Wakazi Mwaboza waishi kwa kunywa maji machafu

Serayamajimbo

Senior Member
Apr 15, 2009
191
38
Asha Bani

amka2.gif

MAJI ni muhimu kwa maisha ya kila binadamu, bila ya maji hakuna binadamu anayeweza kuishi.
Lakini maji hayo hayo ni lazima yawe safi na salama, ambayo yatatumiwa na binadamu yeyote bila kusababisha madhara kama vile magonjwa ya milipuko ikiwa ni pamoja na kipindupindu, homa za matumbo, magonjwa ya ngozi na mengineyo.
Suala hili la maji na salama, kwa upande wa vijijini limekuwa gumu na sugu kutekelezeka ingawa katika maeneo mengine ya mijini suala hili limeonekana kutozingatiwa pia.
Nikiwa katika mkoa wa Tanga nilifanikiwa kutembea takriban majimbo yote, vitongoji na vijiji.
Katika maeneo hayo niliyotembelea ukiondoa tatizo kubwa la njaa lililokuwepo katika wilaya ya Kilindi, lakini pia kuna tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama.
Ukiona kilio cha maji katika mkoa huo hasa maeneo ya vijijini unaweza ukamkufuru Mungu kwa kusema kuwa mkoa huo hauna hata kiongozi mmoja anayewakilisha wananchi wake.
Mkoa wa Tanga umefanikiwa kuwa na wabunge 11, huku wengine wakionekana kupambana na mafisadi pindi wanapokuwa mjengoni (bungeni), lakini majimbo yao yanateketea.
Ingawa mkoa wa Tanga una matatizo lukuki kwa ila hapa nazungumzia tatizo moja la maji hasa katika wilaya ya Mkinga.
Katika kijiji cha Mwaboza, wilayani, humo kuna shida ya maji kiasi cha wakazi wa hapo katika vitongoji vitatu ikiwa ni pamoja na Mwaboza, Mwagula na Kirui, wote hutumia kisima kimoja.
Tanzania Daima ilishuhudia foleni ya watu huku wakisubiri maji huku wakazi hao wakisema kwamba tatizo hilo ni kubwa, ambapo wameiomba wizara husika kuwasimamia ili wapate maji safi na salama kama binadamu wengine.
Wakati nikiwa kijiji cha Mwaboza na msafara wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilichokuwa mkoani humo katika Operesheni Sangara, wakazi wa kijiji hicho waliamua kuuzuia msafara huo uliokuwa ukiongozwa na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, (CHADEMA) John Mnyika, aliyelazimika kusimama na kuwasikiliza shida zao.
Akizungumza kwa jazba mkazi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Asha Makame(60) anasema huwa anaamka asubuhi na mapema na kuchota maji katika kisimani ili kuhakikisha anafanikiwa kupata maji kwa matumizi ya nyumbani.
Anasema licha ya kusubiri kwa muda mrefu, anafanikiwa kupata ndoo moja ya maji kutokana na ukubwa wa foleni na wingi wa watu wanaotegemea kisima kilichopo kijijini hapo.
Alikuwa akizungumza kwa kulazimisha watu waliokuwepo katika msafara huo kuyaonja maji yale, kwa kile alichodai kuwa hayana ladha hata kidogo na kwamba kwa binadamu yeyote hawezi akayanywa maji hayo.
“Kama ninyi waandishi hebu onjeni haya maji ili muweze kuelezea vizuri kwa wakubwa wetu huko Dar es Salaam, wanaweza kusikia kilio hiki… kwa asiyeishi Mwaboza naamini hawezi kuyaonja hata kuyanywa maji haya.
“Sisi tunakunywa kwa kuwa hakuna sehemu nyingine ya kupata maji safi na salama,” anasema Makame.
Hata hivyo katika suala zima la shida ya maji mara nyingi kina mama wengi ndio wanaoteseka kwa kuwa wao ndio waliokabidhiwa majukumu makubwa ya kutunza familia.
Mwanamama mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Amina Mzee anasema wamekuwa wakipata shida kwa kutoka umbali mrefu kwa mashaka ili kutafuta maji, lakini matokeo yake maji hayo wanayoyapata yanakuwa si mazuri kwa afya.
Kila mkazi wa jimbo hilo hasa kina mama wamekuwa wakilalamika kwa kile walichokiita wao ndio waathirika wakubwa wa ukosefu wa maji hayo kwa kuwa wamekuwa wakitumia umbali mrefu na mara nyingine wamekuwa wakitumia siku nzima bila ya kupata maji.
Kutokana na hali hiyo wameiomba serikali kuwatatulia kero hiyo ya maji ambayo kwa upande wao imekuwa sugu huku wakiamini kabisa pindi itakapotokea magonjwa ya mlipuko wengi wao watapoteza maisha.
Naye Salma Saidi ameiomba serikali iwafikirie kuwapatia maji, mara nyingi wamekuwa wakiteseka huku wakiwa na watoto wao migongoni kwa kutafuta maji muda mrefu na wakati mwingine wamekuwa wakifanya kazi hizo ngumu hata wanapokuwa wajawazito jambo ambalo ni hatari kwa afya ya mjamzito.
Hata hivyo wakazi hao walisikika wakipayuka kwa kudai kuwa mbunge hajawahi kufika katika kijiji hicho hata kufanya mkutano nao tangu walipompa kura na kuwa mbunge.
Wanasema kuwa sababu kubwa ya mbunge wao kutoonekana ni kutokana na kwamba anaishi Dar es Salaam muda wote.
Akijibu malalamiko ya wakazi hao, Mnyika aliwaambia kuwa hayo ndiyo makosa makubwa waliyofanya kwa kuchagua mtu asiyewajali hivyo aliwaagiza pindi atakaporejea kudai kura mwaka huu wamfukuze na wasimpigie kura hata moja.
Katika kila kona ya jimbo mkoani Tanga malalamiko yanafanana, mkoa huo una wabunge 11 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) lakini hakuna hata mmoja anayeishi Tanga.
Anasema kutokana na wabunge hao kutokuwa na makazi majimboni mwao ni sababu kubwa ya kushindwa kujua matatizo ya wakazi wao waliowachagua ili kuweza kuwawakilisha pindi wanapokuwa bungeni.
Aidha, Mnyika amewataka mawaziri kuwajibika na kujituma kutokana na kero za wananchi hasa ikiwa kero hiyo kubwa ya maji.
Amemtaka Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Mark Mwandosya, kutembelea wakazi wa vijijini ili aweze kuwatatulia matatizo ya maji kupitia serikali. Naye Naibu Katibu wa Wanawake (BAWATA), Subira Shabani, amewasihi kina mama kutorubuniwa na wanasiasa ‘uchwara’ wanaoonekana majimboni katika kipindi cha uchaguzi. Anasema kina mama wengi ndio wamekuwa wakirubuniwa kwa kuhongwa kanga, vitambaa vya kichwani huku wakati wao ndio wahanga wakubwa wa matatizo ikiwa ni pamoja na kutafuta maji kwenye umbali mrefu na huduma hafifu za afya ya uzazi.
 
Back
Top Bottom