Mlenda wa bamia na nyanya chungu
Kuandaa: dakika 10 Mapishi: dakika 20
Walaji: 2
Ujuzi: Rahisi
Gharama: Nafuu
Mlenda ni mboga yetu cha asili. Kuna mlenda wa aina nyingi sana. Haya mapishi yanaonyesha mojawapo kati ya mlenda unayoweza kuandaa kutumia vitu rahisi – bamia na nyanya chungu, lakini ladha yake si ya kawaida. Inafaa zaidi kuliwa na ugali ukiwa wa moto na pilipili.
Mahitaji
Nyanya chungu
Bamia
Nyanya maji
Kitunguu
Karoti
Pilipili hoho
Mafuta ya kupikia
Maelekezo
Menya nyanya, kitunguu, karoti na pilipili hoho. Kata kwenye vipande vidogo.
Andaa bamia kwa kutoa ncha na mkia kisha kata mara mbili au jinsi utakavyopendezwa
Menya nyanya chungu na kuikata katikati.
Bandika sufuria kisha weka mafuta kiasi. Yakichemka weka nyanya chungu. Kaanga kama dakika kumi ili zibadilike rangi na kuwa za rangi ya udongo (angalia zisiungue). Kisha zitoe kwenye mafuta.
Punguza mafuta ya kula kiasi, bakiza yanayotosha kupikia mboga.
Weka kitunguu. Koroga na subiria kiive.
Weka pilipili hoho na carrot. Koroga kwa muda wa takribani dakika 3
Weka nyanya. Koroga na kisha funika ili ziive.
Weka bamia. Ongeza maji kiasi. Bamia huchukua muda kuiva, hivyo ni vizuri kuongeza maji.
Funika mboga yako na acha ichemke kwa muda wa dakika kama 10 – 15. Bamia zitakua zimeiva. Kuwa makini bamia zisilainike sana.
Weka nyanya chungu kwenye mchuzi. Acha zichemke kama dakika 5 kisha ipua mboga yako inakua tayari kuliwa.
Jirambe na ladha ya maisha, maisha ya kuteleza kama ulivyo mlenda