Yaliyojiri kwenye miaka 10 ya Mkutano wa Uhuru wa Mtandao Barani Afrika, Septemba 28, 2023

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,988

Tanzania ni Mwenyeji wa Miaka 10 ya Mkutano wa Uhuru wa Mtandao Barani Afrika (Forum for Internet Freedom in Africa 2023) ulioandaliwa na taasisi ya CIPESA kutoka Uganda katika Hoteli ya Hyatt Regency, The Kilimanjaro, Jijini Dar es Salaam kuanzia Septemba 27 hadi 29, 2023

Mkutano wa Uhuru wa Mtandao wa Afrika mwaka huu unaashiria muongo mmoja wa mkusanyiko mkubwa zaidi kuhusu uhuru wa mtandao barani Afrika. Mkutano huu ni jukwaa la kuhusisha kwa kina wadau mbalimbali katika kutambua masuala na changamoto muhimu zinazohusiana na haki za mtandao ambazo zinapaswa kushughulikiwa katika ngazi ya kitaifa na kikanda. Pia, unabainisha fursa za kuendeleza mjadala kuhusu umuhimu wa haki za kidigitali katika majukwaa ya kitaifa, kikanda, na kimataifa.

Kama Washirika wa CIPESA na Wachechemuzi wa Haki za Kidijitali, JamiiForums tutashiriki kikamilifu kwa kutoa mada kuhusu "Usimamizi wa Taarifa na Viwango vya Faragha Barani Afrika, Fursa na Changamoto Zake Sasa na Baadaye"

UPDATES

NEEMA LUGANGIRA, MBUNGE WA VITI MAALUM KUPITIA ASASI ZISIZO ZA KISERIKALI (NGO,S)

Nina furaha kubwa kuwa mkutano huu unafanyika Tanzania. Niliona jinsi mkutano huu ulivyo mkubwa na fursa zinazotokana nao. Niliomba CIPESA ikiwezekana tuufanye Tanzania na walikubali. Tuna wageni takriban 230 kutoka nchi mbalimbali za Afrika.

Neema Lugangira Jamiiforums.jpg

Mwaka 2024 tutakuwa na uchaguzi, tafadhali tuhakikishe mtandao unabaki wazi wakati huo. Tuhifadhi haki za binadamu na uhuru wa kutoa maoni wakati wa uchaguzi.

Tafadhali tuhakikishe mtandao unabaki wazi kwa sababu nataka watu waone ninachokifanya na wasikose nafasi ya kurudi Bungeni msimu ujao.

DK. WAIRAGALA WAKABI, MKURUGENZI - CIPESA
Asante kwa Wizara kwa kushirikiana nasi katika tukio hili.

Tulianzisha jukwaa hili miaka 10 iliyopita kwa sababu tuliona jukumu ambalo mtandao unaweza kulifanya na fursa unazoweza kuleta.

Leo tutazindua chapisho kuhusu hali ya uhuru wa mtandao barani Afrika, ambalo limechukua miaka 10 kuandaa. Ripoti hiyo inazungumzia masuala yanayosababisha kikwazo cha uhuru wa mtandao, inaonesha kinachoendelea kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Hitimisho letu ni kwamba mbele yetu bado kuna giza, lakini kuna upande mzuri wa hii. Inaweza kuwa kichocheo cha kuboresha Elimu, Afya na Sekta nyingine.

Leo, zaidi ya muongo mmoja uliopita, tuna changamoto nyingi katika enzi ya kidijitali. Kuna ongezeko la sheria, taarifa za uongo, ambazo zetu katika wakati mgumu sana.

Miaka michache iliyopita, jambo hili lisingekuwa limetokea. Kuna mabadiliko mengi yaliyofanywa na watu binafsi ambao wameona uwezekano na fursa zinazotokana na mtandao. Ni fursa kubwa sana kwetu kuwepo hapa, na tunashukuru sana kuwepo hapa.

NANCY KAIZELEGE, MWAKILISHI WA UNESCO
Taarifa zina jukumu muhimu katika jamii zenye demokrasia. Zinasaidia kupinga taarifa za uongo, kuzuia hotuba za chuki, na kuchochea uelewa. Zinasaidia kupambana na itikadi kali, kuhamasisha maamuzi yaliyo na msingi na kuongeza uwazi na uwajibikaji.

Hata hivyo, ili taarifa iweze kuchukua jukumu hili muhimu, watu wote lazima wawe na fursa sawa ya kuifikia/kuipata, na nchi lazima ziwe na katiba inayowaruhusu watu kupata taarifa.

