Witness: Nilimsubiri mume wangu amalize kifungo cha miaka 30

Oldmantz

JF-Expert Member
Jan 24, 2023
430
996

Wakati tunaelekea Siku ya Wanawake Duniani, Witness Mbangala (45) ni miongoni mwa wanawake waliopitia changamoto katika familia, lakini bado wakasimama imara kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa.​


“Safari ya maisha yangu imepitia changamoto nyingi, baadhi ya watu walinishauri niolewe na mwanamume mwingine kwa sababu sitaweza kuvumilia kukaa peke yangu kwa muda mrefu kwa madai nitashindwa gharama za kuwahudumia na kuwasomesha watoto wangu,” anasema Witness, ambaye mumewe alifungwa miaka 30 jela na baadaye kupata msamaha wa Rais Samia Suluhu Hassan akiwa amekaa gerezani miaka 16.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na mwandishi wa gazeti la Mwananchi, Witness, ambaye mumewe alifungwa kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia nguvu anasema, “naomba mume wangu Richard Mgaya anipende kwa sababu nimevumilia kukaa miaka 16 bila kuolewa na mwanamume mwingine nikimsubiri amalize kutumikia kifungo chake cha miaka 30 ili tuendelee na maisha yetu.”

Witness, ambaye ni mkazi wa Kata ya Ifwagi Wilaya ya Mufindi, Iringa anasema, “maneno hayo yalisababisha wazazi wangu kunihurumia sana, wakaniambia nirudi nyumbani Morogoro na watoto wangu ili waweze kunisaidia kwa sababu walidhani nitashindwa kuwasomesha, lakini moyoni nilitafakari nirudi nyumbani nikasema hapana, ila nashukuru nimeweza kuwasomesha.

“Lakini moyoni nikasema nitapambana kuhakikisha nawalea watoto wangu hadi wafanikiwe kwa sababu nyumba na mashamba vitakuwepo, nitahakikisha nalima huku navuta subra ya kumsubiri mume wangu,” anasema Witness.

Pia, anasema hakuweza kuolewa kwa ajili ya kuwafikiria watoto wake kwa kuhofia, mwanamume mwingine anaweza kuwanyanyasa watoto wake, hali iliyompa moyo wa kupambana kuisaidia familia yake.

Alivyowaendeleza watoto wake
Hata hivyo, anasema watoto wake ndio ilikuwa faraja yake, isipokuwa wamekuwa kinyume na maisha aliyotegemea ataishi nao baada ya mtoto wake wa kike, Mackrina kupata ujauzito akiwa kidato cha nne.

“Niliumia baada ya mwanangu kushindwa kumaliza kidato cha nne kwa sababu ya kupata ujauzito, nilijeruhiwa sana moyoni mwangu nikajiuliza labda baba yao angekuwepo haya yasingetokea.”

Anasema alijitahidi kuhakikisha watoto wake wanasoma hadi kufikia malengo aliyotamani wafike, huku akifanya kilimo cha viazi na mazao mengine.

Witness anasema mtoto wake wa kike ambaye hakufanikiwa kumaliza kidato cha nne alimtafutia chuo cha urembo kujiendeleza ili aweze kujiari.

“Kwa sasa mwanangu amefungua saluni ambayo nilimnunulia vifaa vyote, hivyo nashukuru Mungu anaendelea na kazi yake vizuri,” anasema Witness.

Pia, anasema ana mtoto mwingine wa kiume, Frank aliyemsomesha chuo cha ufundi.

“Lakini kwa bahati mbaya, Frank hawezi kufanya kitu chochote kwa sababu ana tatizo la kisukari, ndio naendelea kumuuguza hadi sasa,” anasema Witness.

Alikuwa na ujauzito
Mbali na hilo, anasema aliendelea kuwasaidia watoto wake kupata kielimu, akiwamo Debora (16) ambaye wakati baba yake anafungwa alimuacha akiwa na mimba yake ya miezi sita.

“Nashukuru mume amerudi, lakini amemkuta mtoto ambaye aliniacha nikiwa na mimba ya miezi sita, amemkuta yupo kidato cha tatu, anaendelea na masomo yake vizuri.” Witness anasema baada ya mume wake kufungwa hakuwa na uelewa kipindi cha nyuma kuhusu masuala ya Magereza, lakini baada ya kusikiliza vyomba vya habari ndio akapata uelewa kwamba ipo siku mume wake ataachiwa huru.Kipindi cha nyuma nilikuwa sijui kama mtu anaweza kufungwa kisha akatoka, ila baada ya kusikiliza vyomba vya habari kwamba kuna baadhi ya wafungwa wametoka kwa msamaha wa Rais ndio na mimi nikajipa imani ipo siku moja mume wangu atatoka, ndio kama leo hii tupo pamoja,” anasema Witness.

Ujumbe
Witness anasema wanawake wanatakiwa kukabiliana na changamoto katika maisha ya ndoa kwa kuwa wavumilivu na kujenga imani ili kuhakikisha wanapambana katika njia nzuri ya kuendelea na maisha yao.

