Watoto 200 wawa viziwi mbagala, 2000 hawaendi shule

Msongoru

JF-Expert Member
Apr 16, 2008
306
24
Na Fredy Azzah, MWANANCHI

ZAIDI ya wanafunzi 200 wa shule za msingi za Mbagala Kuu na Maendeleo, jijini Dar es Salaam, wamebainika kuwa na matatizo ya kutosikia vizuri na kuumwa kichwa kutokana na athari za milipuko ya mabomu iliyotokea katika Kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ya Mbagala Kizuiani, Aprili 29, mwaka huu.


Wakati hali ikiwa hivyo, jana wataalamu wa mabomu wa JWTZ wameendelea kutegua na kulipua mabomu mengine yaliyosalia katika eneo hilo na kuendelea kuwatia hofu wakazi wa eneo hilo na hasa baada ya bomu moja kulipuka kwa kishindo kikubwa.


Bomu hilo limefanya watu 75 wazirai na watoto wawili waliangukiwa na ukuta wa nyumba ya mkaazi mmoja ambayo ilikuwa na ufa uliosababishwa na mlipuko wa awali.


Watoto hao ambao ni wa familia moja ni Isaack Ngalawa na Rose Ngalawa ambao wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Temeke.


Shule za msingi Mbagala Kuu na Maendeleo zinazopakana na ukuta wa matofali, zipo katika umbali wa karibu kilomita moja na nusu kutoka ilipo kambi hiyo.


Mbali na athari hizo, mabomu hayo yalisababisha vifo vya wanafunzi watano wa shule mbalimbali za msingi kata ya Mbagala Kuu, akiwamo Mariam Musa (7) wa darasa la kwanza katika Shule ya Mbagala Kuu na John Joseph, darasa la tano wa shule ya Maendeleo.


Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Maendeleo, Omary Muyenjwa alisema mbali na athari hizo, mahudhurio ya wanafunzi yameshuka na kwamba, karibu nusu ya wanafunzi 3,350 hawafiki shuleni tangu milipuko ya mabomu ilipotokea.


Mwalimu Muyenjwa alisema mbali na mahudhurio kushuka, wanafunzi wake wengi hawasikii vizuri na baadhi wanadai kuwa hawapati usingizi kabisa tangu siku ya tukio.


“Watoto wengi mpaka sasa hivi masikio yao hayasikii vizuri, wengine wanaumwa vichwa muda wote. Pia baadhi hawapati usingizi kabisa tangu kutokea milipuko hiyo ya mabomu na bado tunafuatilia athari hizo kupitia walimu wao wa madarasa,” alisema Muyenjwa.


Kauli ya mwalimu huyo iliungwa mkono na mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mbagala Kuu, Paulo David aliyesema kuwa naye anaendelea kufuatilia taarifa zaidi kuhusu wanafunzi wake kupitia walimu wa madarasa.


Hata hivyo alisema mwanafunzi, Rebeca Abdallah (13) wa darasa la saba katika shule hiyo ni miongoni mwa walioathiriwa na milipuko na kwamba, hivi sasa hasikii vizuri na hapendi kukaa na wanafunzi wenzake.


Akizungumza na gazeti hili mwanafunzi huyo ambaye alikuwa amejitenga na wenzake, huku akiwa ameinamisha kichwa ukutani alisema, tangu aliposikia milipuko hiyo, masikio yake hayasikii vizuri, kichwa kinamuuma, moyo ukwenda mbio na hapati usingizi.


“Nikisikia kelele kichwa kinaniuma sana na moyo unaenda mbio maana nimekaa hapa peke yangu, ili nisisikie kelele darasani; lakini hata nikisikia mlio wa kengele moyo unaenda mbio na kuishiwa nguvu mwilini,’’ alisema Abdallah.


Kwa mujibu wa mwalimu huyo, mbali na mwanafunzi huyo kupata athari hiyo, shule yake imekuwa na tatizo la mahudhurio tangu milipuko hiyo itokee. Alifahamisha kuwa wanafunzi wanaohudhuria hawazidi 1000 kati ya zaidi ya 2000 waliopo katika shule hiyo.


Wataka ukaguzi usiku


Wakati huohuo, Salim Said anaripoti kuwa, baadhi ya waathirika wameiomba serikali kufanya ukaguzi nyakati za usiku katika maeneo waliotoa msaada wa mahema kwa sababu waliopewa hawahusiki na wanaitumia kupata misaada mingine ikiwamo chakula.


Wakazi hao walisema watu hao wanaweka mahema hayo mchana na usiku wanaenda kulala nyumbani kwao, kwa sababu hawakuathirika sana na milipuko hiyo.


Waliitaka serikali kubadilisha mfumo wa kutoa misaada na kutumia mfumo wa nyumba hadi nyumba au kuwaruhusu wanaotoa misaada kusimamia ugawaji.


Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti katika eneo la Mbagala, waathirika hao waliilalamikia baadhi ya mitaa ambayo wanadai kuwa hawakuathirika sana na mabomu hayo na wamepewa mahema lakini hawalali humo.


Miraji Omari alisema, watu hao hutumia mahema nyakati za mchana kwa ajili ya kupata misaada ya vyakula na mahitaji mengine.


“Watu tumekosa uaminifu, mtu anaomba hema kwa madai kuwa amekosa mahali pa kulala, lakini inapofika usiku analala nyumbani kwake,” alilalamika Omari.


Kwa upande wake, Devotha Benjamin alisema kitendo hicho kinasikitisha kwani wao ambao ndio waathirika wakubwa wa mabomu hayo mpaka jana walikuwa hawajapata mahema.


Aliilaumu serikali kwa kugawa mahema katika mitaa ambayo haikuathirika sana na kuiacha ambayo nyumba zake zote ziliangushwa chini kutokana na mtikisiko wa mabomu.


