Wabara watengwa Z`bar

JuaKali

JF-Expert Member
Nov 14, 2007
776
118
Lile chokochoko la kutaka Zanzibar itambuliwe kama nchi kamili sasa limepiga hatua zaidi baada ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuwasilisha sera ya vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi ikilenga kuwaengua wananchi kutoka Tanzania Bara kuruhusiwa kuajiriwa Zanzibar.

Msimamo huo tata uliwekwa bayana jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ, Suleiman Othman Nyanga, alipokuwa akiwasilisha sera ya vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea mjini hapa.

Kwa kauli hiyo, wenye vitambulisho vya Uzanzibari ndio watapewa kipaumbele cha ajira ili kudhibiti nafasi za kazi kuchukuliwa na wageni kutoka nje ya Zanzibar, wakiwamo watu kutokaTanzania Bara.

Waziri Nyanga alisema kwamba waajiri wote katika sekta binafsi watatakiwa na Wizara ya Kazi, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na watoto kuhakikisha wanatoa kipaumbele kwa Wazanzibari kabla ya kuwafikiria watu wengine kutoka nje ya Zanzibar.

``Taasisi zisizokuwa za Serikali zitakuwa na majukumu ya kutumia vitambulisho vya Mzanzibari katika kutoa kipaumbele kwa Wazanzibari katika kutoa ajira, mikopo na misaada ya kimaendeleo,`` alisema Waziri Nyanga.

Alisema kwamba mpango huo endapo utatekelezwa itasaidia vijana wengi wa Kizanzibari kunufaika na ajira na hivyo kufanikisha mpango wa kukuza uchumi na kupunguza umaskini kwa Wazanzibari.

Alisema kwamba Serikali itahakikisha kila Mzanzibari anasajiliwa na kupatiwa kitambulisho hicho na atatakiwa kutembea nacho wakati wote kama alama ya Mzanzibari.

Aidha, alisema kwamba kitambulisho hicho cha Uzanzibari mkaazi pia kitatumika kutoa kipaumbele kwa Wazanzibari wanaohitaji kunufaika na udhamini wa mikopo ya elimu ya juu kupitia mfuko maalum wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Waziri Nyanga alisema kwamba sera hiyo mpya itahakikisha kwamba inadhibiti uingiaji na utokaji wa watu katika maeneo ya Bandari na Uwanja wa Ndege kwa kutumia vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi ili kupunguza tatizo la uhalifu na mmonyoko wa maadili Zanzibar.

Waziri huyo alisema kwamba vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi vitatumika katika ugawaji wa ardhi, viwanja na nyumba za serikali ili kuepusha kupatiwa umiliki wa ardhi kwa watu wasiokuwa na sifa kwa mujibu wa sheria ya Zanzibar.

Aliwaeleza Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwamba watumishi wote wa serikali watalazimika kuonyesha vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi kabla ya kupokea mishahara ili kudhibiti vitendo vya wafanyakazi hewa.

Waziri Nyanga alisema kwamba serikali itahakikisha wanatoa vitambulisho maalum kwa wageni wanaoishi kwa ruhusa maalum za kazi ambayo itafanywa na Ofisi ya Msajili wa vitambulisho Zanzibar.

Alisema kwamba vitambulisho hivyo vimelenga kuimarisha usalama, kulinda haki za kiuchumi na kuongeza kasi ya maendeleo ya jamii kwa wananchi wake.

``Lengo kubwa ni kuwatambua Wazanzibari wote waliopo nchini na shughuli zao kwa lengo la kupanga vyema mipango ya maendeleo,`` alisema Waziri Nyanga.

Alisema kwamba vitambulisho hivyo vitasaidia kuwatambua watu walioko Zanzibar ambao wameingia bila ya kufuata utaratibu na kuhakikisha wananchukuliwa hatua za kisheria.

Alisema miongoni mwa matatizo yaliyojitokeza kutokana na kukosekana kwa vitambulisho vya Mzanzibari ni kushindwa kuthibiti vyema wimbi la uhalifu kutokana na kushindwa kuwatambua wale sugu pamoja na kushindwa kugawanya mapato na rasilimali zake kama vile ardhi kwa ajili ya mashamba, viwanja vya kujenga nyumba na hivyo rasilimali hizo kuangukia mikononi mwa watu wasiohusika kupata haki hizo.