Kwa sababu hii, UNESCO inafanya kazi ya kukuza na kulinda upatikanaji wa taarifa kama haki ya msingi ya binadamu na hatua muhimu kuelekea kufikia malengo endelevu ya maendeleo.

NAPE NNAUYE - WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI
Nina furaha kubwa kuwa pamoja nanyi leo katika FIFAFrica2023. Ni furaha yangu kuwakaribisha nyote hapa Dar es Salaam.

Mmechagua mahali sahihi kwa kuja Tanzania. Hapa ndipo tunapopata mlima mrefu pekee duniani, Mlima Kilimanjaro. Tafadhali jitahidini kufurahia muda wenu. Kwa wale wenye visa zinazokaribia kumalizika, nipo tayari kuwasaidia.

Nape Nnauye jamiiforums.jpg

Nape Nnauye, Waziri wa habari, mawasiliano na teknolojia ya habari
Tunashukuru kwa ushirikiano wa muda mrefu na nchi za Afrika na tunatarajia kupata njia zaidi za kufanya kazi pamoja na wapangaji sera wengine katika kanda hii, huku tukisimamisha jukumu la Afrika katika anga la kimataifa.

Biashara zinaenda mtandaoni na kugundua njia mpya za kujitangaza. Wananchi wetu wanajifunza mtandaoni na kuungana kwa njia ambazo hatukuzifikiria hapo awali.

Afrika sasa inasimama mbele kwenye ukuaji wa sekta ya Internet. Hata hivyo, internet pekee haitaikomboa Afrika, bali tunapaswa kufanya kazi pamoja kuboresha miundombinu yote ya kidigitali pamoja na kuwezesha ushahimilivu na ulinzi wa kimtandao.

Tunawezaje kuwafanya watu wote watumie intaneti, lakini pia tutawezaje kupunguza athari zitokanazo na matumizi haya? Tuuulizane, sio tu kwa jinsi gani wananchi wetu wanatumia nyezo za kisasa za kidigitali, bali uwepo wa usawa wa data za watu wanaotumia mitandao, au wale wanaotoa data hizo.

Afrika imeshuhudia ukuaji na upatikanaji mkubwa wa matumizi ya intaneti ukichangiwa na sera na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali zetu.

Nawasihi watoa mada, wajaribu kuzungumzia uhuru wa intaneti kwenda na mashambulizi ya kimtandao, ulinzi wa taarifa binafsi na ninauhakika kuwa maazimio ya hapa yatachagiza ubadilishwaji wa Sera za nchi zetu.

Tanzania imechukua hatua nyingi za kuhakikisha ufikiaji na uhuru wa habari unakuwepo, kuwapa watu wake maarifa na uwezo kwenye nyanja za kiutawala.

Serikali ya Tanzania imewekeza sana kuhakikisha ushirikishwaji wa watu kwenye matumizi ya mtandao unakuwa mkubwa. Mathalani, Juni 2023, jamii ya watanzania iliyofikiwa na mtandao wa 3G ilikuwa 77%, 65% na zaidi ya milioni 34 wanafikia intaneti.

DR. CHRIS BARYOMUNSI, WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA, UGANDA
Tumesikia kuhusu mapinduzi ya 1-3 ya teknolojia, sasa tunazungumza mapinduzi ya 4.

Sisi Afrika tumekuwa nyuma kwenye mapinduzi yote, na sisi kama viongozi tumejaribu kwenda sambamba na wenzetu na tulipofika ni kwa sababu teknolojia ndio inawezesha kila kitu, hatuwezi kuikimbia.

Maisha yajayo yapo kwenye digitali, . Ukitazama ramani ya Afrika inaonekana kama alama ya kuuliza, na madagaska ndio ile nukta. Bara letu linatuuliza, na ndio maana nimetoka Kampala kuja hapa kujadili namba gani tunafanikisha haya mapinduzi ya kidigitali.

NAPE NNAUYE - WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI
Tunapounganisha afrika na mtandao tusisahau pia maadili na tamaduni zetu. Tuhakikishe tunaunga watu wetu lakini pia tusisahau kuwalinda.

Tanzania ni ya pili barani Afrika kwa Usalama wa Mtandao na kwa sababu hiyo tuna kila sababu ya kulinda bara letu. Ni wajibu wa kila mtu kulinda kizazi chetu.

