Tunaendelea sehemu ya nne!
Baada ya kugundua nilikuwa nimepakwa dawa, ambazo zilikuwa za unga unga za rangi nyeusi na nyekundu. Wazo la kwanza nilifikiria kuoga kuziondoa zile dawa, Lakini kwa sababu bafu lilikuwa ni la nje niliogopa kutoka nje, ningepata wapi ujasiri kwa mazingaombwe ambayo nimekuwa nikiyashuhudia. Nikapata wazo nijifute tu na kitambaa, nikachukua kitambaa nikakilowesha maji nikaanza kujifuta mle mle chumbani. Baada ya pale nikaona sikuwa na jambo lingine la kufanya zaidi ya kusali kuomba msaada wa Mwenyezi Mungu, yeye ndio kimbilio la wanyonge. Nilipiga magoti nikasali, nikamaliza nikazima kibatari nikarudi kitandani kulala. Usiku ule sikupata usingizi kabisa, ulikuwa ni usiku wenye mchanganyiko wa hisia za hasira, uoga na fadhaa. Wazo ambalo liliisumbua akili yangu niliamini kabisa ile ndoto ina uhusiano na hili tukio. Nilikumbuka kanisani tulifundishwa Mungu wakati mwingine huwapa ujumbe watu wake kupitia ndoto. Ndivyo alivyofanya kwa Yusufu, Daniel na baba wa imani Ibrahim. Niliamini ile ndoto itakuwa na uhusiano wa moja kwa moja na tukio lile. Nilipata mawazo matatu juu ya nini nifanye
Wazo la kwanza nilifikiri kesho yake asubuhi nirudi nyumbani nikawaambie wazaz wangu juu ya tukio lile lililotokea.
Wazo la pili nilifikiri niongeze bidii ya kusali halafu nisubiri hadi weekend nikirudi nyumbani, niwaambie baba na mama.
Wazo la tatu nilifikiri nimtafute msichana yule niliyemuota amenibeba kwenye baiskeli (tumpe sasa jina la Vumilia). Niliamini huyu kuna kitu atakuwa anakijua.
Nilichakata mawazo yote nikaona niende na wazo la kusubiri hadi weekend ndio niende nyumbani huku nikiongeza maombi. Mama yangu ni msabato kupita maelezo, na nimelelewa katika maadili ya kuishika imani hivyo niliamini Mungu atatenda. Kwa ufupi nitumie hii fursa kuwakumbusha hata wazazi mnaosoma hiki kisa, muwalee watoto wenu katika njia ipasayo nao hawataiacha hata watakapokuwa wazee, Mithali 22:6 . Sio mnafanya umalaya, kuvaa vinguo vifupi na kupost picha mkivuta shisha mbele ya macho ya watoto wenu. Mkijidanganya ndio usomi na usasa, kumbe ni ushamba na kukosa elimu. Siku hiyo pia nilikumbuka fungu la Hesabu 23:23 hapana uchawi juu ya Yakobo wala, wala uganga juu ya Israeli. Niliamini Mungu atatenda!
Anyway sipo hapa kwa ajili ya mahubiri! Tuendelee na kisa chetu!
Wazo la kwanza nililikataa kwa sababu niliona kuharakisha kuwaambia lingewapanikisha wazazi wangu, na sikupenda hali hiyo. Nilimpenda sana mama na baba yangu hivyo nisingependa kuwaona wamefadhaika kwa sababu yangu.
Wazo la kumuuliza Vumilia niliona ni gumu kwa sababu ningemuulizaje mambo mazito kama yale kwa kigezo kipi na uthibitisho gani. Ingekuwa ni sawa nakusema namtuhumu yeye ni mchawi! Nisingeweza kufanya hivyo!
Nilipiga chini hilo wazo!
Asubuhi kulipopambazuka nilioga na kujiandaa kwenda shule kama kawaida. Sikumwambia yeyote juu ya kilichotokea na nilijitahidi sana kuficha zile chale zisije zikagundulika. Tulitoka ndani wote watatu na kuanza kutembea mdogo mdogo kuelekea shule. Tulikuwa tunatembea umbali wa kama nusu saa hadi kufika shule. Tulifika shule na kuendelea na ratiba zingine kama kawaida, japo kimawazo nilikuwa mbali sana. Zaidi zaidi nilikuwa napata hisia za uoga sana. Darasani vumilia alikuwemo nilitamani niamke kwenda kumuuliza, lakini nilikosa courage ya kuamua. Muda sio mrefu iligongwa kengele ya mpumziko mida ya saa nne. Wanafunzi wakatoka nje kupumzika, wenye pesa walienda canteen kunywa chai na maandazi.
