Watangaza nia wa CCM swali la kisiasa kutafutia majibu ya kitaalamu ni ukosefu wa umakini au ghiliba

Mkodoleaji

JF-Expert Member
Apr 27, 2008
458
138
Toka zoezi la kutangaza na kuchukua fomu kwa CCM kuibuka mambo mengi sana. Lakini kubwa lilillojitokeza ni nguvu za Waziri Mkuu wa Zamani Edward Lowassa. Lowassa alianza kutangaza nia kwenye mkutano wa hadhara na wagombea wengi tu wakafuata nyayo zake. Mimi nitamwongelea Lowassa na jinsi gani wanaompinga inawezekana hawako makini.

Linapokuja suala la kutafuta wadhamini, amekuwa akizoa na kuvunja rekodi kila mkoa. Wagombea wenzie kama Prof. Mwandosya wanasema hakuna haja ya wadhamini wengi maana wanaohitajika ni 450 (yaani 30 kila mkoa kwa mikoa kumi na mitano) na wengine wanasema anahonga ili kupata watu. Huu ni mfano wa kwanza wa kutumia jibu la kitaalamu kutatua swali la kisiasa.

Kwamba kupata wadhamini pia ni njia mojawapo ya kampeni. Inakufanya ujulikane na hivyo kujisafishia njia. Sasa kama mgombe anaongea na watu 100 tu halafu anaondoka, mwenzie anaongea na 50,000 nani anajiweka vizuri? Je hao wanaosema idadi ya wadhamini siyo muhimu wako makini kweli au wanafanya ghiliba na hawana mpango wa uraisi.


Kitu kingine, wanasema Lowassa ni fisadi (hapa sisemi kama Lowassa si fisadi - maana ndani ya CCM kumpata msafi ni kazi) na wanategemea atakatwa na Kamati Kuu ili asigombee. Jambo lile ambalo nimeliongelea mwanzo swali la kisiasa unatafuta jibu la kitaalamu.

Mgombea anashindwa kuwahamasisha watu kiasi cha kutosha ili waje wampigie kura, anasubiri kikao cha sijui watu 20 wapitie kanuni moja baada ya nyingine ili wamuondoe mtu aliyemobilise watu wa kutosha na yeye apate nafasi ya kugombea. Hapo pana ukakasi kidogo. Labda wangemsoma mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Kenya anaitwa Mutahi Ngunyi katika nadharia yake ya tyranny of numbers wangejua wanatakiwa kuwa makini zaidi. Hapo napo najiuliza maswali mengi kidogo:


1. Kama Chama kinataka ushindi, basi lazima kitamchagua mtu ambaye ameshawekeza kwenye kampeni ili kipate ushindi. Kwa Chama kumweka mtu ambaye hajulikani kabisa itakuwa ni kubeba mzigo mzito sana. Kosa kama hilo walilifanya KANU kwa kumweka Uhuru wakati alikuwa bado mpya. Wengine wanalinganisha na uchaguzi wa B.Mkapa 1995. Wanasahau kuwa wakati ule tulikuwa na mtu mwenye nguvu na ushawishi mkubwa ambaye ni J.K.Nyerere na tulikuwa tunafanya uchaguzi wa vyama vingi kwa mara ya kwanza hivyo Nyerere alikuwa anategemewa sana kutoa mwongozo.

2. Kitu kingine, ni kwamba hawa wagombea wengine wanasahau/wanajisahaulisha vitu vinavyompa nguvu Lowassa
a) Kutoka serikalini mwaka 2008 - Lowassa hata kama alijiuzulu kwa ufisadi ni kwamba hajawa serikalini toka mwaka 2008.

