Boris Johnson alivyokiangusha chama cha Labour

Rubawa

JF-Expert Member
Joined
Dec 25, 2015
Posts
2,055
Reaction score
3,267
BARAZANI

Boris Johnson alivyokiangusha chama cha Labour

Na Ahmed Rajab

Tunauzungumzia usiku wa Alhamisi iliyopita. usiku wa kutangazwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Uingereza wa Desemba 12, 2019.

Usiku wa kimbunga kilichozitikisa siasa za Uingereza na ambacho nusura kikigharikishe kabisa chama kikuu cha upinzani cha Labour.

Kulikuwa na fununu, tangu usiku huo ulipokuwa mchanga, kwamba chama cha Labour chini ya uongozi wa Jeremy Corbyn kitapata kichapo ambacho hakitoweza kukisahau kwa miaka kadhaa ijayo. Sio wengi walioziamini fununu hizo.

Wengi walikubali kwamba huenda chama hicho kikashindwa lakini si kwa kishindo kilichodhihiri. Na kuna waliofikiri kwamba chama cha Labour huenda hata kikajinyakulia ushindi, ingawa wa chupuchupu.

Hakuna aliyeyafikiria maafa yaliyokuwa kama kivuli yakikiandama chama cha Labour usiku huo. Na kama walikuwepo basi walikuwa ni wachache mno.

Jambo la kushangaza ni kwamba katika uchaguzi uliopita wa 2017 Corbyn nusura amuangushe Theresa May, waziri mkuu wa wakati huo. Ilikwendaje hata safari hii wabunge 60 wa chama cha Labour wakashindwa?

Ilikuwaje hata Corbyn na chama chake wakashindwa katika maeneo ambayo kwa miaka na dahari yamekuwa yakiwapigia kura? Mengi ya maeneo hayo yako sehemu za kati na kaskazini mwa Uingereza, kwenye viwanda vingi. Pia Labour kimepata pigo kubwa katika majimbo ya uchaguzi ya Wales ambayo kwa muda miaka mingi yamekuwa yakiwachagua wabunge kutoka chama cha Labour.

Maeneo yote hayo, na hususan yale ya kati na kaskazini mwa Uingereza ni yenye kuonekana kuwa ni “nyumbani” kwa chama cha Labour. Ni maeneo ya wavuja jasho, ya wafanyakazi wenye kufanya kazi za sulubu, maeneo ambayo kwa sasa wakaazi wao wengi hawana ajira na maisha yao ni magumu. Ajabu ya mambo juu ya dhiki zao wamehiyari kuwachagua wabunge wa chama ambacho kwa kawaida sera zake huwaumiza wafanya kazi.

Wapigaji kura katika maeneo hayo wamefanya kitu kama miujiza kwa kukiacha mkono chama chao asilia cha Labour na kukikumbatia, kwa mara ya kwanza, chama cha Conservative, ambacho kwa muda wa miaka mingi kimekuwa kikiyapinga maslahi ya wafanyakazi.

Kuna wenye kuyaona matokeo ya uchaguzi huo kuwa ni yenye kuonyesha ushindi wa wakongwe kuwashinda vijana, wabaguzi kuwashinda wasio wazungu na ushindi kwa wale wenye kujali mustakbali wa sayari yetu na mazingara yake.

Chama cha Labour hakijawahi kushindwa vibaya hivi tangu 1935. Safari hiyo thuluthi moja ya wabunge wote wa chama hicho walishindwa, wakiwa pamoja na kiongozi wao mkuu, Ramsay MacDonald, baba yake Malcolm MacDonald aliyekuwa gavana mkuu wa mwisho wa Kenya (1963-1964).

Chama cha Conservative kiliwahi kushinda kwa kishindo kama hiki. Iiikuwa 1987 aliposhinda Margaret Thatcher na kuwa waziri mkuu wa kwanza wa kike Uingereza. Kwa ushindi wake wa juzi, kuna wasemao kwamba Boris Johnson amegeuka na kuwa Margaret Thatcher mpya.

Matokeo ya uchaguzi huo yanalazimisha kupanguliwa kwa safu za mbele katika siasa za Uingereza hasa kwa upande wa vyama vya upinzani.

