Mkeo Kafariki

Ambiele Kiviele

JF-Expert Member
Joined
Dec 29, 2014
Posts
15,270
Reaction score
29,939
MKEO AMEFARIKI.

“Mkeo amefariki Msiba uko hapa nyumbani?”
Denis alipokea ujumbe mfupi kwenye simu
yake, kuangalia ulitoka kwa Mama yake
mzazi.

Nguvu zilimuishia, alikuwa akiongea
na mteja ofisini kwake lakini sauti ilikauka.
Bila kujijua alijikuta ananyanyuka na kuanza
kutembea. tembea ofisini kwake akiwa
hajitambui.

Wafanyakazi wake walimuuliza
bosi vipi lakini hakuwa na jibu la maana la
kuwapa.

Akili yake ilikumbuka maneno ambayo
alimwambia mkewe asubuhi wakati
anaondoka, mkewe alimwambia sukari
imeisha na kwa dharau alimjibu, “Sasa
unaniambia mimi ili nini? Kwani ni lazima
unywe chai, huko kwenu mlikua mnakunywa
chai kila siku?”

Alikumbuka namna usiku wake alivyompiga
makofi baada tu ya mboga kuungua
alipochelewa kuepua kwani alikua
ananyonyesha mtoto wao wa mwisho ambaye
yeye mwenyewe ndiyo alimuita amnyonyeshe
kwani alikuwa analia sana.

Alikumbuka namna siku mbili kabla mkewe
alisema amechoka kupigwa na kunyanyaswa,
anakumbuka namna alivyomjibu kwa dharau
kuwa kama amechoka aondoke amuachie
watoto wake.

“Ameniachia wanangu!” Alijikuta anaropoka
na machozi yalianza kumtoka. Alishindwa
hata kutembea hivyo alikaa chini kabisa
sakafuni. Wafanyakazi wake walikuja na
kumnyanyua na baada ya kumuuliza ndipo
alipowaambia mkewe amefariki.

Walimchukua mpaka kwenye gari na safari ya
kurejea nyumbani ilianza, walifika nyumbani,
kila kitu kilikuwa kimya, nyumba ilikua
imefungwa na hakukuwa na mtu.

Denis alizidi kuchanganyikiwa zaidi asijue nini
cha kufanya ndipo alipokumbuka kuwa Mama
yake alimwambia msiba uko nyumbani hivyo
alidhani kuwa ni nyumbani kwao.
********************

Safari nyingine ilianza, Dennis alikuwa na
mawazo, hayakuwa mawazo tu ya kufiwa bali
ya aibu.

Pamoja na kumiliki kampuni kubwa
akiajiri watu zaidi ya kumi lakini mkewe
alimnyanyasa na kumtesa kama kinyago,
mbali na kumpiga lakini alikua hamhudumii
vizuri.

“Atakuwa amefia kwa Mama wakati ameenda
kuomba hela ya matumizi…”

Aliwaza kwani
mara nyingi alipokuwa akimnyima pesa Mama
yake mzazi ndiyo alikuwa akimsaidia na ndiye
alizuia mara nyingi mkewe asiondoke.

Alifika mpaka nyumbani kwao, kweli kulikuwa
na msiba, maturubai yalishawekwa, watu
walishaanza kupika na watu walishaanza
kujaa taratibu.

Alijitahidi kushuka kwenye gari
na kuanza kutembea kuelekea nyumbani.
Watu walikua wakimsalimia na kumpa pole,
aliipokea kwa aibu huku akiwaza ni kitu gani
kiliwasukuma wazazi wake kufanyia msiba
pale na ni nini kilikuwa kimesababisha mauti
ya mkewe.

“Ameumwa sana muacheni apumzike..”
Ilikuwa ni sauti ya Baba yake mzazi
ikimwambia jirani yao mmoja.

Hapo ndipo
alichanganyikiwa zaidi akiwaza ni kwa namna
gani mkewe alikuwa anaumwa bila yeye kujali.

Lakini alikumbuka ni mara nyingi mkewe
alimwambia anaumwa lakini alidharau na ni
mara nyingi Mama yake alimsema kuhusu
kutokumsikiliza mkewe na mara nyingi tu
Mama yake aliongozana na mkewe
hospitalini.

Yeye kwake yote hayo hakujali, kila mke
alipomwambia anaumwa yeye alidai haki yake
ya ndoa, alizidi kumpiga na alianza
kukumbuka namna ambavyo alimpiga mpaka
kulazwa lakini bado hakujali.

Aliwaza, "Labda ndiyo ilikuwa sababu ya kifo
chake? Au alikuwa anaumwa kimya kimya
halafu hasemi akaja kusema nyumbani?”

