MCT yamshukia Juma Nkamia
na Janet Josiah
KATIBU Mkuu wa Baraza la Habari Nchini (MCT), Kajubi Mukajanga, amemshukia Mbunge wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia (CCM), aliyeponda shughuli za baraza hilo.
Akizungumza na Tanzania Daima jana Mukajanga alisema Nkamia anafahamu kuwa MCT ni NGO ambayo imeundwa na wadau wa habari wenyewe kwa ajili ya kushughulikia taaluma yao katika mambo mbalimbali na si vinginevyo.
Alisema wadau hao ni vyombo vyote vya habari yakiwamo magazeti, redio, televisheni, TEF na klabu mbalimbali za waandishi wa habari ambavyo alisema viko zaidi ya 100 hapa nchini.
Alisema kwa kuwa chombo hicho kimeundwa na wanahabari wenyewe na si cha kiserikali anafahamu namna kinavyofanya kazi na kwamba yeye (Nkamia) kama mwanatalaaluma amefaidika nacho.
"Sielewi Nkamia anazungumza nini; hakuna asichokifahamu kuhusu MCT kwa kuwa yeye kama mwandishi ni mwanachama na ameshafanya shughuli nyingi zinazowahusu wanahabari kwa manufaa yao," alisema Mukajanga.
Alisema kabla hajawa mbunge, akiendelea na kazi yake ya uandishi wa habari aliwahi kusafiri na wenzake kwenda nchini India kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na mambo mengine na wanahabari wenzao kupitia MCT na kuitisha mkutano kwa wanahabari wenzake alijifunza kutoka huko.
Aidha Mukajanga alisema kwa kuwa NGO hiyo ina wenyewe, pia ina bodi kamili ambayo inaongozwa na mwenyekiti wake Jaji Mstaafu Robert Kisanga.
Mei 21 mwaka huu wakati akichangia makadirio ya matumizi ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa mwaka wa fedha 2013/2014 Nkamia alihoji shughuli zinazofanywa na MCT pamoja na Jukwaa la Wahariri (TEF).
Nkamia aliitaka serikali kuharakisha Muswada wa Sheria ya Vyombo vya Habari kwa madai kuwa utasaidia kuboresha tasnia ya habari nchini.
Alisema sheria hiyo ikianza kufanya kazi itasaidia kuanzisha bodi ya kusimamia waandishi wa habari ambayo kwa sasa haipo kwani MCT na TEF zinajiendesha kama NGOs zenye maslahi kwa watu binafsi.