Dr. Wansegamila
JF-Expert Member
- Feb 3, 2012
- 2,954
- 8,093
Mlipuko wa virusi vya zika unaosababisha ulemavu kwa watoto wanaozaliwa kuwa na vichwa vidogo isivyo kawaida (microcephaly), umeripotiwa kuzuka katika nchi za Brazil na Bolivia. kesi za virusi vya zika zimeripotiwa tangu mwezi oktoba na kufikia hadi 3, 500 wiki iliyopita. maofisa wamesema, virusi vya zika vinaambukizwa na mbu aina ya Aedes egyptiae. Mbu ambae ndie anaebeba virusi vinavyosababisha ugonjwa wa dengue, ugonjwa uliolipuka nchini mwaka 2014. Kutokana na ukweli kwamba mbu aina hiyo wapo nchini kwa wingi, kuna uwezekano wa ugonjwa huo kuingia nchini. Uwezekano huo unazidi kuwa mkubwa kutokana na ukweli kwamba, kipindi hiki cha mvua, mazalia ya mbu huongezeka zaidi. Hadi sasa, ugonjwa huo umeripotiwa kudambaa katika nchi 23 za bara la America.
Kirusi hiki cha Zika, sio kipya, lakini madhara yake ni mapya kwa kuwa sasa yanawaathiri watoto waliozaliwa na wajawazito wenye maambukizi ya virusi hivyo. Dalili za ugonjwa huu zinafanana kwa kiasi kikubwa na dalili za ugonjwa wa dengue, na ni pamoja na homa, uchovu wa jumla wa mwili, maumivu ya kichwa na misuli, na dalili hizi huanza kuonekana siku kadhaa hadi wiki baada ya kuata maambukizi, na mara nyingi dalili hizi hupotea zenyewe ndani ya siku au wiki kadhaa. Ni mara chache sana mtu huumwa mpaka kuhitaji kulazwa au kupoteza maisha.
Kitu ambacho kimefanya mlipuko wa safari hii wa ugonjwa huu uwe wa tofauti na kuamsha hisia za wasiwasi, ni madhara mapya ya ugonjwa huu ya kusababisha wajawazito wenye maambukizi ya ugonjwa huu kujifungua watoto wenye vichwa vidogo kuliko kawaida (microcephaly). Madhara haya yaligunduliwa na wanasayansi wa Brazili mnamo mwezi Mei 2015, baada ya utafiti kufanyika kwa kuwafanyia vipimo wamama ambao walijifungua watoto wenye tatizo hilo(Kuna visa 270 vya watoto kuzaliwa na vichwa vidogo ambavyo vimethibitishwa, kwa mujibu wa wizara ya afya nchini humo.Kuna visa vingine 3,448 vya microcephaly ambavyo bado vinachunguzwa).
Kitu cha kutia wasiwasi zaidi ni kwamba, watu wengi hawaonyeshi dalili zozote za ugonjwa huo, lakini wana maambukizi ya virusi hivyo, na wanaweza kusambaza virusi hivyo kwa watoto wao kabla ya kuzaliwa; Pia bado hakuna tiba wala kinga ya ugonjwa huo, na madhara ya ugonjwa huo kwa mtoto ya kuwa na kichwa kidogo na ubongo uliodumaa (microcephaly) ni ya kudumu!
Kuenea kwa kasi kwa virusi vya Zika ndiko kwa karibuni zaidi kati ya magonjwa manne ya virusi yanayoenezwa na mbu mataifa ya Magharibi katika kipindi cha miaka 20, anaandika Dkt Fauci kwenye makala katika jarida la kimatibabu la the New England Journal of Medicine.Mlipuko huu unafuata mlipuko wa maradhi ya kidingapopo (homa ya dengue), virusi vya Nile Magharibi, na majuzi zaidi, chikungunya. Sawa na maradhi haya, virusi vya Zika pia huenezwa na mbu.Lakini kinyume na virusi hivyo vingine, hakuna chanjo dhidi ya Zika. Je, ni njia gani iliyopo ya kukabiliana na virusi hivi?
1. Kutumia dawa au mafuta ya kufukuza mbu
Ushauri wa kwanza kabisa ni kuepukana na mbu. Kituo cha Kudhubiti na Kuzuia Maradhi (CDC) nchini Marekani kinapendekeza watu wajipake mafuta yenye kemikali za kufukuza mbu kama vile N, N-diethyl-meta-toluamide (DEET) au picaridin.Mafuta haya yanafaa kujipakwa mara kwa mara, kwa kufuata maagizo kwenye mikebe, au mtu anapoanza kuumwa na mbu. Mtu anafaa kujipaka baada ya kujipaka mafuta ya kukinga ngozi dhidi ya miali ya jua.Mafuta mengi ya kufukuza mbu ni salama hata kwa kina mama waja wazito, lakini ni vyema kutafuta ushauri wa daktari kabla ya kuanza kuyatumia.
2. Kuvalia mavazi ya kufunika mwili
Wataalamu pia wanakubaliana kwamba inafaa kuvalia mavazi yanayofunika mwili vyema. Mfano shati au nguo zenye kufunika mikono na pia suruali au long’i ndefu. Mavazi yanafaa kuwa mazito kuzuia mbu kufikia ngozi.Katika baadhi ya mataifa, mavazi huwekwa dawa maalum aina ya permethrin, ambao hufukuza mbu.Iwapo utajipaka mafuta ya kufukuza mbu, usijipake na kisha kufunika maeneo uliyojipaka kwa nguo unazovalia.