FELICIA ANTONIO, ACCESS NOW
Uzimaji wa intaneti ni suala lisiokubalika kwa sababu zozote zile.

Unapozima intaneti haizuii wala kusaidia chochote kama ambavyo Serikali huwa zinadai, intaneti ni suala la uhai na kifo.

Tunasisitiza Serikali zisichukulie suala la uzimaji wa intaneti kama kitu cha kawaida. Changamoto zizungumzwe bila kuingilia haki ya msingi ya watu katika kufurahia haki yao ya msingi.

Watoa huduma za intaneti wasikubali propaganda za Serikali zinazowataka kuzima intaneti. Badala yake, tuwekeze kwenye mifumo ya kushughulikia maudhui yanayodhaniwa kuwa yanahatarisha usalama badala ya kuzima kabisa mtandao.

MAXENCE MELO, MKURUGENZI MTENDAJI JAMIIFORUMS
JamiiForums inafikia watu zaidi ya milioni 3 kila siku na tunafahamika kama watu tunosaidia kufanikisha uwajibikaji Tanzania. Tuna mpango wa kufikia nchi 8 zaidi Afrika.

Tunawapa wananchi sehemu ya kuzungumza kwa uhuru bila wasiwasi. Tangu mwaka 2008 tumepitia mengi ikiwemo mimi kuitwa gaidi, kupoteza mapato na kufutiwa usajili, kupelekwa gerezani n.k lakini hatukuacha kujifunza.

Maxence Jamiiforums.jpg

Maxence Melo, Mkurugenzi Mtendaji JamiiForums​

Tulifanya utafiti na kuja na mambo mnayoyaona sasa kama Jamiicheck, sehemu ya kuhakiki usahihi wa maudhui yanayopatikana ndani na nje ya mtandao, lakini pia tunaendesha shindano la Stories of Change.

Kwa sasa tuna wanasiasa, taasisi za Serikali na wanasiasa ambao wamesajiliwa JamiiForums ambao akaunti zao zimethibitishwa (zimepewa blue tick). Wanajibu masuala mbalimbali ya wananchi.

Tuna Fichua Uovu pia ili kupambana na masuala ya Rushwa na uwajibikaji.

Mwaka jana tuliungana na wadau wengine tukaja na muswada wa mfano wa Ulinzi wa Taarifa Binafsi. Tunawashukuru wadau wote pamoja na watu waliosaidia kufanikisha hili.

DKT. PATRICIA BOSHE, MKUU WA IDARA YA SHERIA - JAMIIFORUMS
Sheria ya EPOCA inaruhusu Vyombo vya Usalama kutumia vifaa vinavyofuatilia kwa wakati halisi. Tatizo hapa siyo kuchukua taarifa za vifaa vya mtu binafsi kwa ajili ya kufuatilia shughuli za uhalifu, tatizo ni kwamba Sheria haijafafanua kwa kina kuhusu kiwango cha taarifa kinachoweza kukusanywa na kufikiwa na vifaa hivyo, jambo ambalo linaweza kuathiri hata raia wasiohusika na uhalifu

Patricia Boshe Jamiiforums.jpg

Patricia Boshe, mwanasheria wa JamiiForums

jamiiforums team JF.jpg

Wafanyakazi wa Jamiiforums waliohudhuria mkutano wa uhuru wa mtandao barani Afrika, kuanzia kushoto ni Ole Esseln, Ziada Omary, Melba Sandy, Emmanuel Mkojera, Glory Tarimo na Glory Tausi

JamiiForums jamii Forums (2).jpg

Kiongozi wa maudhui JamiiForums(Pichani kushoto), Franscis Nyonzo akiwaelekeza wageni waliohudhuria banda la Jamiiforums

Jamiiforums visitors JF.jpg

Mgeni akijaza kitabu cha mahudhurio alipotembelea banda la JamiiForums

Jamiiforums visitors.jpg

Afisa wa JamiiForums, Emmanuel Mkojera akimuelekeza jambo Brenda Barnabas Chrispin aliyetembelea banda la JamiiForums​

Fuatilia siku ya mwisho ya mkutano hapa: Yaliyojiri miaka 10 ya Mkutano wa Uhuru wa Mtandao Barani Afrika, Septemba 29, 2023
 
Naona pia kuna umuhimu wa kuelimisha na kuhimiza watu kushiriki katika mijadala kuhusu uhuru wa mtandao. Vijana, kwa mfano, wanaweza kuwa wachambuzi muhimu wa masuala haya.
 
Back
Top Bottom