Viongozi wa kuchongwa hawajali haki

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
SERIKALI ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inazidi kuongeza makucha yake ya udikteta kwa kukandamiza haki na demokrasia.

Katika kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, serikali ya CCM ilitumia ubabe kupitia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, ofisi za wakuu wa mikoa na wilaya, wakurugenzi wa halmashauri za wilaya pamoja na majeshi ya ulinzi na usalama.

Mikutano ya wapinzani ilivunjwa na polisi, msajili akaruhusu mgombea wa CCM ‘kuhubiri’ hadi usiku na Jeshi la Wananchi, ambalo jukumu lake kuu ni kulinda usalama wa mipaka, likaingia kutisha watu.

Kundi hilo ndilo limeshiriki kumchonga rais. Serikali ya CCM sasa inafanya kazi ya kuchonga mameya; kwamba ‘piga ua’, meya lazima atoke CCM.

Hizi ni dalili za juu kabisa kwa CCM, siyo tu kutawala kwa mkono wa chuma, bali pia kuitumbukiza nchi katika machafuko.

CCM, chama chenye wasomi lukuki, inafaa wakumbuke kuwa tawala zote za kidikteta duniani zilichukiwa sana na raia wake hadi zikajikuta zikianzisha mapambano na wananchi na hatimaye ziliporomoka.

Baadhi ya tawala hizo ziling’olewa na mataifa jirani na nyingine na wananchi wenyewe kwa mapambano (nguvu ya umma) au kwa sanduku la kura.

Nicolae Ceausescu wa Romania aliondolewa na raia; Maxamed Siyaad Barre maarufu kama Mohamed Siad Barre wa Somalia aliondolewa na wenzake.

Saddam Hussein wa Irak (alionewa au la) aliondolewa na Marekani pamoja na majeshi ya washirika na ndivyo alivyoondolewa Mullah Muhammed Omar, kiongozi wa Taliban nchini Afghanistan.

Tanzania ina uzoefu mzuri wa kushiriki kampeni za kuziondoa kwa nguvu za kijeshi serikali za kimabavu barani Afrika.

Mwaka 1979 ilishiriki kuing’oa serikali ya dikteta Idi Amin wa Uganda na mwaka 2008 iliongoza Jeshi la Afrika kumtimua Kanali Mohamed Bacar aliyejitangaza rais kisiwa cha Anjouan, nchini Comoro.

Katika hali ya kushangaza, serikali ya CCM inatumia nguvu kukandamiza haki za watu kama Ivory Coast inayotumbukia katika machafuko kutokana na dola kubaka ushindi wa Alassane Ouattara ikidai mshindi ni Laurent Gbagbo.

CCM imetumia dola kumchonga rais, ikaiba ushindi wa wabunge na madiwani wa upinzani ili kutekeleza kaulimbiu ya “Ushindi ni lazima”.

Huhitaji kuwa msomi mtaalamu wa masuala ya utatuzi wa migogoro duniani kujua kwamba uchaguzi wa meya wa Arusha ni batili.

Jiulize, hivi Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Asha-Rose Migiro wa Tanzania anaweza kupiga kura kuchagua rais wa Marekani kwa kuwa anaishi huko kwa sasa?

Au mawaziri kama Dk. John Magufuli (CCM-Chato), Dk. Harrison Mwakyembe (CCM-Kyela), Hawa Ghasia (CCM-Mtwara), Bernard Membe (CCM-Mtama), na wengineo, wanaweza kuhudhuria vikao vya halmashauri ya manispaa ya Kinondoni kwa kuwa kwa sasa wanaishi Dar es Salaam?

Inawezekana waziri mkuu Mizengo Pinda (CCM-Katavi), Spika Anne Makinda (CCM-Njombe Kusini) na William Lukuvi (CCM-Isimani) wakashiriki kikao cha halmashauri ya jiji la Dar es Salaam kwa kuwa wanaishi Dar es Salaam?

Je, kwa sababu zozote zile kikao chochote kinachokosa akidi ya wajumbe wenye sifa ya kuhudhuria kinaweza kisheria kupitisha maamuzi yakakubaliwa?

