Marekani imemfungilia mashitaka mapya muasisi wa tovuti ya uvujishaji wa nyaraka za siri Wikileaks, Julian Assange, ikimtuhumu kwa kuiweka Marekani katika kitisho cha kukumbwa na "madhara makubwa" kwa kuchapisha nyaraka mnamo mwaka wa 2010.
Mashitaka hayo 17 yaliyowasilishwa na waendesha mashitaka wa Wizara ya Sheria yanadai kuwa Assange alisaidia katika wizi wa nyaraka za siri, na akazichapisha hovyo taarifa za siri.
Muasisi huyo wa Wikileaks sasa anakabiliwa na jumla ya mashitaka 18 ya uhalifu, na huenda akakabiliwa na adhabu ya kutupwa gerezani kwa miongo mingi kama atahamishwa kutoka Uingereza na kuhukumiwa nchini Marekani.
Waendesha mashitaka wanamtuhumu Assange kwa kumuagiza aliyekuwa mtaalamu wa ujasusi wa jeshi la Marekani Chelsea Manning kutafuta na kisha kuvujisha taarifa za siri zenye kusababisha uharibifu mkubwa.
DW