Ni tatizo la matamshi linalomfanya mtu asiwe na mpangilio wa moja kwa moja wa maneno na sauti anazotoa.
Watu wenye kigugumizi hufahamu maneno wanayotaka kutamka lakini hupatwa na ugumu katika kutengeneza mtitiriko wa matamshi hayo.
Changamoto hii inaweza kuambatana na tabia za kufumba macho, kukakamaa kwa misuli ya uso pamoja kutetemeka kwa midomo wakati wa kuzungumza. Pia, mambo yafuatayo huonekana-
- Ugumu wa kuanzisha na kutamka maneno
- Kuvuta sana neno au sauti kwenye matamshi
- Kurudia kwa maneno
- Kuongeza maneno ya ziada mfano “um..” kati ya neno moja na lingine
Hali ya kigugumizi huwa mbaya zaidi wakati wa furaha, uchovu au pindi mhusika anapokuwa na stress kubwa za kimwili na kiakili.
Sababu zinazofanya mtu apatwe na kigugumizi huwa hazipo wazi sana, lakini huhusianishwa na uwepo wa changamoto kwenye sehemu ya ubongo inayohusisha lugha na matamshi, jini za urithi (genetics) pamoja na udumavu wa mtoto kwenye hatua za awali za ukuaji.
Aidha, mtu anaweza kupata kigugumizi baada ya kupitia kiharusi au ajali yoyote kubwa inayohusisha kichwa na ubongo.
Tatizo hilo linalomfanya mhusika apunguze kujiamini, akwepe mazungumzo hasa yale yanayohusisha hadhara kubwa, ajihisi myonge pamoja na kudhihakiwa na watu wengine huwa halina tiba ya moja kwa moja isipokuwa hutegea umri wa mhusika, historia pamoja na matarajio yake.