Hivyo makosa na kashfa zote za serikali toka 2008 hazimkumbi yeye. Hiyo imempa nguvu hata ya kuongea. Kitu kingine kwa sababu yuko nje ya serikali (power) wananchi wanaona kama vile ni mtu wao wanayetaka kumwingiza madarakani. Mara nyingi watu huwa wanawachukia watu walio madarakani na kuwapenda walio nje. Ni asili ya binadamu kuwaonea huruma wale wanaonekana kama ni wanyonge (msisitizo kwa wanaonekana).


b) Madai kwamba Lowassa haelewani na Kikwete- kuna madai kwamba Raisi Kikwete na familia yake hawaelewani na hawamtaki Lowassa. Wale wagombea wengine wanaona hili ni baraka kwao kwa sababu Raisi Kikwete anaweza kutumia rungu la uenyekiti kumponda Lowassa. Kitu kinachonishangaza ni kwamba kabla ya uchaguzi wa mwaka 2005, kulikuwa na madai kuwa Kikwete haelewani na Raisi Mkapa, hivyo wapinzani wa Kikwete walitegemea atakatwa jina. Lakini hakukatwa, sasa wapinzani wa Lowassa kwa nini wana matumaini hayo?

Kitu wanachokisahau ni kama nilivyoongea hapo juu. Kupendwa na familia ya kwanza (Raisi na familia yake) mara nyingi huwa haiwi baraka kwa sababu wananchi huwa wanapenda kumchagua mtu mwenye maamuzi na siyo mtu anayekuja kuendeleza mambo ya Raisi anayeondoka. Mara nyingi wananchi huwa wanaamini kumchagua mtu ambaye ni independent atakuwa mzuri zaidi (ingawaje ukweli mambo huwa hayaji kuwa kama wananchi walivyotegemea - but people are not rational)


c) Kuna wanaosema anahonga ili apate watu - sasa kama ukihonga unapata watu kwanini na hao wagombea wengine wasihonge ili wapate watu? Sina maana kama natetea rushwa ya kuhonga watu, lakini kama wananchi wanashawishiwa kwa pesa na wewe unataka uongozi unakwepaje kutoa pesa? Ukweli Lowassa anaweza kuwa anatoa pesa lakini sidhani kama kuna mgombea ambaye hatoi pesa. Tofauti inaweza kuwa nani unayempa pesa na unazo kiasi gani cha kutoa. Kwa hiyo kama wote wanatoa pesa- huo mtazamo wa kisheria za kijinai ambao unategema kumwondoa Lowassa unatoka wapi?

d) Lowassa anaungwa mkono na mafisadi - sasa hapa ndiyo tatizo kwa hao wagombea wengine. Nasema hivyo kwa sababu wanaomuunga mkono Lowassa na matajiri ambao siku zote wamekuwa wakikifadhili chama au kukijengea mikakati ya kupata fedha. Hapo unaongelea akina Rostam na sasa hivi Mzee Mengi na kundi lake la akina Sendeka. Sasa badala ya kuwatukana watu ambao wamekuwa wakikifadhili chama, nadhani wagombea ilibidi wawe makini na kuwashawishi ili wawaunge mkono.

Kifupi ni kwamba watangaza nia wengi wanaompinga LOwassa wanaweza wakashindwa na Lowassa kuibuka kidedea kwa sababu wanatafuta majibu ya kitaalamu kwenye swali la kisiasa (yaani looking for technical answers to solve a political question).

Mwenzao Lowassa kaamua kuwa mwanasiasa kuanzia mwanzo, wao wameamua kuwa wataalamu hivyo itakuwa ngumu kumshinda. Maana anatoa ushawishi mkubwa, hivyo hata wagombea ubunge wanaotaka kushinda ni lazima wamtake mtu mwenye ushawishi mkubwa. Nadhani kama kweli wanautaka Uraisi waende washawishi watu kwa nguvu na waache kulialia, vinginevyo itakuwa wanafanya ghiliba ili wamsindikize Lowassa
.
 
Simba mwenda kimya ndio mla nyama, ngoma ikilia sana huwa inapasuka, polepole jamani tusije umizana bure na utabiri wa shehe ukatimia
 
Back
Top Bottom