Viongozi wawili wa klabu ya Simba -- mmoja wa kuchaguliwa na mwingine wa kuteuliwa -- wamejiuzulu katikati ya wiki huku wakitoka sababu ambazo, tunaona Nipashe, ni za kupotosha.
Makamu mwenyekiti Geofrey 'Kaburu' Nyange aliyekuwa akitegemewa kufanya makubwa na wanachama wa Simba walipomchangua, amekaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema amebwaga manyanga kutokana na, pamoja na mambo mengine kutukanwa na mashabiki.
Zakaria Hans Pope, mjumbe wa kamati ya utendaji na mwenyekiti wa kamati ya usajili amedai amejiuzulu nafasi zake za uongozi ili kutoa nafasi kwa wengine kuiendeleza Simba.
Ni ukweli ulio wazi kuwa viongozi hawa wamejiuzulu katika kipindi ambacho mwenendo wa Simba kwenye ligi kuu ya Bara na michuano ya kimataifa umekuwa mbovu pengine kuliko ambavyo imewahi kutokea tangu timu hiyo ilipolazimika kuifunga Yanga katika mechi yake ya mwisho ya ligi ya msimu ndipo isishuke daraja.
Ni ukweli ulio wazi pia kuwa kutokana na matokeo mabovu ya Simba ndani na nje ya nchi msimu huu, pamezuka kundi la wanachama linaloshinikiza viongozi kuachia ngazi baada ya kukosa imani nao.
Ni wanachama waliokosa imani na uongozi katika kuwezesha kurudi kwa heshima ya timu yao kwenye ligi kuu ya Bara na, pengine, Kombe la Kagame la klabu bingwa ya soka ya Afrika Mashariki na Kati katikati ya mwaka huu.
Kwenye ligi kuu ya Bara, kwa mfano, Simba inaweza kupata mafanikio yote ispokuwa kutetea ubingwa wake wa mwaka jana.
Lakini, kwenye michuano hiyo pia, kwa mara ya kwanza tangu miaka ya katikati ya 1980, Simba inaweza kujikuta nje ya timu tatu za juu katika michuano ambayo imetwaa ubingwa mara 19 -- tatu pungufu ya Yanga inayoshikilia rekodi.
Kwa nini Simba ipo katika hali ngumu kiasi hicho raundi nane kabla ya msimu wa ligi kumalizika?
Ni siri nyingine iliyo wazi.
Kwamba mwenendo mbovu wa Simba umetokana na usajili wa hovyo mara mbili wa wachezaji uliofanywa na uongozi wa klabu hiyo chini ya mwenyekiti wake Ismail Aden Rage.
Katika klabu ambayo usajili umefanywa na watu wasio na chembe ya taaluma ya ufundi wa soka wa kisasa, Simba ilianza ligi kuu ikiwa si tu na mapengo dhahiri katika usajili wake wa hovyo iliyofanya katikati ya mwaka jana, lakini pia ikikosa mshambuliaji halisi wa kati wa pili mwenye uhodari wa kufunga magoli uwanjani.
Na ikifahamika fika kuwa udhaifu wa Simba wa kutofunga magoli ya kutosha hasa kwenye mechi za mwishoni za duru la kwanzal la ligi kuu ya Bara ni kutokana na kasoro hiyo, uongozi ulifukuza kocha, ukasajili mlinda mlango na kutaraji si tu timu hiyo ifanye vizuri kwenye lala salama bali pia kuitoa Recreativo Libolo kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika.
Ndipo katikati ya mapungufu haya mwenyekiti wa kamati ya usajili anabwaga manyanga akidai anatoa nafasi kwa wengine kuongoza wakati lililo dhahiri ni kuwa anaonyrsha udhaifu wa pili -- kukimbia baada ya kuboronga kwenye jukumu alilokabidhiwa.
Akiwa makamu, mikono ya 'Kaburu' ni kama ilifungwa katika klabu ambayo imeonekana kuwa mwenyekiti amehodhi kila jukumu alilokabidhiwa na katiba.
Lakini, tunaona Nipashe, makamu mwenyekit hakupaswa kujizulu kwa sababu tu, eti, anatukanwa wakati kiini cha hasira za wanachama wa Simba ni udhaifu ulioonyeshwa na uongozi wake.
Ni mtizamamo wetu, Nipashe, kwamba viongozi hawa kwa vyovyote walistahili kujizulu kwa kushindwa kazi ama waliyoomba ama kuteuliwa kuifanya hivyo kutoa maelezo mengine yoyote nje ya hayo ni kuwakosea heshima wanachama ambao wameachiwa timu isiyo na matumaini yoyote ya kuwapa raha kwa kutwaa kikombe 2013.
Na kama tunaamini, Nipashe, kuwa 'Kaburu' na Hans Pope walistahili kuwajibika kwa kushindwa vibaya kuipa Simba kile ambacho wanachama walitaraji kutoka kwao, msimamo utakuwaje kwa Rage?
Rage aliyeteua mwenyekiti na kamati yake ya usajili, ambaye kwa sababu hiyo ni yeye HASA aliyeboronga usajili wa timu kiasi cha kutishia kukosa hata nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi kuu ya Bara.
CHANZO: NIPASHE