SoC03 Uwajibikaji kwenye elimu Tanzania - ni nani anahusika?

Stories of Change - 2023 Competition

Digital Ticha

Member
Jun 16, 2023
26
55
Matokeo ya mtihani wa moko wilaya ya darasa la saba yametoka na kutangazawa na mamlaka ya elimu. Ni matokeo mabaya kuwahi kutokea kwa miaka mingi tangu kuanzishwa kwa shule hii ya msingi Nyakavangala. Kamati ya shule inaweka taarifa ya matokeo katika ubao wa matangazo.

Wazazi na wananchi wa Nyakavangala wanakwenda kuyatazama matokeo na kubaini wanafunzi wengi wamefeli mtihani huo na somo la Kiingereza ndio lina matokeo mabaya zaidi kwani wanafunzi wote wamepata alama hafifu. Hakuna mwanafunzi hata mmoja aliyeweza kufaulu somo ili, hakika ni matokeo ya kushtusha na kuwasikitisha wazazi. Kinachowasikitisha zaidi ni shule yao kushika mkia katika matokeo ya jumla ya wilaya ya Iringa.

Wazazi wana hamaki na kuanza kutoa lawama nzito kwa walimu kuwa hawafundishi vizuri na ndio chanzo cha matokeo mabaya hapo shuleni. Mzozo unakuwa ni mkubwa maeneo ya shuleni kiasi kwamba inatokea sintofahamu.

Baada ya mjadala wa muda mrefu hatimaye kunapatikana muafaka. Sasa wazazi wanataka kukutana na Mwalimu Mkuu wa shule ili wafanye mazungumzo ya dharula na ni dhairi bado wana hasira kali. Hakuna wa kushusha munkari yao kwa urahisi isipokuwa neno kutoka kwa mkuu wa shule.

Mwalimu Mkuu anakuwa muungwana anakubali kuonana na wazazi na wanafanya kikao cha dharula. Wazazi wanataka kujua kwa nini watoto wamefeli kwa kiasi hicho mitihani yao. Na haswa somo la Kiingereza ambalo watoto wote wamefeli kwa kupata daraja F.

Kwenye kikao Mwalimu Mkuu anawajulisha wazazi kuwa walimu shuleni hawatoshi na mwalimu wa somo la Kiingereza ameondoka shuleni miezi nane (8) iliyopita na tangu aondoke wilaya haijatuma mbadala wake.

Mwalimu Mkuu anaendelea kuwataarifu kwamba licha ya yeye kufanya jitihada zakupeleka maombi wilayani mara kwa mara ili waongeze walimu shuleni hususani mwalimu wa somo la Kiingereza lakini jitihada zake bado hazijazaa matunda kwani bado hajapata majibu rasmi kutoka kwenye idara ya elimu wilaya.

Kwenye kikao wazazi wanaazimia kuandika barua ya malalamiko yao kwa mbunge na kusainiwa na wazazi wote. Malalamiko yao yanahusu matokeo mabaya ya wanafunzi na upungufu wa walimu hususani wa somo la Kiingereza ambalo wanafunzi wamefanya vibaya zaidi.

Mwalimu Mkuu naye anaamua kuandika barua nyingine kwa Afisa Elimu wa wilaya akimkumbusha kuhusu hali hiyo pia kumjulisha kuhusu mgogoro uliotokea shuleni.

Mbunge baada ya kusikia hii habari anaguswa na kilichotokea hivyo anaomba taarifa rasmi kutoka kwa Afisa Elimu Wilaya. Anataka taarifa rasmi ili aweze kuifanyia kazi.

Afisa Elimu anajibu kwamba kuna upungufu mkubwa wa walimu lakini walipata mwalimu mmoja kwenye awamu iliyoisha ya ajira mpya, alikuwa ni mwalimu wa Kiingereza ila mwalimu alikataa kwenda kufundisha Nyakavangala kwa sababu hakuna nyumba ya mwalimu na huduma zingine muhimu kama maji safi, umeme, zahanati na mawasiliano ya simu.

Shule ya msingi Nyakavangala ipo umbali wa zaidi ya kilomita 120 kutoka makao makuu ya wilaya ya Iringa Vijijini. Inapatikana kijiji cha Nyavangala kwenye kata ya Malenga Makali. Ni shule iliyozungukwa na msitu mkubwa wa miti ya mibuyu kwenye eneo lenye ukame na imejengwa pembeni kidogo ya kijiji . Wakazi wake wanafanya shughuli za kilimo na ufugaji kama njia kuu ya kujipatia kipato.

