Waziri Dkt. Ndumbaro Ahimiza Watanzania Kuzichangia Timu za Taifa

Stephano Mgendanyi

JF-Expert Member
May 16, 2020
1,903
945
Waziri wa Uatamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro ametoa wito kwa Watanzania na wadau mbalimbali wajitokeze kuzichangia timu za Taifa katika harambee itakayofanyika Januari 10, 2024 jijini Dar es Salaam akisisitiza kuwa zoezi hilo litakuwa endelevu ili kuzijengea uwezo timu za Taifa pia kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ili timu hizo ziweze kushiriki Mashindano mbalimbali ya Kimataifa.

Ametoa kauli hiyo leo Januari 9, 2024 wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Harambee kwa Timu za Taifa itakayofanyika Januari 10, 2024 Jijini Dar es Salaam ambapo amesema harambee hiyo ni ya Watanzania wote.

“Tunahitaji kila Mtanzania mwenye mapenzi mema ashiriki kuchangia na kuwezesha ushiriki wa timu zetu ambazo ni zaidi ya 20 na hamasa hii pia ni njia nyingine ya kuongeza uwajibikaji kwa wachezaji”

Amesema Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan imekua ikichukua hatua mbalimbali za kuziwezesha timu za Taifa kushiriki michuano mbalimbali ya Kimataifa pia kushughulikia na eneo la kisera, fedha, diplomasia na maeneo mengine muhimu ili kuziwezesha timu za Taifa zifanye vizuri.

Kuhusu Kamati aliyoiteua hivi karibuni amesema itafanya kazi katika kipindi cha mwaka mzima ambapo kutakuwa na matukio manne ya ukusanyaji fedha huku akisisitiza kuwa tukio la kwanza linafanyika Januari 10, 2024 jijini Dar es salaam na litakalofuata litafanyika nje ya mkoa wa Dar es salaam huku akitoa wito kwa Wakuu wa Mikoa mingine watakaopenda tukio hilo lifanyike kwenye mikoa yao wawasiliane na Wizara hiyo kupitia TAMISEMI.

“Kamati niliyoiteua siyo kamati ya kusafiri wala kulipana posho, hii ni kamati inayoweza kuongezeka kwa kuzingatia mgawanyo wa majukumu uliopo sasa wa uwepo wa kamati ndogo mbili ambazo ni Kamati ya fedha na kamati ya hamasa ambazo zote zinaendelea kufanya kazi nzuri’’.
 
Back
Top Bottom