Waziri Chikawe ang`aka na afya yake

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,318
33,125
Chikawe(20).jpg

Waziri Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe


Waziri Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe, ameibuka na kusema watu wanaosema mawaziri wanaoumwa watoswe uwaziri, hizo ni siasa tu kwani kwa upande wake wanaotamani hivyo watashindwa labda wamtafutie sababu nyingine, lakini si ya ugonjwa.

Kuthibitisha kwamba afya yake ni madhubuti, Chikawe alisema kuwa katika kipindi cha hivi karibuni hajaugua hata mafua.

Akizungumza juzi usiku katika mahojiano kwenye kipindi cha dakika 45 kinachorushwa na kituo cha ITV jijini Dar es Salaam, alisema wanaomzushia ugonjwa wanamkufuru Mungu kwani hivi karibuni hajaumwa na yupo salama kiafya.

“Jana nilikuwa natoka nyumbani, asubuhi huwa napenda kusikiliza magazeti redioni nikasikia kwamba kuna mawaziri fulani ni wagonjwa, afya zao ni tete na katika hao mawaziri na mimi nikatajwa, nikamwangalia dereva wangu naye akanitazama tukasema heee na mimi nipo,” alisema Chikawe.

Alisema baada ya kufika ofisini alipelekewa gazeti lililoandika habari hizo na kulisoma na kuanza kuhoji kwanini walioandika habari hiyo hawakumpigia simu kumuuliza afya yake ikoje, ili awaeleze kuwa hata mafua hana na wala haumwi na hivi karibuni hajaumwa.
Chikawe alisema kutokana na kuripotiwa kwa habari hizo, alipigiwa simu nyingi sana, na baada ya hapo alimpigia simu mama yake mzazi ambaye ni mzee ili asidhani kuwa anaumwa kweli.

Chikawe ni waziri wa pili kuibuka na kudai kuwa haumwi. Wa kwanza kusema hivyo ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami, ambaye alisema kuwa yeye si moja kati ya mawaziri wanaonekana kuwa mzigo katika serikali ya Rais Jakaya Kikwete na kutaka Watanzania kuacha tabia ya kuombeana mabaya, ikiwa ni pamoja na kuombeana vifo na kuzushiana magonjwa.

Mbali na Dk. Chani, mawaziri wengine ambao walikuwa wagonjwa na kulazwa nchini India ni Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya na Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe.

SHERIA YA MAADILI KUREKEBISHWA

Chikawe alisema Serikali inakusudia kufanya mabadiliko ya Sheria ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma itakayowezesha fomu wanazojaza viongozi hao pasiwepo ugumu kwa wananchi kuziona na kuzisoma ili wapate fursa ya kukosoa kama wamedanganya kuhusu mali wanazomiliki.

Alisema lengo ni kuhakikisha panakuwepo uwazi na uwajibikaji katika ofisi za umma.

“Itabadilishwa sheria ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ili kusiwe na ugumu wa kwenda kukagua fomu ya kiongozi fulani ili kama inawezekana ziwekwe hata kwenye ‘website’ (tovuti) kwa mfano, kama wewe ni dereva wangu unajua najenga gorofa kule umetazama fomu yangu lile gorofa sijaandika, unaweza ukasema huyu mzee muongo,” alisema Chikawe.

Alisema uamuzi wa kufanya mabadiliko hayo ni kwa sababu kuna viongozi wengi wanajaza fomu, lakini wanajaza uongo kuhusu mali zao na wanafanya hivyo kwa sababu wanajua wao wenyewe wamezipataje.

“Sasa una mali una mkopo wa benki, unaogopa nini si useme na mshahara wako unakatwa kila mtu anao umekopa Baypot na nyumba umejenga kwa mkopo wa Baypot, lakini sasa hawafanyi hivyo, tunachotaka kufanya ni nini, tunajaribu kuiwezesha tume iwe na nguvu zaidi za kufuatilia,” alisema na kuongeza:

“Unajua kuwa watu zaidi ya 8,000 wanaojaza hizi fomu kwa hiyo kumfuatilia kila mtu kuona ukweli wake ni gharama kubwa.”

Chikawe alisema viongozi 60 ambao watakaohakikiwa mali zao katika awamu ya kwanza wakibainika wamedanganya, watachukuliwa hatua na wale ambao itabainika mali zao zinatia mashaka kwa maana zina dalili za rushwa, watapelekwa Takukuru.

Februari 14 mwaka huu, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ilitangaza kuwa imeanza kuhakiki kama mali za viongozi wa umma walizojaza kwenye fomu za tamko ndizo wanazomiliki.

Kamishina wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Salome Kaganda, alisema Tume yake itaanza kutekeleza kazi hiyo kwa kufanya uhakiki wa mali za viongozi 60 wa umma.

Kati ya viongozi hao wamo mawaziri, wabunge, wakuu wa mamlaka zinazojitegemea za serikali na viongozi wengine waandamizi.



CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom