Na Saleh Ally GPL
MABINGWA wa Afrika, TP Mazembe ya DR Congo imekubali kutoa kitita cha Sh milioni 273 kwa Simba ili iwachukue wachezaji wawili tu.
Mazembe imekubali kutoa dola 100,000 kwa Mbwana Samatta (pichani juu) na dola 80,000 ili imnase Patrick Ochan (pichani chini) hivyo kufanya imwage Msimbazi jumla ya dola 180,000 (Sh milioni 273).
Kwa upande wa Samatta kila kitu kimekamilika na Simba imekubali kuchukua dola 100,000 huku ikisubiri TP Mazembe imalizane na Ochan ambaye yupo Lubumbashi kwa ajili ya makubaliano.
Pamoja na kuilipa Simba kitita hicho, Mazembe imeonyesha jeuri ya fedha kwa kukubali kutoa dola 50,000 (Sh milioni 75) kwa Samatta.
Makubaliano ya Samatta yamefikiwa Ijumaa iliyopita katika hoteli ya Movenpick jijini Dar es Salaam lakini kumekuwa na mvutano katika suala la mkataba huo uwe wa miaka mingapi.
Mazembe inataka kuingia mkataba wa miaka mitano kitu ambacho hata kwa sheria za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) si sahihi.
Lakini ukiachana na hivyo, wanataka Simba isiwe na haki tena na Samatta. Hii si sawa pia kwa kuwa akiuzwa huko mbele hatutafaidika, kilisema chanzo.
Kuhusu suala la Ochan, inaelezwa kuwa Mganda huyo naye anataka kulipwa dola 50,000 kama zilizotolewa kwa Samatta wakati timu hiyo imekubali kutoa dola 25,000 (Sh milioni 37,000).
Akizungumzia suala hilo, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange Kaburu alielezea kwa ufupi tu.
Suala la Samatta tumemalizana, ingawa kuna vipengele kadhaa tunamalizia vizuri na tayari tumetoa ruhusa, ila yeye anakwenda Lubumbashi wiki ijayo kusaini mkataba. Kuhusu Ochan, yupo huko huko sasa tunasubiri wamalizane naye maana tumewapa ruhusa ya kuzungumza naye, alisema Kaburu.
Kutokana na fedha hizo, maana yake Simba ina nafasi ya kufanya usajili wa uhakika kama wahusika watatuliza akili.