Japo baba alikuwa ananipa pesa ya kunywa chai kila siku. Lakini siku hiyo sikuwa na mzuka hata wa kuinywa chai yenyewe. Nilitoka nikajitenga nikaenda kupanda kwenye jiwe moja refu, linalopatikana pale shule nikakaa angalau kupata vitamin D. Wakati nikiwa nimekaa pale ghafla nilimuona Vumilia akija na sahani yenye maandazi kwenye sahani mkono mmoja, mkono mwingine amebeba vikombe viwili vya Chai. Nilitamani nimkwepe lakini nikasema hapana ngoja nione atakuwa na jipya gani, nikajiapiza sitakunywa chai yake. Vumilia kiukweli alikuwa ni msichana aliyekuwa anavutia kwa kiasi chake, si haba. Ni msichana ambaye nisingekuwa kumuogopa bibi yake na undugu wa uongo na kweli uliopo kati yetu basi ningetamani kuwa naye. Alifika pale akaniambia nishuke chini nimpokee, mtoto wa watu sikuwa na hiyana nilishuka na kutii amri bila kuuliza kama niko jeshini. Alinikabidhi kikombe kimoja akaniambia "karibu chai"
"Asante leo sijisikii kula kabisa" nilijibu
"Hujisikii kwani umekula wapi, au unaogopa nitakuwekea dawa unipende"
Nilijichekesha kwa lengo la kupotezea!
Baada ya kukataa hakunibembeleza tena, alianza kunywa chai huku nikimkodolea macho hadi akamaliza. Alipomaliza aliniangalia kwa macho ya huruma kidogo kisha akasema
"Kuna kitu nataka nikwambie"
"Kitu gani" nilijibu haraka kwa pupa
"Mbona una haraka hivyo, uko sawa Kweli"
"Niko sawa we niambie tu"
Alikaa kimya kidogo baadae akaanza kuimba wimbo fulani kwa sauti ya chini, dizaini kama ananichora hivi
Aisee! Alivyoimba palepale kuna kitu nilikumbuka!
Huo wimbo ndio wimbo ambao wale wachawi walikuwa wanauimba siku ile nilipotoka ndani usiku. Kipindi nikiwa darasa la tatu 2005.
Daktari Ben Carson katika kitabu chake cha Think Big aliwahi kusema ubongo wa binadamu una seli zaidi ya bilioni moja. Seli hizi ni nyingi sana kiasi kwamba zinaupa ubongo uwezo mkubwa wa kutunza kumbukumbu nyingi kwenye maisha. Kuna jambo linaweza kuwa lilitokea miaka mingi pengine ukiwa bado mtoto ukadhani umeshalisahau, lakini siku ikitokea "stimuli" fulani kuhusiana na lile tukio, utakumbuka kila kitu kama unaangalia runinga. Maneno hayo ya huyo daktari yalithibitika kwangu siku hiyo!
Nilikumbuka haswa ule wimbo niliusikia ukiimbwa siku ile. Kumbukumbu zangu zilinichukua hadi usiku ule nikiwaona wanawake kwa wanaume wakiwa wameshika myoto na wamevaa nguo nyeusi wakiimba na kunengua.Baada ya kumbukumbu hiyo kwa Vumilia Sikutaka kuuliza chochote kwa sababu yeye mwenyewe Vumilia aliwahi kuniambia alikuwepo siku ya tukio. Alivyoona sijaongea chochote aliniuliza
" Jana usiku ulikuwa wapi?"
Nilichanganyikiwa kidogo na lile swali, wakati mwingine nilijiona geneous kwa kudhani toka mwanzo ni lazima kuna kitu Vumilia atakuwa anafahamu.
" Nilikuwa getto tu kwani kuna nini" nilijifanya sielewi
"Sema ukweli mr the dragon jana hujachanjwa chale wewe Kweli?"
Nilishtushwa na taarifa ile ni kama nilikuwa siamini kama Vumilia kweli anajua kuhusiana na tukio lile.
"Hamna" nilikanusha
"Mmmh! Labda lakini kama unanidanganya na tayari umeshachanjwa chale, jua unajidanganya mwenyewe" alikaa kimya kidogo kisha akaendelea
" Ndio unajidanganya mwenyewe! Maana kama umeshachanjwa chale tayari wewe ni nusu mfu nusu hai! Usipoharakisha kutafuta tiba utaitwa marehemu na mimi nipo hapa kwa ajili ya kukusaidia"
"Nimechanjwa" nilikurupuka kujibu pasipo kujiuliza kama ni jambo sahihi au sio sahihi kujibu vile. Uoga ulikuwa umenitawala isivyo kawaida
"Sasa na ulivyokuwa unanificha,ulitegemea nini"
"Naomba unisaidie unajua ni kama nimechanganyikiwa tokea nilivyogundua hilo usiku wa jana nimechanjwa"
Nilivyomwambia hivyo alivuta pumzi ndefu kama mtu aliyekuwa ananionea huruma.
"Kuna kitu nataka nikwambie ila usiogope, unahitaji kuwa jasiri" alikaa kimya kisha akaendelea!
