KAIMU Mkuu wa Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, Dk Halfani Haule ametaka makaburi yote walipozikwa watu wenye ulemavu wa ngozi yajengwe vizuri na taarifa muhimu za marehemu ziandikwe vizuri kwenye makaburi hayo.
Alisema lengo ni kuondoa dhana potofu iliyojengeka kwenye jamii kuwa albino huwa hawafi bali wanapotelea kusikojulikana katika mazingira ya kutatanisha. Dk Haule ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga alieleza hayo alipokuwa akizindua mradi wa kupinga mauaji ya albino wilayani Nkasi katika mkoa wa Rukwa, huku akisisitiza kuwa walemavu hao wanakufa kama watu wengine.
Mradi huo unatekelezwa na Taasisi isiyo ya kiserikali ya Grace Community Development and Education (GCDE) katika kata kumi za wilayani Nkasi kuanzia Agosti mosi 2017 hadi Januari 2019.
Aliongeza kuwa licha ya kuwa hakuna tukio lolote la kuuwawa au kushambuliwa na kunyofolewa viungo kwa albino katika wilaya Nkasi, elimu na ulinzi iendelee kutolewa pia watu hao waendelee kutunzwa na orodha yao ifahamike rasmi.
“Walemavu hawa wanakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo uono hafifu, wengi wao wanakufa mapema kabla ya kufikisha umri wa miaka 40 kutokana na kushambuliwa na saratani ya ngozi, lakini baya zaidi wanaendelea kupata maumivu makali kwa kunyanyapaliwa na jamii ikiwemo kuhifadhiwa kwenye kambi kwa usalama wao kama iliyotokea katika mkoa wa Shinyanga.
Pia kuhifadhiwa kwenye shule maalumu kwa ajili ya usalama wao katika ilivyo katika Shule ya maalumu iliyopo katika Manispaa ya Sumbawanga,” alisisitiza. Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa GCDE, Batister Mbwana alisema katika utekelezaji wa mradi huo vitaanzishwa vilabu viwili vitakavyohusisha watoto wenye uelemavu wa ngozi na wasio walemavu, ili kuwajengea mahusiano mazuri na kuondoa unyanyapaa.