Wenye Kuhofia Uenyekiti wa Magufuli CCM Wana Hoja za Msingi? Ndiyo!!

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,489
40,018
magufuliccm2.jpg
Na. M. M. Mwanakijiji

Ukiwasikiliza wanaotaka au wanaoombea Magufuli asiwe Mwenyekiti wa CCM Taifa unaweza kupuuzia hoja zao. Lakini ukichukua muda kuwasikiliza utakubaliana na mimi kuwa wapo kati yao ambao wana hoja za msingi. Hoja hizi za msingi si lazima kuzikubali zilivyo bali zinastahili kutafakariwa na kukataliwa kwa sababu.

Ukizisikiliza sababu hizi kwa akili iliyotulia unaweza kuona ni sababu nzito na wanaozitoa wanaweza kabisa wanaamini wanaongozwa na uzalendo na fikra za kidemokrasia. Nitaziangalia baadhi ya sababu hizi zinazotolewa na kwanini zinaonekana na uzito wake kiasi cha kusababisha kuwepo kwa minong’ono ya kundi la vigogo ndani ya CCM ambao wanataka au wanaoombea au wengine wanaweza kuwa wanajaribu kuzuia Magufuli asiwe Mwenyekiti wa CCM.

1. Magufuli Hatabiriki

Kati ya vitu ambavyo vinaonekana kuwakwazwa baadhi ya watu ni kutokutabirika (unpredictability) kwa Magufuli hasa ni kwa namna gani anaelekea au anapanga kukiunda upya chama. Hii kwa baadhi ya watu inaonekana ni kwa sababu Magufuli hana historia ya ndani ya kuwa mtumishi wa chama katika ngazi mbalimbali. Kwa mfano Kikwete kabla ya kuwa waziri aliwahi kuwa kiongozi ndani ya chama na inadaiwa alikuwa anakielewa chama vizuri. Lakini kutokutabirika kwake huku kunatokana pia na mwenendo wake kama Rais ambao unaonekana hautabiriki; yaani huwezi kujua kesho anataka kufanya nini au atafanya nini. Kwa watu ambao walizoea hali ya kuweza kuhisi nini kinaendelea Magufuli anawapa kazi kubwa sana na wanaona anaweza kusababisha mvurugano mkubwa ndani ya chama.


2. Alivyothubutu Serikalini Inatishia Watu ndani ya Chama

Kitu kingine ambacho kinaonekana kusumbua baadhi ya watu ni jinsi gani Magufuli tangu aingie madarakani Novemba mwaka jana inaonekana ameendelea kuthubutu kwake kusafisha utumishi wa umma, kurejesha nidhamu na weledi na vile vile kutoa uongozi wa kitaifa ambao kwa baadhi ya watu ulionekana umepungua kwa kiasi kikubwa au kukosekana kabisa. Uthubutu huu wa kuleta mabadiliko (audacity of change) unawafanya watu kukaa na hali ya wasiwasi, kutokujisikia wamezoea viti vyao n ahata kutokuwa na usalama katika nafasi zao. Watumishi ambao wanaitwa kutumikia taifa sasa wanajihisi kuwa wapo pale kwa muda na mujibu wa majukumu yao; si kwa sababu wao ndio bora zaidi kuliko Watanzania wengine na kwamba hawako hapo kwa sababu nyingine yoyote isipokuwa dhamana ya kiuongozi ambao wamekabidhiwa na taifa.


Hili likielekezwa ndani ya chama wasiwasi unakuwa ni mkubwa zaidi. Kuna watu ndani ya chama kutokana na uzoefu wao, miaka yao na muda ambao wanaweza kuona kuwa umewapa umangimeza fulani wanazidi kuwa na wasiwasi hasa kama Magufuli ataingia na timu mpya na kuanza safisha safisha ndani ya chama. Hili linawafanya watu waone kuwa labda huu si wakati wa kumkabidhi Uenyekiti wa chama; kwani akiwa mwenyekiti akaja na watendaji wapya- kitaifa na mikoani basi hakuna atakayekuwa salama.


