MATUMIZI ya teknolojia ya kadi kabla ya kupata huduma ya maji wilayani Karatu mkoani Manyara imesaidia kuongeza ukusanyaji wa mapato kwa asilimia 187 na kupunguza upotevu wa maji.
Akiwasilisha mada katika Wiki ya Ubunifu juzi jijini Dar es Salaam, Mhandisi wa Maji kutoka Shirika la Catholic Relief Service (CRS), Ephraim Tonya alisema kuanza kutumika kwa teknolojia hiyo ni baada ya kupata ufadhili kutoka Mfuko wa Ubunifu na Maendeleo ya Watu (HDIF).
Tonya alisema kuwa kabla ya kutumika kwa mfumo huo, asilimia 30 ya maji yalikuwa yakipotea kutokana na watu kuyachezea na kwamba hata ukusanyaji wa mapato haukuwa mzuri. Alieleza kuwa waliona haja ya kubuni njia mbadala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(Tehama) ili kuwezesha ukusanyaji wa mapato ambazo zitatumika na halmashauri pamoja na kudhibiti upotevu wa maji bila sababu maalum.
“Tulikuja na teknolojia mpya ya kutumia kadi ambapo malipo hufanyika kabla ya kuchota maji na kukatisha malipo ya baada. Kwanza, tuliboresha miundombinu kwa kichimba visima ili mwananchi anapolipia huduma hii aweze kuipata kwa wakati. Kwa njia hiyo tulifanikiwa kuongeza mapato kwa asilimia 187 ambazo ni mara mbili ya kusudio letu la ukusanyaji wa mapato,” alisema.
Aliongeza kuwa fedha zilizokuwa zinapatikana katika mradi huo zimewezesha vikundi vilivyokuwepo kwa kufanya marekebisho ya haraka kwenye miundombinu hiyo na kuboresha miundombinu ya maji ili kutatua tatizo lolote linaloweza kusababisha ukosefu wa maji kwa wakati.
Kwa upande wake, Mtati kutoka Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Arusha, Hans Komakech alisema kabla ya kuanzisha mfumo wa malipo kabla waliangalia kama mfumo unatumika vizuri na kwamba hakuna mtu yoyote anayeachwa kwa sababu ya ugumu wa teknolojia hiyo. Alisema pia waliangalia namna mapato yanayopatikana upande wa maji kwamba yanaweza kutumiwa na mamlaka za maji kuwekeza katika miundombinu ya maji sa katika maeneo mengi