“Maisha ya hapa duniani yana changamoto nyingi, unaweza mtu asifungwe lakini akatekeleza familia, hivyo wanawake tunapaswa kuwa wavumilivu na kujipa moyo,” anasema Witness.

Witness anasema baada ya mumewe kutoka wamefungua ukurasa mpya wa maisha yao ya ndoa.

“Faraja yangu kwa sasa tumefungua ukurasa mpya na mume wangu, naamini atanipenda na kunithamini kwa mapenzi ambayo nimemuonyesha kwa kuilea familia yake.”

Mama mzazi wa Mgaya
Anjerina Luwumba ambaye ni mama mzazi wa mume wa Witness anasema baada ya mtoto wake kuhukumiwa kifungo hicho alilazimika kuwa karibu na familia ya mtoto wake ili kuhakikisha wajukuu zake wanaendelea kupata mahitaji kama alivyokuwa wanafanya baba yao.

Anatoa ushauri kwa mtoto wake kuwa ajihadhari na makundi ambayo hapo mwanzo walimsababishia matatizo aliyoyapata.

“Naomba sana mwanangu ajiepushe na vijana wenzake waliomsababishia matatizo kwa sababu ametoka na amewakuta, wasije wakamvuta tena kwani siwapendi hata kidogo,” anasema mama huyo.

Dada, mtoto wazungumza
Asnat Mgaya ambaye ni dada anasema anamshukuru Mungu kwa kumsaidia kaka yake hatimaye wapo pamoja katika familia yao, lakini pia anampongeza wifi yake kwa kuweza kuvumilia miaka yote hiyo.

“Kitu ambacho nashauri kaka yangu amsikilize sana mke wake, inafikia sehemu watu wanapoteza malengo yao ambayo wamejipangia hivyo ni muhimu kusikilizana katika maisha ya ndoa kuliko jamii,” anasema Asnat.

Mackrina Mgaya (20) ambaye ni mtoto anasema anamshukuru mama yake kwa sababu aliwafunza namna bora ya kuishi, ikiwa kujitambua na kumshirikisha Mungu kwa kila jambo wanalotaka.

Mackrina anasema licha ya kukatiza ndoto zake kwa sababu ya kupata ujauzito akiwa kidato cha nne, hakukata tamaa, aliona bado ana nafasi anaweza kufanya jambo lingine.

“Baada ya kukatiza ndoto zangu nilikaa nyumbani mwaka mmoja nikatambua bado nina nafasi ya kuandaa maisha yangu kwa njia nyingine, nilimuomba mama akanitafutia chuo nikasoma kwa miezi minne kwa sasa nimejiajiri mwenyewe,” anasema Mackrina.

Mume azungumza
Richard Mgaya ambaye alisamehewa mwaka jana anasema wakati anafungwa alimuacha mke wake akiwa na ujauzito wa miezi sita na mtoto alizaliwa yeye akiwa gerezani ambaye ni Debora mwenye miaka 16.

Mgaya anasema mbali na Debora, aliwaacha watoto wengine wakiwa na mama yao Frank na Mackrina.

Anasema dada yake alikuwa anakwenda na watoto wake wakati akiwa gerezani ili waweze kumfahamu baba yao kwa sababu alipofungwa walikuwa wadogo.

“Yaani siamini hadi leo kama kweli nipo nyumbani na familia yangu, bado sielewi kweli nipo na hawa watoto, naendelea kumuomba Mungu anisaidie niweze kuwa mfano mzuri katika jamii ili wajifunze kupitia mimi,” anasema Mgaya.

Mgaya anamshukuru mke wake kwa kuweza kukaa miaka yote hiyo na kuwasomesha watoto kwa shida hadi kufanikisha kuwafikisha katika hatua aliyowakuta nayo.

Naishukuru sana familia yangu, mama yangu mzazi na dada yangu walikuwa bega kwa bega na mke wangu kuwasaidia watoto wangu kwa sababu maisha ya sasa ni vigumu mwanamke kuvumilia miaka 16 wakati mume hayupo,” anasema Mgaya.

“Wapo wanawake wengi wanaoachwa kwa namna moja au nyingine, miezi miwili hadi mitatu anakuwa ameolewa, lakini mke wangu Mungu ameendelea kumuongoza kupambana miaka 16 hadi sasa nimerudi na nimemkuta,” anasema Mgaya.

Credit: Mwananchi
 
Sema mara moja moja atakuwa ameuza mechi. Yaani ile kibinadam. Watu wazima tunafahamu namna hiyo miaka 16 ilivyo mingi.

Halafu huyo Richard Mgaya aufuate ushauri wa mama yake. Aachane na tabia zake mbaya za ujambazi na uporaji. Na yeye ajifunze kushinda kwenye vinyungu, kama afanyavyo huyo mke wake Witness.
 
Back
Top Bottom