Baadhi ya watu wanarejea hotuba yake aliyoitoa mara baada ya kutangazwa mshindi na kabla ya kuapishwa ambapo alizungumza wazi mbele ya viongozi wengine wa CCM na kusema kuwa alikuwa anawajua watu ambao walikuwa wanakihujumu chama na kuwa alisema hawezi kufanya nao kazi. Kama watu hawa bado wapo na wanajulikana basi usalama wa watu hawa haupo tena hasa kwa vile wanajua mtu ambaye alikuwa tayari kumuondoa rafiki yake mpenzi kwenye nafasi kubwa kwa hakika anaweza kumng’oa hata mwanae kwenye nafasi hizo! Hili linawatisha watu.


3. Tayari Magufului Amegusa Baadhi ya Vigogo na Wafadhili wa CCM; Na hapo Hajawa Mwenyekiti Bado

Sababu nyingine ambayo inaonekana kuwapa baadhi ya watu mshawasha wa uenyekiti wa Magufuli CCM ni kuwa tayari hadi hivi sasa kuna baadhi ya watu wameng’olewa, kuna watu ambao walijijua ni kismati ya CCM na wafadhili ambao makampuni yao au wao wenyewe wamejikuta matatani na kuna baadhi ya watu ambao wanaamini walitoa mchango mkubwa mwaka jana ambao sasa hivi hawapati ujiko waliokuwa nao. Watu hawa wa CCM ni watu wazito ambao wanasumbuka kwani hawana tena ule ujiko wa kisiasa (political clout) ambayo waliamini kuwa wanayo.


Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana ambao baadhi ya watu walisimama kidete kukataa mabadiliko feki yaliyoongozwa na baadhi yetu; wapo ambao walitarajia kama sehemu ya ‘shukrani’ fulani basi watu hao watakuwa salama na kukumbukwa. Kuna mtu mmoja kigogo tu alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kabisa kupata mshikemshike wa serikali ya awamu ya tano licha mchango wake mkubwa. Vyanzo vyangu vya uhakika vinathibitisha kuwa mshikeshike wa mtu huyo uliwakwaza baadhi ya viongozi wa juu kabisa wa CCM (kwenye Sekretariati) na mara moja waliapa kutokufanya kazi chini ya Uenyekiti wa Magufuli.


Mmoja wa viongozi hawa aliamua hata kukaa pembeni kwa muda hasa baada ya kuamini kuwa Magufuli ana tatizo jingine ambalo ni sababu ya nne.


4. Magufuli Haambiliki

Sifa hii kwa wanaokumbuka sana (wazee wenzangu) ilikuwa ni moja ya sifa ya muda mrefu ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere hasa kwenye maneno mitaani. Wengi walimuita kuwa “haambiliki” na yeye mwenyewe alikuwa anajua (rejea hotuba yake ya “Mara ya Kwanza Waliniita Musa”.


Magufuli anaonekana Haambiliki kwa maana ya kwamba, kuna baadhi ya maneno ambayo baadhi ya watu wanataka wanong’one lakini mwenzao kaweka pamba. Mfano wa hili ni haya aliyoyasema wakati wa uteuzi wa ma DC na DAS siku chache zilizopita. Kwamba kuna watu waliandika vimemo watu wao wakumbukwe na matokeo yake watu wale hata kama walikuwa wanafikiria ilibidi awakate majina yao.


Kutokuambilika huku kwa Magufuli kunawapa tatizo; kimsingi ina maana hadhibitiki (uncontrollable). Kuna viongozi wa kisiasa ambao walitarajia kutokana na uzoefu wao au nafasi zao walipaswa kuwa na ‘sauti’ mbele ya Magufuli lakini kwa mwendo huu Magufuli inaonekana sauti anayoisikiliza ni ya watu wake lakini wao wanapaswa kwanza kusikiliza sauti yake. Sasa kama amewakuwa haambiliki akiwa Rais tu itakuwaje akishavaa kofia zote mbili?


5. Kutaka Kutenganisha Uenyekiti na Urais

Mojawapo ya mijadala ya muda mrefu ambayo pia inaibuka tena wakati huu kama ilivyowahi kuibuka huko nyuma ni uwezekano au ulazima wa kutenganisha vyeo vya Urais na Uenyekiti wa Chama. Hoja hii hutolewa kwa jina la demokrasia na ni miongoni mwa sababu nzito kweli kweli. Kwamba, ili chama kiweze kusimamia serikali iliyoko madarakani basi ni vizuri Rais asiwe Mwenyekiti wa chama wakati huo huo. Kutenganisha vyeo hivi au kofia hivi basi itaweka utaratibu mzuri wa kusimamiana kati ya chama na serikali yake.