``Kutokana na kushindwa kumtambua nani Mzanzibari, serikali hushindwa kutoa huduma kama vile elimu, matibabu na maji bila ya malipo na hivyo serikali hubeba mzigo mkubwa wa kutoa huduma kwa watu wasio Wazanzibari ambao wangesitahiki kuchangia huduma hizo,`` alisema Waziri Nyanga.

Alisema kwamba kwa msingi huo kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi ndiyo kitakachotumika katika utoaji wa ajira na leseni za vyombo vya baharini na angani.

Vilevile, alisema vitambulisho hivyo vitatumika kama alama ya Mzanzibari ndani na nje ya nchi na wale ambao ni wageni watakuwa na sifa ya kupewa vitambulisho hivyo baada ya kuishi Zanzibar kwa miaka kumi na kuomba kupewa Uzanzibari ukaazi kupitia Serikali za Mitaa na baadaye Mkuu wa Wilaya.

Wakichangia sera hiyo, Wajumbe wa Kambi ya Upinzani ya Chama cha Wananchi (CUF) walisema ili kukabiliana na vitendo vya uhalifu wa kutumia silaha na ukahaba Zanzibar ni vyema SMZ ikarejesha utaratibu wa watu wenye asili ya Tanzania Bara kuingia kwa hati maalum za kusafiria.

Wawakilishi waliochangia suala hilo ni Mwakilishi wa Jimbo la Gando, Said Ali Mbarouk, Mwakilishi wa Wawi, Soud Yusuf Mgeni na Mwakilishi wa Jimbo la Chakechake, Ali Omar, ambao walisema hivi sasa Zanzibar inakabiliwa na tatizo kubwa la uhalifu na biashara ya ukahaba kwa vile hakuna udhibiti wa watu wanaoingia na kutoka Zanzibar.

Hatua hii ya kuwatenga Watanzania kutoka bara ni mwendelezo wa Zanzibar kujitangaza kuwa nchi huru baada ya kufanikiwa kupata wimbo wa Zanzibar, bendera na hivi karibuni waliibua hoja nzito kuhusu rasilimali za nchi yakiwamo mafuta na madini.

Wazanzibari bila kujali itikadi zao, wameapa kwamba endapo mafuta yatapatikana kamwe hayawezi kuwa mali ya Muungano. Hivi karibuni Wazanzibari walianza kudai gawio kutoka benki Kuu ya Tanzania (BoT), na Waziri Kiongozi wiki hii atatoa tamko la SMZ kuhusu hisa zao BoT.

Mambo mengine ambayo yanaashiria kusukwasukuwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliofikiwa mwaka 1964, ni kutaka kutolewa wazi hati ya Muungano ili kubainisha ni mambo yapi Mwalimu Nyerere na Abeid Karume waliafikiana wakati wa kuundwa kwa taifa la Tanzania.
 
mnawachagulia watawala amba wao hawawataki

mnangania muungani amabo wao hawautaki

mnapeleka ujambazi na kuchangia kuharibu mila na desturi zao

mnawaburuza left and right

halafu mnategemea wasiwatenge?
 
Kwenye suala la kazi, nadhani wanaofanya kazi nyingi zanzibar haswa kwenye sector ya utalii unakuta wengi ni foreigners (hata sio kutoka bara), nadhani wao walitakiwa wakae chini wajiulize kwa nini watu wetu hawaajiriwi na wakishafahamu wanatafuta solution ya muda mrefu sio mambo ya kuzima moto.

Kwa mimi kwa kutumia tu muono wa nje nadhani tatizo kubwa la wazanzibari kutoajiriwa kwenye sector ya utalii ni elimu ndogo, elimu ya kawaida ya darasani na elimu kuhusu mambo ya sekta yenyewe ya utalii.....wasidhani kwa kuzaliwa na kukulia zanzibar inakufanya u-qualify.....it goes beyond that.

Wasipoangalia hao investors wachache walionao kwenye sekta ya utalii wanaweza kukimbia kama watalazimishwa kufanya mapenzi ya serikali inavyotaka bila kuangalia kuwa mtu aliyewekeza hela yake anahitaji kurudisha hiyo hela aliyowekeza, na mojawapo ikiwa ni kwa yeye kuajiri wafanyakazi competent watakaovutia watalii kuja.
 
Back
Top Bottom