Baada ya kupata mrejesho huo kutoka wilayani wanajamii wa Nyakavangala wanakaa tena kikao ambacho cha sasa kikihusisha wazazi wote na viongozi kujadili taarifa kutoka kwa Afisa Elimu.

Wazazi kwenye kikao wameafikiana kuajiri mwalimu wa muda mfupi ambae atalipwa na shule kwa michango ambayo wamekubaliana kuchangia. Kila mzazi mwenye mtoto shuleni atachangia shilingi elfu tano kwa ajili ya posho ya kila mwezi ya mwalimu wa somo la Kiingereza. Lakini pia wamekubaliana kujenga nyumba mbili za walimu kwa kutumia mfuko wa maendeleo ya kijiji.

Mbunge wao ametoa ahadi ya kuwaunga mkono kwa kutoa mifuko ya saruji na mabati ya kusaidia ujenzi.

Hatimaye baada ya kuzungumza na kusikilizana Nyakavangala inapata suluhisho la baadhi ya changamoto zake.

Kisa hiki cha Nyakavangala kinafanana na shule nyingi zilizopo ndani ya nchi yetu. Bado mfumo wetu wa elimu una changamoto nyingi zinazopelekea kupata matokeo mabaya ya kitaaluma pamoja na kuzalisha watoto wasio na maarifa ya kutosha kuweza kukabiliana cha changamoto za kimaisha.

Moja ya changamoto kubwa ni ukosefu wa uwajibikaji, uwazi na ujumuishi. Shule zetu nyingi zinaendeshwa bila kuzingatia uwazi, ufasaha na kuhakikisha kila mmoja anayepaswa kushirikishwa anashirikishwa.

Changamoto nyingine ni upungufu mkubwa wa walimu pamoja na vifaa vya kujifunzia na kufundishia. Pia miundombinu haitoshi na iliyopo ni mibovu bila kusahau watoto hawapati chakula cha mchana shuleni hivyo kusababisha kiwango cha taaluma kuendelea kuwa chini.

Shule ni mali ya jamii lakini jamii zinazozunguka shule bado hawaoni kama wanawajibika kuzilea na kuzisaidia shule kadhalika serikali inafanya jitihada ila bado imeshindwa kutosheleza kila raslimali inayohitajika shuleni. Hivyo matatizo mengi bado yanaendelea kuzisumbua shule zetu miaka na miaka.

Nini kinapaswa kufanyika? Ili ni swali ambalo kila mmoja anapaswa ajiulize. Kwanza serikali kwa kushiriana na wadau wa elimu inapaswa kutengeneza muundo na sera zinazochochea uwajibikaji na ufanisi kutoka katika pande tatu zinazosimamia shule yani jamii, uongozi wa shule na serikali.

Mfano, kwenye idara ya elimu ngazi ya halmashauri anakosekana mtaalamu ambaye ni kiungo kati ya jamii, shule na serikali. Hivyo ili kuhakikisha kuna ushirikiano mzuri kati ya shule na jamii ni wakati sasa wa serikali kuongeza nafasi ya Afisa Mhamasishaji Jamii Elimu ambaye atakuwa kwenye halmashauri akimsaida Afisa Elimu kuratibu shughuli ambazo jamii inatakiwa kufanya kuzisaidia shule ambaye pia atakuwa na jukumu la kuzijengea uwezo jamii kutafuta namna ya kuongeza rasilimali kwa ajili ya shule.

Wazazi na jamii wao wanapaswa kupewa elimu na hamasa ili wafahamu wajibu na majukumu yao kwenye shule. Hii kazi inapaswa kufanywa na wadau wote wa elimu. Wazazi wanapaswa kufahamu kuwa wao ndio wachangaiaji namba moja wa maendeleo ya shule kwani tukiiachia serikali peke yake changamoto haziwezi kumalizika kwa urahisi.

Utawala wa shule na walimu wanawajibu wa kuwashirikisha wazazi na jamii kwenye maamuzi ya msingi na kuhakikisha kila mdau anafahamu kinachoendelea shuleni na kuna uwazi kwenye matumizi ya fedha za maendeleo ya shule. Kamati za shule zinapoandaa mipango kazi ya maendeleo ya shule waanzie kwenye jamii kwa kuchukua maoni ya wanajamii wanaozunguka shule waseme wanataka nini kiingie kwenye mpango wa maendeleo ya shule hii itasaidia mipango ya shule kutekelezeka.

Nina hakika haya yakifanyika tutaona ubora wa elimu yetu ukiongezeka.
 
Back
Top Bottom