Alitembea mpaka kufika ndani, alikaa na
kusalimiana na ndugu wengine ambao nao
walikuwa wanampa pole kwa msiba.

Alizipokea huku akijaribu kujizuia machozi
yasitoke. Mara mtoto wake wapili wa miaka
minne alikuja. Alikuwa akilia akimtaka Mama
yake watu wakimwambia asubiri Mama yake
anakuja.

Mtoto alimkimbilia Dennis na kuanza kulia
"Baba namtaka Mama, namtaka Mama." Denis
alichaganyikiwa kwani hakuwa na jibu la
kumpa, hakujua amwambie nini kuhusu Mama
yake.

Mara mtoto mwingine mkubwa kidogo wa
miaka saba alikuja, alikuwa amembeba mtoto
wao mdogo mchanga wa miezi sita. Alimfuata
Baba yake na kumuuliza, "Baba, Mama yuko
wapi Jack anataka kunyonya."

Hapo ndipo aliishiwa nguvu kabisa, maneno
yake ya “Ondoka niachie wanangu"
yalizunguka kichwani kwake. Aliwaangalia
wanawe na kusema, "Kweli nimeachiwa,
umeniweza Juddy mke wangu."

Alijikuta anaanza kulia kama mtoto kitu
ambacho kiliwafanya na wanawe wote kulia.

Dennis alichanganyikiwa, kila mtu aliyekuwa
anakuja nyumbani alienda kumpa pole, nguvu
zilimuishia alikata tamaa, na majuto ya hali
ya juu, kila tendo baya alilokuwa akimfanyia
mkewe lilimjia kichwani.

*********************
“Mama Jose njoo umnyonyeshe mtoto analia
toka muda mrefu.” Ilikua ni sauti ya Mama
yake. Dennis alishtuka na kunyanyuka
kuangalia, Mama Jose ni mkewe na hakujua
ni kwa nini Mama yake alikuwa anamwambia
aje kumnyonyesha mtoto wakati alishafariki
dunia.

Kabla hajasema chochote Mama yake aliingia
kisha, “Ohhh Dennis umekuja? Nikajua utakuja
baadaye kazi zimekubana, mkeo alisema
hupatikani kwenye simu.”

Dennis alizidi kuchanganyikiwa, alibaki na
mshangao. Mara mkewe aliingia, hapo ndipo
alichanganyikiwa zaidi, alishtuka kama vile
ameona mzimu, kidogo amdondoshe mtoto
aliyekuwa amempakata.

“Vipi Baba Jose…” Mkewe alimuuliza kwa
maana namna alivyokuwa akimuangalia
haikuwa kawaida yake.

“Uko hai mke wangu?”

Alijikuta anauliza. “Ndiyo kwani vipi ulitaka
nife?” Mkewe alijibu kwa kebehi kidogo kwani
alijua ni dharau ya mumewe.
“Lakini Mama......”

Dennis aliongea kwa
kushangaa huku akimuangalia Mama yake.
Mama yake alitabasamu na kumwambia,

"Aliyefariki ni Bibi yako si ndiyo alikuwa
anakuita mume wangu?

"Wewe mbona kila siku ukipiga simu unaulizia
mke wangu hajambo." Dennis alipumua kwa
nguvu huku akikaa chini, mkewe alimchukua
mtoto kwenda kumnyonyesha.

Denis alimfuata
huko huko chumbani, alipiga magoti mbele
yake na kusema, “Samahani mke wangu
nilikuwa sijajua thamani yako mpaka leo.

Yaani leo ndiyo nilichanganyikiwa, nilijua
umekufa na tayari nilishaona maisha
hayawezekani bila wewe.

Ninaahidi
nitabadilika nitakuwa mume mwema na
kamwe sikunyanyasi tena."

Mama yake ambaye alisimama mlangoni
alitingisha kichwa na kucheka huku akisema,
“Unavyoringa uachiwe watoto kila siku, unajua
uchungu wa kulea wewe au unataka uachiwe
ili uje kunitupia wanao hapa nianze kulea
wajukuu?!”

Hakusubiri hata jibu aliondoka akimuacha
mwanaye akiendelea kuomba msamaha akiwa
haamini kuwa mkewe yu hai.

Siku ile ndiyo
ilikuwa siku ya Mabadiliko kwa Dennis kwani
hakuwahi kumpiga wala kumnyanyasa tena
mkewe.

*****MWISHO******

Kama umejifunza chochote niachie Comments

Na iwe Fundisho kwa wengine pia
walio na tabia kama ya Dennis.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…