3. Kuzuia mbu kuingia nyumbani
Ikiwezekana, wataalamu wanawashauri watu walale ndani ya nyumba zilizojengwa vyema na kuwekwa kinga ya kuzuia mbu kuingia.Usiku, lala chini ya neti zilizotibiwa.Lakini usitahadhari usiku pekee kwani mbu aina ya Aedes aegypti, wanaoeneza virusi vya Zika, hupenda sana kuuma watu mchana.
4. Chunga mimea inayokua ndani ya nyumba
Ingawa ni muhimu kuzuia mbu kuingia, ni muhimu hata haidi kuzuia mbu kuzaana. Na mbu huhitaji maji.Watu wanashauriwa kuchunga sana maeneo yenye maji yaliyosimama kwani huko ndiko viluwiluwi wa mbu huwa. Maeneo haya ni pamoja na mikebe, maeneo ya kuwapa mifugo na wanyama wengine lishe, jagi za kuweka maua, vibanda vya kufugia ndege na mimea ya kupandwa ndani ya nyumba.Ni vyema pia kusafisha mifereji ya maji mara kadha kila wiki, mufunika matangi ya mali na vidimbwi la sivyo kuweka dawa ya krolini (krolini huwafukuza mbu).Maji ambayo yametulia kwa zaidi ya siku tano yanafaa kutupwa kwa kumwagwa ardhi kavu, kwani viluwiluwi wa mbu watafariki baada ya maji kukauka. Kiasi kidogo tu cha maji kinatosha kwa viluwiluwi hao kukua kwa hivyo, ni vyema kuosha na kukausha vyema maeneo hatari.
5. Kufunika taka
Maeneo ya kutupwa taka mara nyingi huwa na maji na hutumiwa sana na mbu kuzaana.Ili kuzuia hili, ni vyema kufunika taka, hasa katika mifuko ya plastiki.Tairi kuukuu na vitu vingine vya ujenzi pia vinafaa kuwekwa vyema, kwani sana huhifadhi maji ambayo yanaweza kutumiwa na viluwiluwi wa mbu.
6. “Kunyunyizia dawa”
Maafisa nchini Brazil, ambako virusi vya Zika vimeenea sana, wanatafakari wazo la kunyunyizia maeneo yaliyoathiriwa na virusi hivyo dawa ya kuua mbu.Hata hivyo, kuna utata kwani njia hii inaweza kuwa na madhara mengine kwenye mazingira na pia kuathiri afya ya wakazi.
7. Kudhibiti mbu
Serikali katika nchi kadha za Amerika Kusini tayari wameanza kampeni ya kuangamiza mbu wanaobeba virusi vya Zika kwa kutumia teknolojia.Moja ya njia tata zinazopendekezwa ni kueneza mbu waliofanyiwa mabadiliko ya kijeneti ambao hawana uwezo wa kuzaana. Hili litapunguza idadi ya mbu na kuzuia ugonjwa huo kuenea.Wengine wamejaribu mbinu nyingine, mfano jiji la Itapetim nchini Brazil. Maafisa mjini humo wanatumia samaki kuangamiza mbu huo.Samaki hao hula mayai ya mbu na hivyo kuzuia kuongezeka kwa idadi ya mbu hao.
8. Vifaa ya kukabili mbu nyumbani
Maafisa wa serikali wanapojaribu kukabiliana na mbu kwa kiwango kikubwa, watu binafsi manyumbani pia wanatumia njia mbalimbali kukabili mbu.Wanatumia vifaa mbalimbali vya kuwawinga na kuwaua mbu. Mfano ni kutumia kifaa kinachoiga mwili na kutoa hewani ya kaboni dayoksaidi pamoja na joto, ili mbu waingie ndani wakidhani ni binadamu.Mitambo mingine ya kunyunyiza dawa ya kuua mbu pia inatumiwa, lakini inapingwa na baadhi ya watu kwani inaathiri pia nyuki, vipepeo na wadudu wengine.
9. Kukwepa kusafiri
Wale wanaoishi maeneo ambayo hayajaathirika na virusi hivyo, wanajizuia kusafiri.CDC(Center for Diseases Control-Marekani)imewashauri wanawake waja wazito nchini Marekani kuahirisha ziara zao Amerika Kusini na visiwa vya Caribbean kadiri wawezavyo.Kituo hicho kimewashauri wanawake wanaopanga kusafiri maeneo hayo kutafuta ushauri wa madaktari kwanza.Shirika la Afya Duniani (WHO), hata hivyo, halijaunga mkono ushauri huo wa CDC.“Kwa kutumia ushahidi uliopo, WHO haipendekezi vikwazo vya usafiri au biashara kuhusiana na virusi vya Zika. Lakini kama tahadhari, mataifa mbalimbali yanaweza kutoa mapendekezo mbalimbali ya kiafya na kuhusu usafiri kwa raia wake, kwa kuzingatia utathmini,” WHO imesema.
10. Kuzuia kuenea
Mtu anapoambukizwa, hatua zaidi zinafaa kuchukuliwa kuzuia kuumwa tena na mbu wiki ya kwanza baada ya kuugua, CDC inasema.Hii ni kwa sababu virusi vya Zika vinaweza kusambazwa kutoka kwa mtu mmoja hadi kwa mtu mwingine kupitia damu baada ya kuumwa na mbu.Ingawa hatari ya kuenezwa kwa virusi hivi kupitia kujamiiana haijathibitishwa kisayansi, baadhi wanapendekeza watu watumie mipira ya kondomu hadi wiki mbili baada ya kupona.Aidha, watu wachukue tahadhari kuepusha kuambukizwa virusi hivyo kupitia mate na majimaji ya mwili.