Wapo baadhi ya watu ambao wanaona kutokana na sababu nyingine nyingi kama za hapo juu basi Magufuli anahitaji kusimamiwa na chama kuliko apewe mkono huru wa kutawala na kusimamia serikali na chama. Wanaona kuwa akiwa Mwenyekiti itakuwa vigumu sana kusimamia serikali yake na chama kwa wakati mmoja.


Sababu hii ya tano pia inatajwa kwa jina la demokrasia. Kwamba, ni vizuri kwa nchi ya kidemokrasia kutenganisha nafasi hizi ili kuhakikisha kuwa upo mfumo mzuri usiominywa.

Ndugu zangu, sababu hizi zote na bila ya shaka zipo nyingine ambazo nazo zinaonekana ni nzito au ni nzito kweli ambazo zinawafanya baadhi ya watu kutotaka Magufuli asipewe Uenyekiti. Kwa maoni yangu hata hivyo, wakati huu sisi kama taifa na katika historia sababu hizi hazitoshi kuzuia au kuwa sababu ya kuvuruga uwezekano wa Magufuli kuwa Mwenyekiti wa chama ambacho kimelaumiwa kwa muda mrefu kwa matatizo mengi ya nchi yetu.

Tuangalie basi majibu ya hoja hizi.

Kwamba, Magufuli hatabiriki; hoja hii tatizo lake kubwa ni kudhania (assume) kuwa Watanzania wanataka Rais anayetabirika kwa kila jambo. Lakini pia inashindwa kuelezea tatizo la kutokutabirika ni nini hasa. Upande mwingine ni kuwa hoja hii haina ukweli kwa sababu Watanzania sasa hivi wana Rais anayetabirika labda kuliko wakati mwingine wowote ukiondoa wakati wa Baba wa Taifa.

Sisi tuliomuunga mkono Magufuli na ambao tulitakaa mabadiliko ‘yale’ tulikuwa tunajua kabisa Magufuli ni mtu wa namna gani. Tulijua udhaifu wake kama kiongozi lakini pia tulijua nguvu yake kama kiongozi. Wengi wetu tumemuona kwa miaka hii ishirini ya utumishi wa umma na tunajua ni wapi alionesha udhaifu lakini ni wapi katika udhaifu huo alionesha nguvu na uthubutu wa kiongozi ambaye Tanzania inamhitaji.

Hakuna jambo lolote ambalo Magufuli amefanya hadi hivi sasa ambao baadhi ya sisi tuliomuunga mkono hatukuweza kulijua au kulitabiri. Kwa walionisoma mapema baada ya ushindiwa Magufuli niliweka bayana ni mambo gani ambayo yanaenda kutokea; kuanzia “tengua tengua” hadi “ugumu wa maisha utakaotakana na kuusahihisha uchumi uliojengwa kwa misingi ya kifisadi”. Tupo tuliojua kuwa kuna baadhi ya mashirika yatahitaji kusafishwa mapema zaidi kwani matatizo yake yamejulikana muda mrefu lakini yalifunikwa kishkaji. Magufuli anatabirika.

Tatizo ni kuwa huwezi kumtabiri kirafiki au kishkaji. Ukifikiria ni mwenzako na kwamba anautii sana kwako kuliko maslahi ya Watanzania wengi zaidi utapotea na kujikuta kwenye matatizo. Kuna mambo ambayo ameshajifunza na inaonekana baadhi ya makosa yake ya nyuma haelekei kuyarudia tena.

Hoja ya kwamba alivyothubutu serikalini inatishia ndani ya chama nayo ni ya kupuuzia. Hoja hii nayo inadhania kuwa ndani ya chama hawatakiwi kuguswa au kufanyika marekebiso yoyote. Kwamba, walioko ndani ya CCM hata kama kuna wabovu na ambao wamekuwa sababu ya tatizo la kisiasa nchini basi waachwe tu kwa vile wanajiona kama chama ni ‘chao’. Kudhania huku nako kuna makosa. Kuna wanachama na wasio wanachama wa CCM ambao kwa muda mrefu hawakufurahia jinsi chama kinaendeshwa na jinsi gani kwa muda mrefu kilikuwa kimeshindwa kujisafisha.

