawaida na hali yake inaendelea vizuri.
Chanzo: Nipashe