“Tunasikitika, hapa kwetu waliopata mahema ni wachache sana. Angalia mwenyewe (akionyesha nyumba zilizoanguka), nyumba zote hapa ziko chini, lakini mahema hayaonekani,” alilalamika Devotha.


Alifafanua kuwa mfumo unaotumiwa na serikali kugawa misaada kupitia wajumbe wa nyumba 10 si mzuri, kwa kuwa wengi wamekuwa wakikosa misaada hiyo, licha ya wasamaria wema kuitoa kwa wingi.


“Ni bora taasisi zinazotoa misaada zisimamie ugawaji au waigawe wenyewe kama walivyofanya hawa masheikh wanaogawa hivi sasa (jana saa 5:00 asubuhi),” alisema Devotha.


Naye Severina Joseph alisema: “Bora serikali ije usiku ikague, kwani mitaa ya Kichemchem, Mwanamtoti, Mbagala Kuu na Mtaa wa Warangi wamepewa mahema mengi, lakini usiku hawalali humo wanaenda nyumbani kwao,” alisema Severina na kuongeza:


“Huku kwetu hema moja linalaliwa na watu zaidi ya 10, wakati kule hayatumiwi.”


Aliishukuru taasisi ya Shura ya Maimamu kwa kuamua kusimamia na kugawa msaada wenyewe kwa walengwa, akisema haki inatendeka kupitia mfumo huo na si kupitia wajumbe.


“Kila siku naenda kwa wajumbe narudi mikono mitupu, kwani wakati mwingine wajumbe wanawakana watu wao, lakini leo (jana) nashukuru, mapema nilishapata msaada na sasa naondoka zangu…,” alisema Severina.


Omari Bakari pia alilalamikia utaratibu wa kupitishia misaada kwa wajumbe, akidai kuwa, namba za misaada husomwa katika kituo zaidi ya kimoja na kama haupo, wasiowaaminifu wanajitokeza na kuichukua badala ya muhusika halisi.


“Kwa mfano majina yanatajwa katika vituo tofauti, unaweza ukaenda kituoni ukakuta jina lako limetajwa na msaada umeshachukuliwa, ukidai unaambiwa tayari umeshapata,” alilalamika Bakari na kusisitiza:


Katika hatua nyingine, masheikh wa taasisi ya Shura ya Maimamu, walisimamia na kugawa msaada wa tani moja ya maharage, tani mbili na nusu za Sembe, nguo, chumvi na sabuni vyote vikiwa na thamani ya sh4.2 milioni kwa waathirika.


Ugawaji wa msaada huo kwa watu zaidi ya 500 bila ya kujali tofauti za kiimani, ulifanyika chini ya usimamizi wa Amiri wa Shura hiyo,Sheikh Mussa Kundecha katika viwanja vya Msikiti wa Taq-wa ulioathirika na milipuko ya mabomu hayo.


Akizunguza muda mfupi kabla ya kuanza kugawa msaada huo, Katibu wa Shura hiyo Sheikh Ponda Issa Ponda alisema, wameamuwa kugawa msaada huo kutokana na malalamiko yanayotolewa na walengwa kwamba haiwafikii.
 
Yani hii ingekuwa marekani, ma-lawyers wangekuwa wameshajipanga kushusha bonge la lawsuit, maana kazi yao ni kuzunguka mahospitalini na kungojea matukio kama haya wakombe hela. Sasa bongo na wanasheria wote, bado wamelala. Kwa kawaida sheria inakuwa kutokana na kesi zinazokwenda mahakamani. Sasa nyie mkikaa na kuhofia kushindwa kila siku, lazima sheria yenu pia ibaki nyuma. Mambo ya jurisprudence hayo. Hii inasikitisha.
Na ukiongea na wanasheria bongo, siku zote ni kukatishana tamaa. Mara huwezi kupambana na system ya bongo, nk. Penye nia pana njia bwana. Hata kama itachukua miaka mitano, watu lazima waende mahakamani. Watu wanasoma sheria wengi alafu wanashindwa kujiajiri wenyewe. Huwezi kukaa na kusuburi uajiriwe kila siku, hili ni tatizo la kuwa narrow minded. Anyway...thats besides the point here!
 
Yani hii ingekuwa marekani, ma-lawyers wangekuwa wameshajipanga kushusha bonge la lawsuit, maana kazi yao ni kuzunguka mahospitalini na kungojea matukio kama haya wakombe hela. Sasa bongo na wanasheria wote, bado wamelala. Kwa kawaida sheria inakuwa kutokana na kesi zinazokwenda mahakamani. Sasa nyie mkikaa na kuhofia kushindwa kila siku, lazima sheria yenu pia ibaki nyuma. Mambo ya jurisprudence hayo. Hii inasikitisha.
Na ukiongea na wanasheria bongo, siku zote ni kukatishana tamaa. Mara huwezi kupambana na system ya bongo, nk. Penye nia pana njia bwana. Hata kama itachukua miaka mitano, watu lazima waende mahakamani. Watu wanasoma sheria wengi alafu wanashindwa kujiajiri wenyewe. Huwezi kukaa na kusuburi uajiriwe kila siku, hili ni tatizo la kuwa narrow minded. Anyway...thats besides the point here!

Good advice, inaboa sana at least journalist wanafanya kazi yao.
 
Kumbeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeee ndio mmaaaaana kuna jamaaaaaaaaaaa wanajitangaza itv kuombaaaaa misaaaaaaad ya elimu kununulia vifaa vya elimu kwa ajili ya walemavu..........walishalijua hili
loh!!!!!!kaz kweli kweli
 
Back
Top Bottom