Hivyo, ujio wa Magufuli unawapa matumaini watu hawa kuwa yumkini CCM inaenda kupitishwa kwenye tanuru la moto. Tanuru ambalo litasafisha na kutakatisha vilivyokuwa vichafu. Lakini pia inajulikana mapema tu kuwa siyo watu wote walioko ndani ya CCM hasa baadhi ya viongozi walikuwa wanataka mabadiliko ya kweli. Wapo ambao walipokuwa wanaimba “tunaimani na Lowassa” kwa kweli walikuwa wanamaanisha kuwa wanataka mambo yaendelee katika CCM ile ile; CCM ya wanaojuana, CCM ya wanaobebana, CCM ya wenzetu huu. Hawa walijua kama Lowassa angekuwa mgombea wa CCM, CCM ingeendelea kweli kuwa ile ile.

Hivyo ujio wa Magufuli ndani ya chama unaenda kuvunja mtandao huu uliokuwa umeuza haki zake kwa mtu mmoja. Hili linawatisha lakini pia ni lalazima. Kama Magufuli anataka kweli kusimamia serikali vizuri hawezi kuwa na chama kilichogawanyika na kilicho na makundi yenye maslahi ya watu mbalimbali. Hivyo, hofu hii haina msingi; kwa wana CCM na watu wengine ambao wamekuwa wakiingalia CCM kwa mbali ujio wa Magufuli unaweza kuwafanya watu waingalie CCM kwa karibu na kuona kama inaweza kujisafisha.

Kwamba, Magufuli Anaweza Kugusa Watu Wazito Zaidi ndani ya Chama nayo ni hoja ya kupuuzia. Kama kuna watu wazito na vigogo ambao wamekuwa wakikichafua chama hicho na ambao kwa muda wamefanya watu waichukie na kuona CCM ni tatizo na miongoni mwao ni mimi mwenyewe sasa kwanini tusifurahie ujio wa Magufuli kama Mwenyekiti CCM? Kama ameweza kugusa mawaziri, wakuu wa mikoa, wakurugenzi n.k ndani ya Serikali kwanini tusitake akatumbue majipu mengine ndani ya CCM majipu ambayo yaliifanya CCM sehemu ya kuficha maovu yao?

Kwa wanaotaka utawala bora Tanzania Magufuli Uenyekiti wa CCM siyo tatizo kwa taifa; na inaweza kuwa ni baraka kwani sehemu ile ambayo imekuwa tatizo la muda mrefu inaenda kushughulikiwa na wale ambao labda kwa sababu ya CCM waliamini kuwa wanaweza kufanya lolote, popote na kwa yeyote wanaenda kutetemeka na wengine – naweza kutabiri kwa urahisi kabisa wanaelekea kustaafu siasa moja kwa moja.

Hoja ya kuwa Magufuli Haambiliki nayo ina matatizo yake; kwani inataka watu wakubali kuwa mtu akiambiwa kitu hata cha kipuuzi basi akubali. Au kwamba, Magufuli akiambiwa afanye jambo ambalo halina maslahi kwa taifa japo linaweza kuwa na maslahi kwa mtu mmoja au kikundi fulani basi afuate tu jambo hilo na kwamba asipofanya basi ‘haambiliki’.

Kiongozi mzuri ni yule anayeweza kujua tofauti ya mambo ya kusikiliza na wakati wa kusikiliza na uzito wa mambo hayo. Huwezi kuwa na kiongozi anayefuata upepo wa kila neno linalopeperuka; huyo si kiongozi ni mfuasi!

Hoja ya mwisho ambayo ina uzito wake ni hii ya kutenganisha vyeo vya Urais na Uenyekiti wa CCM. Jambo hili linawezekana kwa maana ya kiutendaji tu. Kwamba, Mwenyekiti wa CCM asiwe Rais ili kwamba awe na muda wa kushughulikia mambo ya chama bila kuwa na adha ya Urais. Kwa baadhi yetu hili tulilipenda kwa sababu hatukufurahia sana kuona vikao vya chama vinafnyika Ikulu; kama Mwenyekiti wa Chama anataka kuitisha vikao vya chama basi ofisi za chama zipo aende huko kama ambavyo tumeona siku za karibuni Kikwete akifanya hivyo.

