Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,478
- 40,000
1. Lowassa baada ya kukatwa jina lake alitakiwa kujitoa wakati ule ule kabla ya kura za NEC na Mkutano Mkuu. Sijui ni nani walikuwa washauri wake lakini kipindi cha yeye kukatwa na kabla ya mkutano wa NEC thamani yake kisiasa kwa CCM na hata nje ya CCM ilikuwa haishikiki wala kukamatika; iliendana kabisa na idadi ya watu waliokuwa wanamuunga mkono kwenye udhamini. KUshindwa kwake kufanya uamuzi wa lazima ambao rafiki zake walimtengenezea daraja la kupitia kumethibitisha kile ambacho wengine tumekuwa tukikisema kuwa si mtu wa maamuzi sahihi au ya lazima. Aliamua kufanya uamuzi mgumu; kubakia ndani ya CCM.
2. Lowassa amewaangusha watu waliomtengenezea daraja la kupitia kwenda chama kingine (isipokuwa Chadema - rejea mada yangu nyingine kwa hili). Emmanuel Nchimbi, Adam Kimbisa na Sofia Simba waliamua kumtengenezea daraja na nadhani ilikuwa ni sehemu ya makubaliano ya awali ili yeye afuatie na kusema kuwa na yeye hakubaliani na maamuzi ya kamati kuu na hivyo ameamua kurudisha kadi ya CCM na kujitoa akifikiria hatua inavyofuatia. Uamuzi huu ungetosha kabisa kuipasua CCM na vikao vilivyokuwa vimebakia.
3. Bahati mbaya Lowassa alijikuta anaburudishwa na ule wimbo wa "tuna imani na Lowassa" lakini alishindwa kutumia clout (ujiko) ule ipasavyo. Alisimama kama swala aliyepigwa na mwanga wa gari barabarani. Hakujua afanye nini.
4. Hata baada ya kura za NEC - chombo ambacho kingeweza kusahihisha maamuzi ya Kamati Kuu (NEC ni chombo cha juu ya CC) Lowassa hakuoneakana kutaka kupigania nafasi yake na badala yake akala 'kobisi' na kuvumilia hadi Mkutano Mkuu ambako nako akaburudishwa na kushangiliwa jina lake lilipotajwa na Da' Amina Ali. Alishindwa kufanya uamuzi wa lazima na uamuzi sahihi. Aliamua kufanya uamuzi mgumu wa kubakia na watu waliomsaliti, kumtupa na kumgeuka.
5. Sasa hivi hata baada ya Mkutano Mkuu watu wengine walitarajia angefanya ule uamuzi japo thamani ilikuwa inazidi kushuka lakini hakufanya hivyo. Matokeo yake hata kina "Msukuma" ambao waliapa ati wanaenda naye nchi ya ahadhi liwalo na liwe wote wakageuka na kuanza kuimba nyimbo za Magufuli. Hata Nchimbi ambaye alisimama kupinga maamuzi ya Kamati Kuu - hili sikumbuki kutokea tangu CCM ianzishwe - naye amegeuka na kusema ati Magufuli ndiye mgombea sahihi - kana kwamba alikuwa hajui kabla. KUshindwa kwake kufanya uamuzi huu wakati muafaka na sasa ati anajadiliana na familia na wadau wengine inashangaza na kuchekesha. Hivi hawa watu walikuwa hawajakaa na kufikiria "the worst case scenario"? Unaweza vipi kupanga harakati au jambo lolote lile muhimu bila kufikiria mambo yakienda vibaya kabisa utafanya nini?
Ni kwa sababu hiyo hata kumfikiria ati kuna watu wanataka aende upinzani sasa sijui kama itakuwa na matokeo kama angeamua kwenda kabla ya Kura za NEC na Mkutano Mkuu. Sijui kama thamani yake kisiasa bado ipo kivile tena na sidhani hata wale wadhamini karibu milioni wanamtaka sasa hasa kama anataka kupambanishwa na Magufuli. Kama kuna kiongozi yeyote wa upinzani au chama kinamfikiria kuwa anathamani ile aliyokuwa nayo kabla naomba niwape taarifa mbaya - hana tena. Ni sawasawa na kutaka kununua tiketi ya Mayweather na Pacquiao baada ya pambano; ni sawasawa na kutaka uende mpirani kuangalia mechi ya MaNU dhidi ya Chelsea wakati watu wanatoka uwanjani kipenga cha mwisho kishalia. Sidhani wale wana CCM wapenda madaraka na wafuata upepo leo watakuwa tayari kumfuata "kokote atakakokwenda". Hata wale Wachungaji waliomba "Pamoja na wewe" sidhani kama akiwaita leo nyumbani wataimba tena vile; labda wataimba "Tulimwambia Lowassa Bai Bai"!
Ushauri wangu wa kiutu tu ni kuwa uamuzi sahihi sasa kwa Lowassa ni kustaafu siasa kabisa na kwenda kupumzika. Mihemko ambayo ameipata miaka hii tangu kujiuzulu inamtosha kabisa katika maisha na sidhani ana sababu nyingine yoyote - iwe ya kisasi au vinginevyo - ya kujiingiza siasa za Tanzania. Kama akitaka zaidi kuonesha kutofurahishwa na CCM yake anaweza kujiunga na chama kimoja cha upinzani kama mwanachama wa kawaida tu na kuwasaidia kukiondoa chama kilicho mlea. Kwani CCM siyo mamake! Ingekuwa mamake au hata umbu yake kisingemgeuka hivyo.
Nimpe pole tu kuwa hizi nazo ni 'ajali za kisiasa' hata kama nyingine zinasababishwa na watu kwa makusudi. UKAWA - iwe mtu mmoja au timu nzima - wakifiria kuwa Lowassa ana thamani aliyokuwa nayo baada ya jina kukatwa na kabla ya vikao vya NEC na Mkutano Mkuu watakuwa wanajidanganya. Wamuache mzee wa watu apumzike. Ila kama kuna chama cha upinzani kinafikiria kinaweza kumtumia Lowassa vizuri kama mgombea wake wajaribu; sidhani kama kuna kundi kubwa CCM litamfuata kama nilivyofikiria mwanzoni. Wale wote waliokuwa wanamuunga mkono tangu ajiuzulu wengi walikuwa wamepigia mahesabu yeye kuwa mgombea wa Urais kwa CCM. Hili halitatokea sasa hivi isipokuwa kwa njia nje ya za kibinadamu.
MMM