Mary Chatanda, Mbunge wa Viti Maalum kupitia mkoa wa Tanga, hana sifa ya kuwa mjumbe katika vikao vya madiwani wa halmashauri ya Arusha hata kama yeye ni Katibu wa CCM wilaya ya Arusha.

Kadhalika hana sifa ya kushiriki vikao vya CCM mkoa wa Tanga japokuwa ni kwao, ila kwa tiketi ya ubunge amepata sifa ya kushiriki vikao vya madiwani katika manispaa hiyo. Kinyume cha hayo, ni vurugu.

Inashangaza waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Mkuchika anasema “taratibu zimefuatwa.” Huyu ndiye Rais Jakaya Kikwete aliona kuwa ni kiongozi makini? Mtu makini anatetea uhuni?

CCM na vurugu

CCM walijitahidi kutengeneza mazingira ili wafuasi wa vyama vya upinzani walazimike kuanzisha vurugu. Sasa wanatumia polisi kuzuia mikutano halali ya CHADEMA na wamemdunda hata mbunge wao, Godbless Lema (Arusha), lakini wafuasi wao wamejizuia.

Wamegundua CCM inaandaa vurugu ili ipate kisingizio cha kutumia polisi kupiga, kujeruhi na ikibidi kuua wananchi – vyama vya kidikteta havioni shida kuua.

Polisi Kigoma wamemfungulia kesi Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe; wa Mwanza walimtia mbaroni Ezekiel Wenje (Nyamagana) na polisi wa Mbeya wamezuia mikutano ya Joseph Mbilinyi (Mbeya mjini) eti wakidai hali bado haijatulia Arusha. Mbeya na Arusha wapi na wapi?

CCM inatengeneza mazingira ili wabunge wa CHADEMA waonekane wamezaliwa kufanya fujo, watu wasiojali sheria. Wanadhani wakiwafarakanisha wabunge hao na wapigakura, wao CCM watapendwa. Wasahau.

Mamlaka yoyote inayozuia mikutano, inayozulia kesi na itakayomtambua Gaudence Lyimo kuwa meya halali manispaa ya Arusha inachochea vurugu. Hapahitaji mtu kurundikiwa digrii za heshima kujua CCM inapalilia vurugu.

CCM wameonja pepo

Kisa cha CCM kung’ang’ania madaraka kimesimuliwa vizuri na Farouk Topan katika tamthiliya ya “Aliyeonja Pepo” iliyojaa ucheshi.

Eti malaika mtoa roho alimpaisha peponi jamaa mmoja wa Bagamoyo aitwaye Juma Hamisi mwaka mmoja kabla ya siku yake.

Eti Bwana Mkubwa akiwa amekaa alishangaa kuona aliyepaswa kula raha, John Houghton wa Birmingham bado alikuwa anapata dhiki duniani.

Akafoka sana halafu akaagiza Juma Hamisi arejeshwe haraka duniani na atwaliwe John Houghton. Je, inawezekana?

Je, NEC inaweza kufuta matokeo ya rais waliyemchonga na ikatangaza mshindi wa kweli? Kazi ngumu! Hicho ndicho Topan anakijadili; kwamba ama kwa uzembe au upendeleo Juma Hamisi amepewa fursa au ushindi asiostahili.

Anapendekeza kisanii Juma Hamisi afufuliwe na arudi kuendelea na kazi zake Bagamoyo. Kwamba taratibu zilizotumika kumpa fursa hiyo au ushindi zitenguliwe.

Kazi akapewa malaika mfufuaji kumwita Juma Hamisi na kuzungumza naye. Katika kikao chao, Juma Hamisi akasema hawezi kuacha raha na wanawake wa bure.

“Kati ya sisi wawili mmoja wetu ni mwendawazimu, lakini si mimi,” alisema.

CCM inawaona wendawazimu wote wanaopendekeza matokeo ya urais yatenguliwe. Hawawezi kuacha raha ya ufisadi wanaofanya kupitia miradi ya Richmond, Meremeta, mikataba ya madini; wizi wa EPA; rushwa za rada na miradi mikubwa ya nchi; uporaji wa ardhi ya wananchi. Rais wa kuchongwa atalinda haya.
Viongozi wa kuchongwa hawajali haki | Gazeti la MwanaHalisi
 
Back
Top Bottom