Hatujaona katika nafasi nyingine yoyote ambapo Mwenyekiti wa CCM wa tawi ambaye ni mwalimu wa shule akaruhusiwa kufanya kikao cha kamati ya tawi shuleni kwake tena muda wa kazi! Hatujawahi kuona mtu ambaye ni katibu wa CHADEMA wa wilaya akaamua kuitisha kikao cha siasa mahali pa kazi na akaachwa. Kama hili halipaswi kuwa kwa sababu itaonekana ni kuleta siasa kazini basi haipaswi kwa Mwenyekiti wa CCM kufanya kikao chochote cha kisiasa (cha Kikatiba) katika ofisi za Serikali. Hili ni suala la nidhamu tu.

Hili hata hivyo halihitaji kutenganisha ofisi hizo mbili; hili linahitaji kuchukuliwa maamuzi tu ya kinidhamu ya kazi na binafsi naamini Magufuli akishapima uzito wa hoja hii atakapokuwa Mwenyekiti mojawapo ya maamuzi ya kwanza kufanya ni kutokufanya vikao vya chama Ikulu.

Pamoja na hilo hata hivyo, kwenye nchi nyingi za kidemokrasia, cheo cha Mwenyekiti ni cheo cha utendaji; ni kama Afisa Mkuu wa Kampuni (CEO). Hata hivyo, endapo mgombea wa chama chake anashinda Urais au Uwaziri Mkuu basi yule Rais au Waziri Mkuu kutoka chama hicho ndiyo anakuwa “Kiongozi wa chama” kwa maana ya kwamba, anakuwa juu ya Mwenyekiti wa chama kwani yeye ndiye yuko mahali pa kuweza kutekeleza sera na mipango mbalimbali.

Rais Magufuli wakati wanafanya kampeni mwaka jana kwa kiasi kikubwa alikuwa anauza ajenda zake. Ajenda zile mbalimbali anadaiwa na Watanzania kuzitimiza. Kwa vile mfumo wetu hauko kama nchi nyingine basi ni yeye anawajibu wa kuona zinatekelezeka kisiasa na kiutawala.

Lakini pia tukumbuke kuwa mfumo wetu wa kisiasa Tanzania bado umejengwa katika mfumo wa nchi za Kijamaa au Kikomunisti ambapo Chama kinashika uongozi wa nchi na kinashika kweli kweli. Kwenye hizo za kijamaa kiongozi wa chama ndiye pia anakuwa Rais. Kwa mfano, Xi Jinping ambaye ni Rais wa China yeye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha China na ndiye anayeongoza Kamati Kuu ya chama hicho. Cuba mfumo uko hivyo hivyo, Katibu Mkuu wa chama cha Kikomunisti cha Cuba ni Raul Castro; ambaye pia ni Rais wa Cuba.

Hata hivyo, Kwenye nchi kama Vietnam ambayo nayo inafuata Ukomunisti Rais siyo Katibu Mkuu wa Chama; lakini Katibu Mkuu wa Chama ndiye kiongozi mkuu zaidi Vietnam. Rais ni mtu wa pili baada ya Katibu Mkuu na ni mjumbe wa Kamati Kuu ya chama. Hata hivyo, madaraka makubwa ya kiutawala yako kwa Katibu Mkuu na Rais ni cheo cha “maadhimisho” zaidi kuliko kiutendaji. Tukiamua kufuata mfano wa Vietnam basi ni lazima ukubali kupunguza madaraka makubwa toka kwa Rais. Lakini kwa vile nchi yetu ni ya vyama vingi siyo kimoja cha Kikomunisti ni wazi kuondoa madaraka ya Rais na kuyaacha kwa kiongozi wa kisiasa haiwezekani.

Ni kwa sababu hiyo utaona kuwa hoja hii japo ni nzito lakini katika mfumo wetu wa sasa ulivyo haiwezekani kuwa na viongozi wawili kitaifa ambao wana nguvu kubwa – mmoja nguvu za kisiasa na mwingine nguvu za kiutawala. Hawa wawili wasipopatana au wakishindana inaweza kusababisha matatizo mengine makubwa yasiyo ya lazima.

Hivyo basi suala la Uenyekiti wa Magufuli CCM haliepukiki na hekima inalazimisha iwe hivyo. Kama tunataka kubadili mfumo wa aina hii basi kuna mabadiliko mengine mengi yanahitaji kufanyika ili kuhakikisha kuwa hatutengenezi matatizo makubwa zaidi kwa kujaribu kuondoa tatizo lisilo tatizo kubwa. Tusije kuamua kuua nzi kwa bomu; tena ndani ya nyumba.

