Wahubiri Wakongo wapewa siku 7 kuondoka nchini

BabuK

JF-Expert Member
Jul 30, 2008
1,845
329
WAHUBIRI wawili Raia ya Jamhuri ya Demokrasia ya Watu wa Congo (DRC) wamepewa amri ya kuondoka nchini ndani ya siku saba.

Watu hao wameamriwa kuondoka baada ya kubainika kuwa walikuwa wakiishi nchini bila kuwa na kibali huku wakiendesha huduma ya kuhubiri mitaani.

Watu hao ambao ni waumini wa kanisa la Sabato walikamatwa kufuatia taarifa zilizotolewa na raia kuwa kuna watu waliokuwa na mashaka na uhalali wao wa kuishi hapa nchini.

Akizungumza na gazeti hili jana, Naibu Kamishna wa Uhamiaji Mkoa wa Dodoma, Norah Masawe amewataja watu hao kuwa ni Ulinzi Bahuta Jean (36) na Kibariro Rwabajara Darius (52), ambao walikamatwa Mei 20, mwaka huu.

Alisema kuwa pamoja na kukosa vibali vya kuwa watumishi wa kuhubiri neno la Mungu pia walikuwa na hati ya muda ya miezi mitatu iliyotolewa kwa ajili ya kutembea nchini na si kwa ajili ya kuja kuhubiri injili, ambapo walikuwa wakifanya huduma hiyo kwa kutembea nyumba hadi nyumba.

Masawe alisema kuwa, kukamatwa kwa raia hao kulifuatiwa na taarifa iliyotolewa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Hazina aliyemtaja kwa jina la Monata baada ya wananchi kutoa taarifa ofisini kwake kuwa kuna watu walikuwa wakifanya huduma ya kuhubiri nyumba hadi nyumba hali iliyopelekea ofisa mtendaji huyo kutoa taarifa ofisi za Uhamiaji.

Naibu Kamishna huyo alidai kuwa, baada ya Wakongo hao kuhojiwa na Idara ya Uhamiaji walidai kuwa walikuwa wametokea mkoani Shinyanga na kufikia Kibaigwa wilayani Kongwa na baadaye Dodoma Mjini na walianza kuhubiri katika eneo la Hazina.

"Hata hivyo, Wakongo hao hawakuwa na vibali vilivyokuwa vikionesha kuwa vimetolewa na kanisa la Sabato nchini Kongo kuja kuhubiri hapa. Kutokana na hali hiyo uhamiaji waliiona ichukuwe hatua ya kuweza kuwahoji na hatimaye kuwapatia hati ya kuwafukuza ya wiki mmoja inayofahamika (PI) ili waweze kurudi nchini kwao mara moja," alisema.

Alisema kuwa, kukamatwa kwa Wakongo hao kumetokana na ushirikiano wanaoonesha wananchi baada ya zoezi la Elimu ya Uraia ya Uhamiaji Shirikishi ambayo inayotolewa na idara ya Uhamiaji nchini kote kwa ajili ya kuwaelimisha wananchi kwa lengo la kuwatambua wahamiaji haramu wanaoingia nchini.

 
Back
Top Bottom