Vitu vingi sana husababisha matatizo ya ufisadi na wizi na matumizi mabaya ya ofisi za serikali, kwa kiswahili cha awamu ya tano linatumika neno majipu kumaanisha mambo yote hayo.
Uwezo mdogo wa maofisa wanaopewa ofisi kubwa za kiserikalini, wanakuwa mzigo na mambo mengi ya kitaalam yanawapiga chenga, matokeo yake wale wanaokuwa chini yao wanaichukulia nafasi hiyo katika kuiibia serikali kwani wanajua bosi mkubwa yupo kwenye cheo chake lakini ni "mtupu" kiuwezo.
Kulipa fadhila, kwa maana ya mtu anapewa cheo fulani serikali na mtu fulani, hivyo muda wote wa uwajibikaji wake anakuwa yupo kwenye mchakato wa ulipaji wa fadhila kwa yule aliyempigania mpaka akapata cheo alichonacho. Huyu aliyepiganiwa mpaka akawa bosi anakuwa ni mateka wa yule aliyempa ulaji, wanakula pamoja, wanatengeneza networks chafu za ulaji.
Kuna ile tabia ya mtu kutazamwa katika mtazamo wa kuingilia riziki za watu. Wapo wataalam ambao wanafanya interview vizuri sana, maprofesa wa vyuo vikuu wanasimamia interview wanaukubali uwezo wao. Majina yanapelekwa Ikulu, kiongozi mkuu wa awamu ya nne anawakubali na anarudishia faili kwa katibu mkuu wa wizara, huyu katibu mkuu kwa sababu anakula na yule mtu ambaye anakaimu ukurugenzi, anaamua kulificha lile faili ili lisimfikie waziri mwenye dhamana ya kukubaliana na ujumbe uliotoka kwa rais. Yaani katibu mkuu wa wizara na kaimu mkurugenzi wote wawili wanakuwa ni tatizo kwani wanamnyima mtu mwenye uwezo na sekta husika ile nafasi ya kuitumia elimu kwa faida. kwa hiyo mitandao kama hiyo ya urafiki na yenyewe imekuwa ikichangia katika uwepo wa majipu kila siku ndani ya mfumo wa uongozi.
Zipo sababu nyingi zinazosababusha uibukaji wa majipu, wakati mwingine tamaa za kibinadamu. Mtu anatamani kuw ana nyumba kama ile ambayo anaiona kila siku asubuhi pale Mbezi Beach wakati akipita na gari yake kutokea Tegeta akielekea ofisini posta mpya. Hiyo nyumba anayoiona thamani yake ni shilingi milioni 500, ili aweze kuijenga kwa pato lake, haiwezekani, hivyo kinachofuata ni kuchora michoro ya wizi.
Nadhani hizo ni baadhi tu ya sababu zinazochangia uwepo wa majipu ndani ya serikali, ndani ya awamu zote tano.