Corbyn amechaguliwa mbunge kwa mara ya kumi tangu 1983. Ameshinda kwa kishindo kwa kupata kura nyingi zaidi ya zile za Boris Johnson katika majimbo yao ya uchaguzi. Corbyn amepata asilimia 64.3 ya kura za jimbo lake na Johnson amepata asilimia 52.6.

Lakini ushindi binafsi wa Corbyn hauyafichi masaibu yaliyokikuta chama anachokiongoza. Kwa sababu hiyo ametangaza nia yake ya kujiuzulu. Yumkini uchaguzi wa kumchagua kiongozi mpya wa chama cha Labour utafanywa Januari 7, 2020.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vimekwishaanza ndani ya Labour kuwania nafasi za kiongozi mkuu na wasaidizi wake.

Jimbo la uchaguzi la Sedgefield ambalo miaka ya nyuma lilikuwa likiwakilishwa bungeni na aliyekuwa waziri mkuu Tony Blair limeponyoka kutoka mikono ya Labour na limemchagua mbunge wa Conservative. Lakini mtu angetarajia nini wakati Blair mwenyewe amekuwa kigeugeu kuhusu chama chake na akitahadharisha kwamba Corbyn hafai kuwa waziri mkuu.

Jo Swinson, kiongozi wa Liberal Democrats, chama cha tatu kwa ukubwa, ameshindwa kwa kura 147 tu kulinyakua jimbo lake huko Uskochi. Lakini kushindwa ndo ameshindwa na chama chake kitabidi kitafute kiongozi mwengine.

Nigel Dodds, kaimu kiongozi wa chama cha Ireland ya Kaskazini cha Democratic Unionist Party (DUP), aliyekuwa kiongozi wa chama hicho katika bunge la Uingereza alishindwa kwenye jimbo lake la uchaguzi. Kushindwa kwake ni pigo kwa chama cha DUP. Chama hicho sasa hakitokuwa tena na ubavu mbele ya mshirika wake mkuu, chama cha Conservative.

Kama tulivyoeleza wiki iliyopita vyombo vya habari vya Uingereza vimekuwa vikimuandama Corbyn, usiku na mchana, kwa takriban miaka minne tangu achaguliwe kiongozi wa chama chake. Vyombo vya habari vimekuwa vikimchimba na kumsingizia uongo wa aina kwa aina.

Ubaya wa wapiga kura wa Uingereza ni kwamba walijiachia watekwe na propaganda za vyombo vya habari hasa magazeti na televisheni. Waliacha kufikiri na wakaviachia hivyo vyombo vya habari viwe vinafikiri kwa niaba yao.

Ndipo walipolishwa yaliyo ya kweli na ya uongo kuhusu Corbyn. Na mengi waliyolishwa yalikuwa ya uzushi. Lakini waliyatafuna wakayameza.

Baadhi ya mambo ya uzushi yaliyowakera na kuwafanya wamchukie Corbyn hata hayaingii akilini.

Kwa mfano, kwamba Corbyn amekuwa akivaa kofia kama aliyokuwa akivaa Vladimir Lenin, mwanamapinduzi wa Urussi na mwana nadharia wa Kimarx.

Au kwamba amekuwa akiendesha baiskeli ya KiMao. Na usiniulize imekaaje baskeli ya aina hiyo kwa sababu siijui.

Lakini wako walioamini kwamba ipo baskeli aina hiyo, kwamba Corbyn amekuwa akiipanda na, kwa hivyo, kumfanya asifae kuwa waziri mkuu wa Uingereza.

Katika jaribio la kumkashifu Corbyn na kuzidi kumpaka tope vyombo vya habari vimekuwa vikimtuhumu kwamba amekuwa akiwasiliana na chama cha kigaidi cha IRA cha Ireland ya Kaskazini.

Vyombo hivyo hivyo vya habari vilijifanya kusahau kwamba mawaziri wakuu watatu wa zamani,Thatcher, John Major na Tony Blair wote walikuwa wakizungumza na IRA.

Uzushi mwingine aliokuwa akivumishiwa Corbyn ni ule wa kwamba yeye ni mbaguzi mwenye kuwachukia Wayahudi.

