Viongozi wa DECI matatani tena

Invisible

Robot
Feb 11, 2006
9,075
7,878
Imeandikwa na Regina Kumba;
Tarehe: 15th December 2009
HabariLeo


VIONGOZI wa Taasisi ya Development Entrepreneurship for Community Initiative (Deci), jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwa mashitaka mengine ingawa hawakusomewa mashitaka hayo kwa sababu muda wa mahakama ulikuwa umekwisha.

Vigogo hao ambao wanashikiliwa na polisi tangu Desemba 8, mwaka huu, walirudishwa rumande katika Kituo cha Polisi cha Msimbazi hadi leo watakapopelekwa tena mahakamani kusomewa mashitaka yao, kwa sababu walifikishwa mahakamani hapo baada ya saa nane mchana bila kufahamika sababu ya kuchelewa kufikishwa.

Mahakama humaliza kazi zake saa 9.30 alasiri, ingawa watuhumiwa wakishafikishwa hao sio lazima wapandishwe kizimbani muda huo huo, kwani kuna taratibu za kimahakama zinazopaswa kufanyika kwanza.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana mahakamani hapo, viongozi hao walikamatwa katika benki moja hapa mkoani Dar es Salaam wakidaiwa kufanya shughuli za kibenki katika akaunti ambayo haikuwa ikifahamika na serikali wakati akaunti zao zote zinazofahamika zimeshikiliwa na serikali.

Ilielezwa kwamba viongozi hao kabla hawajafikishwa mahakamani Juni 13, mwaka huu, wakikabiliwa na mashitaka ya kufanya biashara ya upatu bila kibali, walitaka kununua jengo jijini ambalo gharama yake inadaiwa kuwa Sh milioni 260, wakalipa Sh milioni 120 na fedha nyingine wakakubaliana kulipana baadaye.

Hata hivyo, ilielezwa kwamba hawakumalizia deni hilo baada ya kufikishwa mahakamani, hivyo mwenye nyumba hiyo akapata mteja mwingine ambaye alitaka kulipa fedha zote na hivyo kuamua kuwasiliana na viongozi hao wa Deci ili kuwarudishia fedha zao.

Ilielezwa kuwa walikubaliana kukutana katika benki hiyo waliyokamatwa ili mwenye jengo awarudishia Sh milioni 120 zao na jengo kuuzwa kwa mteja mwingine, ndipo walipokamatwa na polisi baada ya kupata taarifa.

Vigogo hao waliondolewa mahakamani jana ambapo ilielezwa kwamba Hakimu Mkuu Mfawidhi, Elvin Mgeta hakuwepo muda huo, jambo lililofanya warudishwe rumande na kuondolewa mahakamani saa 9.30 alasiri katika gari aina ya Toyota Carina lenye namba za usajili T833 BDU na Mitsubishi Pajero lenye namba T515 BBH.

Katika kesi inayowakabili vigogo hao ambao wako nje kwa dhamana, ni ya kuendesha na kusimamia mchezo wa kuchangisha fedha kwa ahadi ya malipo maradufu, maarufu kama Panda Mbegu.

Wanadaiwa kufanya kosa hilo kwa tarehe tofauti kati ya mwaka 2007 na Machi mwaka huu, wakikiuka kifungu namba 171A (1) na cha (3) cha kanuni ya adhabu cha mwaka 2002. Wanadaiwa kufanya kosa hilo kwenye makao makuu ya Deci yaliyo eneo la Mabibo Mwisho wilayani Kinondoni.

Washtakiwa hao wanadaiwa kusimamia mradi wa upatu kwa kuchukua fedha kwa wananchi kwa ahadi ya kuwapa matumaini ya fedha zaidi kuliko mapato ya mradi waliokuwa wakiuendesha.

Vigogo hao ni Jackson Mtaresi, Dominic Kigendi, Samwel Mtaresi, Arbogasti Kipilimba na Timothy ole Loiting’inye.

Akaunti zao zote zinashikiliwa na serikali kutokana na kesi hiyo inayowakabili na walikuwa hawaruhusiwi kufanya shughuli zozote za kibenki.
 
Back
Top Bottom