Mkeo amefariki

Abunwasi

JF-Expert Member
Joined
Jun 25, 2009
Posts
5,486
Reaction score
3,483
.“Mkeo amefariki Msiba uko hapa nyumbani?”
Denis alipokea ujumbe mfupi kwenye simu yake,
kuangalia ulitoka kwa Mama yake mzazi. Nguvu
zilimuishia, alikuwa akiongea na mteja ofisini
kwake lakini sauti ilikauka.
Bila kujijua alijikuta ananyanyuka na kuanza
kutembea. tembea ofisini kwake akiwa
hajitambui. Wafanyakazi wake walimuuliza bosi
vipi lakini hakuwa na jibu la maana la kuwapa.
Akili yake ilikumbuka maneno ambayo
alimwambia mkewe asubuhi wakati anaondoka,
mkewe alimwambia sukari imeisha na kwa
dharau alimjibu, “Sasa unaniambia mimi ili nini?
Kwani ni lazima unywe chai, huko kwenu mlikua
mnakunywa chai kila siku?”
Alikumbuka namna usiku wake alivyompiga
makofi baada tu ya mboga kuungua alipochelewa
kuepua kwani alikua ananyonyesha mtoto wao
wa mwisho ambaye yeye mwenyewe ndiyo
alimuita amnyonyeshe kwani alikuwa analia sana.
Alikumbuka namna siku mbili kabla mkewe
alisema amechoka kupigwa na kunyanyaswa,
anakumbuka namna alivyomjibu kwa dharau
kuwa kama amechoka aondoke amuachie watoto
wake.
“Ameniachia wanangu!” Alijikuta anaropoka na
machozi yalianza kumtoka. Alishindwa hata
kutembea hivyo alikaa chini kabisa sakafuni.
Wafanyakazi wake walikuja na kumnyanyua na
baada ya kumuuliza ndipo alipowaambia mkewe
amefariki.
Walimchukua mpaka kwenye gari na safari ya
kurejea nyumbani ilianza, walifika nyumbani, kila
kitu kilikuwa kimya, nyumba ilikua imefungwa na
hakukuwa na mtu.
Denis alizidi kuchanganyikiwa zaidi asijue nini
cha kufanya ndipo alipokumbuka kuwa Mama
yake alimwambia msiba uko nyumbani hivyo
alidhani kuwa ni nyumbani kwao.
********************
Safari nyingine ilianza, Dennis alikuwa na
mawazo, hayakuwa mawazo tu ya kufiwa bali ya
aibu. Pamoja na kumiliki kampuni kubwa akiajiri
watu zaidi ya kumi lakini mkewe alimnyanyasa na
kumtesa kama kinyago, mbali na kumpiga lakini
alikua hamhudumii vizuri.
“Atakuwa amefia kwa Mama wakati ameenda
kuomba hela ya matumizi…” Aliwaza kwani mara
nyingi alipokuwa akimnyima pesa Mama yake
mzazi ndiyo alikuwa akimsaidia na ndiye alizuia
mara nyingi mkewe asiondoke.
Alifika mpaka nyumbani kwao, kweli kulikuwa na
msiba, maturubai yalishawekwa, watu
walishaanza kupika na watu walishaanza kujaa
taratibu. Alijitahidi kushuka kwenye gari na
kuanza kutembea kuelekea nyumbani.
Watu walikua wakimsalimia na kumpa pole,
aliipokea kwa aibu huku akiwaza ni kitu gani
kiliwasukuma wazazi wake kufanyia msiba pale
na ni nini kilikuwa kimesababisha mauti ya
mkewe.
“Ameumwa sana muacheni apumzike..” Ilikuwa ni
sauti ya Baba yake mzazi ikimwambia jirani yao
mmoja. Hapo ndipo alichanganyikiwa zaidi
akiwaza ni kwa namna gani mkewe alikuwa
anaumwa bila yeye kujali.
Lakini alikumbuka ni mara nyingi mkewe
alimwambia anaumwa lakini alidharau na ni mara
nyingi Mama yake alimsema kuhusu
kutokumsikiliza mkewe na mara nyingi tu Mama
yake aliongozana na mkewe hospitalini.
Yeye kwake yote hayo hakujali, kila mke
alipomwambia anaumwa yeye alidai haki yake ya
ndoa, alizidi kumpiga na alianza kukumbuka
namna ambavyo alimpiga mpaka kulazwa lakini
bado hakujali.
Aliwaza, "Labda ndiyo ilikuwa sababu ya kifo
chake? Au alikuwa anaumwa kimya kimya halafu
hasemi akaja kusema nyumbani?” Alitembea