Huo ni uzandiki usio kifani kwa sababu kwa miongo kadhaa Corbyn amekuwa mstari wa mbele miongoni mwa wale wenye kuwalaani wenye chuki dhidi ya Wayahudi.

Hata hivyo, shutuma hizo za kwamba ana chuki dhidi ya Wayahudi zimemganda na zilipaliliwa na vyombo vya habari pamoja na hata mahasimu wake wa kisiasa ndani ya chama chake cha Labour.

Vyombo vikuu vya habari vya Uingereza zimekuwa vikizitumia shutuma za chuki dhidi ya Wayahudi kuwashambulia wenye kufuata siasa za mrengo wa kushoto na hasa zile za kisoshalisti.

Ni kweli Corbyn amekuwa mpinzani mkubwa wa Uzayoni na sera za serikali ya Israel dhidi ya Wapalestina. Wapenzi wa Israel wameugeuza upinzani wa Corbyn dhidi ya Israel na kuufanya uonekane kuwa ni chuki zake dhidi ya Wayahudi kwa jumla, jambo ambalo si la kweli.

Ni jambo lililo dhahiri kwamba kuna ujinga mwingi uliowagubika wapiga kura wa Uingereza.

Siku hizi siasa za Uingereza zimejaa sumu. Jengine lililojitokeza katika uchaguzi huu ni kwamba wapiga kura hawaoni kwamba kuna tofauti kubwa baina ya vyama vikuu vya Conservative na Labour.

Ilani ya uchaguzi ya Corbyn ilionesha kama kikitaka kurejea katika asili yake lakini wapigaji kura walipotoshwa na propaganda za wafuasi wa mrengo wa kulia na wakawababaisha.

Baada ya kusema yote hayo lazima tukiri kwamba chama cha Labour kinastahiki kulaumiwa kwa makossa ya kimkakati kilichoyafanya wakati na hata kabla ya kampeni ya uchaguzi.

Kosa kubwa kabisa ni la kuonekana kwenda kinyume na mchakato wa kidemokrasia wa kuitoa Uingereza kutoka Muungano wa Ulaya (EU).

Wananchi walikuwa wamekwishaamua 2016 kwamba Uingereza ijitoe kutoka EU. Labour hakikuwa na msimamo ulio wazi na madhubuti kuhusu suala hilo.

Kosa jengine lililofanywa na chama cha Labour ni ya kuyapuuza majimbo ya kati na kaskazini mwa Uingereza pamoja na ya Wales. Kikiamini kwamba majimbo hayo yatakiunga mkono tu.

Serikali mpya ya Johnson imeyalenga maeneo hayo na imeahidi kuingiza rasilmali nyingi za kuyanyanyua kiuchumi na kijamii maeneo hayo.

Ikitimiza ahadi hizo na ikaleta mageuzi yatayoyastawisha maeneo hayo basi ni muhali kwamba yatarudi tena mikononi mwa chama cha Leba.

Wakereketwa wa chama cha Labour wamebabaika na wameparaganyika. Ikiwa huyaoni machozi machoni mwao niamini nikikwambia kwamba yanatiririka nyoyoni mwao.

Machozi yao yatapokauka watabidi wakae, wajipime na kujitathmini na hatimaye waipange mikakati mipya na mbinu mpya za kuelekea uchaguzi ujao miaka mitano kutoka sasa. Mbinu na mikakati hiyo lazima izipiku sera mpya za serikali ya Boris Johnson.

Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Ahmed rajab fuata mkumbo

Kabla ya Uchaguzi alikuja na uwongo wake kuwa labor itashinda kwa kishindo

Akatoa sababu za ajabu kweli

Moja ya sababu ni kuwa ati Jeremy anaunga mkono kuundwa kwa dola la ki Palestine mashariki ya kati

Kaka rajab unazeeka vibaya
 
Na hili ndio lilikuwa lengo la uzi wake

Uzi wake uliopita kuhusu hili nilimeambia ni ujinga tu na Corby hawezi kushinda katu maana maislamu walishaanzisha vikundi vyao vya kupiga kampeni miskitini ili wamshushe Johnson kisa tu ana misimamo mikali juu yao😝😝
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…