"Kama umeshachanjwa chale mpaka hapo maisha yako, yako mikononi mwa wachawi waliokuchanja, Wewe unaonekana mizimu ya ukoo wa kwenu ina nguvu sana lakini pia umezaliwa na nguvu fulani za asili"
"Kwa nini"
"Unajua wachawi kabla hawajamloga mtu ni lazima waijue kwanza nguvu yake inayomlinda hasa kimizimu. Maana ili mchawi akuloge kwanza kabisa huwa kuna makubaliano baina yake na mizimu yako yaani ya upande wa baba yako pamoja na mama yako, makubaliano yakishindikana haulogeki kamwe, labda atakutesa tu ila hawezi kukuua. Ukionekana mizimu ya kwenu ni mikali na makubalino hayawezi kuwepo ni lazima kuna tambiko lifanyike likihusisha kafara ya kondoo mweusi ili kuua nguvu zako. Sasa kilichofanyika jana wachawi wamekuja kukuchukua usiku wakakupeleka hadi kwenye makaburi ya ukoo wenu upande wa baba yako. Wakafanya tambiko lao, ambalo ndio lilihusisha wewe kuchanjwa chale. Baada ya kumaliza ndio wakakurudisha. Na tambiko hilo likishafanyika unakuwa hauna nguvu tena inayokulinda kimizimu hivyo mchawi kukuloga ni kazi nyepesi zaidi ya kusukuma mlevi. Hivyo nguvu zote zilizokuwa zinakulinda wewe zimeshaondolewa na sio muda mrefu wataanza kukushughulikia na nina uhakika usipofanya jitihada kutatua hiyo shida wiki moja humalizi"
Mpaka hapo nilikuwa nimechanganyikiwa kijasho chembamba kilikuwa kinanitoka. Swali ambalo nilijiuliza ni kwa nini wanataka kuniua, nimewakosea nini na wamejuaje yalipo makaburi ya ukoo wa baba yangu ilhali ni kijiji kingine kabisa japo ni jirani.
"Kwa nini sasa wanataka kuniua nimewakosea nini"
"Hata mimi sijajua bado lakini huwezi amini wanaotaka kukufanyia hivyo ni ndugu zako kabisa"
"Heeeeh! Wakina nani hao?"
"Utawajua tu tena utajionea kwa macho yako mwenyewe"
Nilimuuliza tena
"Wamejuaje yalipo makaburi ya ukoo wetu"
"Wachawi ni shirika kubwa lenye ushirikiano mkubwa, hakuna ukoo usio na wachawi. Na huwa wanasaidiana kutimiza mambo yao" alinijibu
"Sasa naomba unisaidie" niliomba kwa unyenyekevu
"Nitakusaidia ila mpaka ukubali sharti langu"
"Sharti gani"
"Uwe mpenzi wangu kuanzia leo na ukubali kuja kunioa"
Ulikuwa ni uamuzi mgumu kuufanya lakini kwa sababu niliogopa sana. Niliamua kukubali bila kufikiria mara mbili. Niliona ngoja kwanza nipambane na kifo baadae ndio nipambane na mapenzi.
"Asante kwa kukubali, Mr the dragon nimefanya hivi kwa vile nakupenda tu, nakupenda tokea tukiwa wadogo. Na ujue mimi ni miongoni mwa watu wachache ambao wanaweza kukuonyesha njia ya kukusaidia. Nasema hivyo kwa sababu mimi naijua siri iliyoko kwenye mwili wako ambayo bila hiyo siri kuifumbua hakuna mtu anaweza kukusaidia"
"Siri gani"
"Kuhusu hiyo siri nitakwambia muda mwingine, tupambanie maisha yako kwanza, usiku nitakuja kukuchukua twende sehemu ila unahitaji uwe jasiri. Tukishamaliza hili suala sitegemei utaniacha" alisema Vumilia
Baada ya mazungumza hayo tulielekea darasani sikuamini kama nilikuwa katikati ya bonde la kifo na uzima. Ni kama nilikuwa nimechanganyikiwa nikimkumbuka mama yangu, baba yangu, kaka, dada na marafiki zangu halafu lisipofanyika jambo ndani ya wiki moja nitakuwa nimewaacha wote. Sikupata hata mood ya kuendelea kukaa darasani nilichukua begi langu nikatorokea porini na kuanza kutembea mdogo mdogo kuelekea getto. Njiani machozi yalinibubujika mashavuni. Wakati mwingine niliiangalia ardhi na kutabasamu mwenyewe yaani mimi huyu mr the Dragon kijana barobaro wa shule ndani ya wiki hii nitakuwa nimefukiwa na hii ardhi ninayoikanyaga. Ama kweli dunia ni uwanja wa fujo kila mtu atafanya fujo zake na kuondoka!
Lakini pia niliyawaza maneno aliyoniambia Vumilia kwamba kuna ndugu zangu ndio wanataka kuniua, nilijiuliza ndugu gani huyo lakini sikupata jibu. Nilijiapiza sitomsamehe kamwe kama nitapona.
Itaendelea baadae kidogo ngoja nipate lunch!