mpaka kufika ndani, alikaa na kusalimiana na
ndugu wengine ambao nao walikuwa wanampa
pole kwa msiba.
Alizipokea huku akijaribu kujizuia machozi
yasitoke. Mara mtoto wake wapili wa miaka
minne alikuja. Alikuwa akilia akimtaka Mama
yake watu wakimwambia asubiri Mama yake
anakuja.
Mtoto alimkimbilia Dennis na kuanza kulia "Baba
namtaka Mama, namtaka Mama." Denis
alichaganyikiwa kwani hakuwa na jibu la kumpa,
hakujua amwambie nini kuhusu Mama yake.
Mara mtoto mwingine mkubwa kidogo wa miaka
saba alikuja, alikuwa amembeba mtoto wao
mdogo mchanga wa miezi sita. Alimfuata Baba
yake na kumuuliza, "Baba, Mama yuko wapi Jack
anataka kunyonya."
Hapo ndipo aliishiwa nguvu kabisa, maneno yake
ya “Ondoka niachie wanangu" yalizunguka
kichwani kwake. Aliwaangalia wanawe na
kusema, "Kweli nimeachiwa, umeniweza Juddy
mke wangu."
Alijikuta anaanza kulia kama mtoto kitu ambacho
kiliwafanya na wanawe wote kulia. Dennis
alichanganyikiwa, kila mtu aliyekuwa anakuja
nyumbani alienda kumpa pole, nguvu zilimuishia
alikata tamaa, na majuto ya hali ya juu, kila
tendo baya alilokuwa akimfanyia mkewe lilimjia
kichwani.
*********************
“Mama Jose njoo umnyonyeshe mtoto analia
toka muda mrefu.” Ilikua ni sauti ya Mama yake.
Dennis alishtuka na kunyanyuka kuangalia, Mama
Jose ni mkewe na hakujua ni kwa nini Mama
yake alikuwa anamwambia aje kumnyonyesha
mtoto wakati alishafariki dunia.
Kabla hajasema chochote Mama yake aliingia
kisha, “Ohhh Dennis umekuja? Nikajua utakuja
baadaye kazi zimekubana, mkeo alisema
hupatikani kwenye simu.”
Dennis alizidi kuchanganyikiwa, alibaki na
mshangao. Mara mkewe aliingia, hapo ndipo
alichanganyikiwa zaidi, alishtuka kama vile
ameona mzimu, kidogo amdondoshe mtoto
aliyekuwa amempakata.
“Vipi Baba Jose…” Mkewe alimuuliza kwa maana
namna alivyokuwa akimuangalia haikuwa
kawaida yake. “Uko hai mke wangu?” Alijikuta
anauliza. “Ndiyo kwani vipi ulitaka nife?” Mkewe
alijibu kwa kebehi kidogo kwani alijua ni dharau
ya mumewe.
“Lakini Mama......” Dennis aliongea kwa
kushangaa huku akimuangalia Mama yake. Mama
yake alitabasamu na kumwambia, "Aliyefariki ni
Bibi yako si ndiyo alikuwa anakuita mume
wangu?
"Wewe mbona kila siku ukipiga simu unaulizia
mke wangu hajambo." Dennis alipumua kwa
nguvu huku akikaa chini, mkewe alimchukua
mtoto kwenda kumnyonyesha. Denis alimfuata
huko huko chumbani, alipiga magoti mbele yake
na kusema, “Samahani mke wangu nilikuwa
sijajua thamani yako mpaka leo. Yaani leo ndiyo
nilichanganyikiwa, nilijua umekufa na tayari
nilishaona maisha hayawezekani bila wewe.
Ninaahidi nitabadilika nitakuwa mume mwema na
kamwe sikunyanyasi tena."
Mama yake ambaye alisimama mlangoni
alitingisha kichwa na kucheka huku akisema,
“Unavyoringa uachiwe watoto kila siku, unajua
uchungu wa kulea wewe au unataka uachiwe ili
uje kunitupia wanao hapa nianze kulea
wajukuu?!”
Hakusubiri hata jibu aliondoka akimuacha
mwanaye akiendelea kuomba msamaha akiwa
haamini kuwa mkewe yu hai. Siku ile ndiyo
ilikuwa siku ya Mabadiliko kwa Dennis kwani
hakuwahi kumpiga wala kumnyanyasa tena
mkewe.
*****MWISHO******
Jee umejifunza chochote ???????????
 
Inafunza sana hasa kwa wanaume wanaopenda kunyanyasa wake zao kuna watu natamani wangepita hapa wakasoma
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…