Jambo kubwa la kuzingatia ni kuwa:

CCM ya Magufuli haiwezi kuwa kama zilizopita; tulishawahi kuwa na viongozi wanaotabirika, wanaosikiliza kila mtu na ambayo hawakuwa wakali ndani ya CCM na matokeo yake sote tunayajua;

CCM ya Magufuli inaweza kujikuta inakuwa ni kama chama kilichozaliwa upya na viongozi wake wakajikuta wanawajibika kwa wananchi kwani watakuwa chini ya kiongozi ambaye tayari amejionesha ni wa namna gani;

CCM ya Magufuli inaweza kuwa ndio tishio kubwa zaidi la upinzani uliojivuruga na ni rahisi kutabiri kuwa endapo mabadiliko makubwa yatafanyika ndani ya CCM kuna uwezekano mkubwa – na hili ni rahsi kulikona – tukaona watu wengi walioikataa CCM na kuibeza wakirudi taratibu kwani watakuwa wanakiona chama kipya. Kwa sisi wengine wenye mashaka na CCM bado hatujawa na sababu ya kufurahia CCM au kuiunga mkono CCM kwani bado haijaonesha kuwa inatambua kuwa ilikuwa ni sehemu ya matatizo ya muda mrefu ya kitaifa. Tunasubiri tuone Magufuli atafanya nayo nini. Hofu yangu nyingine ni kuwa tusipoangalia kama Magufuli atafanikiwa kuisafisha CCM, kuibadilisha na kuiweka kwenye misingi sahihi ya kidemokrasia na kiutawala basi tunaweza kushuhudia Ulazima wa tukio la 1965 kujirudia. Hili linatufanya tusite na kutafakari kidogo maana yake.

CCM ya Magufuli inaweza kuwa ni CCM ya zama mpya; CCM ambayo inaendana na serikali yake na kuwa badala ya kuwa sababu ya matatizo yenyewe inakuwa sababu ya masuluhisho ya matatizo.

Ni kwa sababu hizo zote basi mjadala wa watu kuhofia Magufuli kuwa Mwenyekiti wa CCM nimeufunga rasmi; na nimeufunga kwa uwezo na madaraka niliyojipatia mwenyewe. Tunasubiri kuona Mwenyekiti Magufuli ataipeleka wapi CCM kuelekea kufanikiwa kwa zama hizi mpya za mabadailiko.
 
Kabla ya mengine, mimi nataka kujua huko Dodoma kunaenda kufanyika uchaguzi au uteuzi? Ni kipi kati ya hivyo viwili kipo kikatiba? Kama ni uchaguzi, mbona sioni faida au/na hasara za mgombea mwingine zaidi ya JPM zikichambuliwa hadharani?
 
Kabla ya mengine, mimi nataka kujua huko Dodoma kunaenda kufanyika uchaguzi au uteuzi? Ni kipi kati ya hivyo viwili kipo kikatiba? Kama ni uchaguzi, mbona sioni faida au/na hasara za mgombea mwingine zaidi ya JPM zikichambuliwa hadharani?

Dodoma kutakuwa na uchaguzi na jogoo ameshawika, kwahiyo kinachofuata ni kumpa kada wa CCM kura za ndio...
 
Magufuli atatuvusha, na asipokuwa mwenyekiti, kuna watu watalia zaidi atakacho wafanyia. All in all ni kuwa neema inakuja Tanzania kwa walio wengi
 
Kabla ya mengine, mimi nataka kujua huko Dodoma kunaenda kufanyika uchaguzi au uteuzi? Ni kipi kati ya hivyo viwili kipo kikatiba? Kama ni uchaguzi, mbona sioni faida au/na hasara za mgombea mwingine zaidi ya JPM zikichambuliwa hadharani?
Kinachokwenda kufanyika Dodoma ni Magufuli anakwenda kuunda secretarieti mpya ya ccm maana yeye tayari ni mwenyekiti, Hakuna uchaguzi ndani ya safu ya ccm Taifa.
 
Hivi nyie ndo mnajigamba huko CCM kuna demokrasia uenyekiti wa chama mtu kupinga anaonekana msaliti kwa mujibu wa kada wa CCM Lizaboni bundi ameshatoa dodoma mtaparuana sana mwisho wenu unakaribia
 
Back
Top Bottom