IDADI ya watalii walioingia nchini imeongezeka kutoka 1,327, 143 mwaka 2017 hadi kufi ka watalii 1,505, 702 mwaka 2018 na ongezeko hilo limechangia kuongezeka kwa mapato yatokanayo na utalii kutoka dola za Marekani bilioni 2.2 mwaka 2017 hadi kufi kia dola za Marekani bilioni 2.4 mwaka 2018.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla akiwasilisha bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/10 alisema mafanikio hayo yametokana na jitihada mbalimbali za kutangaza vivutio vya utalii kupitia maonesho mbalimbali ndani na nje ya nchi, kutangaza vivutio vya utalii kupitia vyombo vya habari ndani na nje ya nchi.
Alisema pia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imeanzisha chaneli maalumu kutangaza vivutio vya utalii ambayo itasaidia kuwavutia wageni wengi kutembelea nchini na kwamba wizara ya maliasili na utalii imeendelea kuchangia katika kugharamia uanzishaji na uendeshaji wa chaneli hiyo.
Waziri huyo alisema katika kuendeleza utalii, wizara imeendelea kufanya jitihada za kupanua wigo wa mazao ya utalii ikiwa ni pamoja na utalii wa fukwe, utalii wa mikutano, utalii wa meli, utalii wa majini, utalii wa michezo, utalii wa utamaduni na kuanzisha shughuli mpya ya utalii katika maeneo ya hifadhi.
Alisema idara ya utalii imepewa jukumu la kuandaa na kusimamia sera, sheria, kanuni na miongozo ya kuendeleza utalii na kuwa wizara imeendelea kufanya kaguzi za mara kwa mara kwa wakala wa biashara za utalii katika mageti ya hifadhi za Taifa, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Pori la Akiba Selous ili kuhakikisha kuwa wanazingatia sheria, kanuni na miongozo iliyopo.
Waziri Kigwangalla alisema katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu, Wakala wa Biashara za Utalii 1,330 walisajiliwa na kupatiwa leseni za kufanya biashara ya utalii kwa kutumia mfumo funganishi wa kielektroniki.
Katika hatua nyingine, wizara imefanya uhakiki wa huduma ya malazi 428 katika Mkoa wa Dodoma na kati ya huduma za malazi zilizohakikiwa, 45 zimekidhi vigezo vya daraja la ubora na imekamilisha maandalizi kwa ajili ya kuhakiki na kupanga huduma za malazi katika viwango vya ubora wa nyota moja hadi tano katika mikoa ya Mwanza, Kilimanjaro na Tanga.
Alisema pia wizara imebaini vivutio 59 vya utalii na maeneo ya uwekezaji kwa ajili ya shughuli za utalii katika mikoa ya Ruvuma na Kigoma na pia kwa kushirikiana na halmashauri za wilaya na sekta binafsi itaboresha na kuanza kuvitangaza vivutio hivyo ndani na nje ya nchi.