Utii wa sheria usalama barabarani sasa unahitaji msukumo mpya

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,318
33,125
Kuzidi kuboreshwa kwa barabara nchini kwa kujengwa kwa kiwango cha lami kumekuwa na athari zake, kikubwa kuzidi kuhatarishwa kwa maisha ya watumiaji wake, hususani waenda kwa miguu.

Wakati ubora wa barabara ulitarajiwa kurahisisha sekta ya usafirishaji na kupunguza uharibifu wa vyombo vya moto, mwenendo wa utumiaji wa barabara kwa maana ya wadau mbalimbali kama madereva, watembea kwa miguu na watumiaji wa vyombo vingine vya usafiri kama pikipiki na baiskeli nao umeibua changamoto juu ya usalama wa barabara hizo.

Mathalan, kutokana na uendneshaji wa ovyo kabisa wa magari barabarani, kwa maana ya kutokuzingatia sheria za usalama barabarani, kama vile vivuko vya waenda kwa miguu, ishara za miinuko mikali na hata madaraja, imelazimisha Wakala wa Barabara (Tanroads) kujenga matuta katika barabara ambazo kimsingi sheria za kimataifa za barabara kuu haziruhusu, ili tu kunusuru maisha ya watumiaji wa barabara hizo kutokana na ajali.

Ukichukuliwa mfano wa vivuko vya waenda kwa miguu, ni nadra sana kuona madereva wakiheshimu alama hizo, hivyo kusababisha madhara makubwa kwa watembeao kwa miguu. Imetokea mara nyingi tu watu kugongwa wakivuka kwenye vivuko hivyo, mara nyingi madereva wa vyombo vya moto wanaamini kwamba wana haki ya kutumia barabara kuliko wadau wengine wote.

Ni kwa maana hiyo, upuuzaji wa sheria za usalama barabarani ni wa kiwango cha juu kwa upande wao, hali ambayo imezifanya barabara zetu kutokuwa salama kabisa.
Hali hii ya kutokuzingatia sheria imefikisha baadhi ya madereva, hasa wanaotumia magari binafsi, kusema kuwa uendeshaji wa magari katika miji mikubwa kama Dar es Salaam suala si kuzingatia sheria tu, ila kujihadhari hata kama unafuata sheria kwa sababu wapo madereva wengi vichwa maji.

Kundi kubwa la madereva vichwa maji ni wale wanaoendesha mabasi ya daladala, madereva pikipiki, lakini pia madereva wa malori ya mchanga, maarugu kama Fuso.
Pia wapo madereva teksi, kwa umoja wao kundi hili kila awaye barabarani anaamini ama ana haki kuliko mtumiaji mwingine yeyote wa barabara, au ana haraka kuliko mtumiaji mwingine yeyote.

Ndiyo maana matukio ya madereva kuyapita magari mengine kwenye kona na miinuko mikali kiasi cha kusababisha ajali ni ya kawaida kabisa, matukio ya kugonga waenda kwa miguu ni mambo ya kila wakati katika miji mikubwa nchini, hususan Dar es Salaam.
Lakini pia kuna tatizo la madereva wa daladala kuamini kabisa kuwa kuegesha gari pembeni mwa barabara ili kushusha na kupakia abiria ama ni kupoteza muda au kujichosha bure, hivyo husimama katikati ya barabara na kusababisha msongamano mkubwa wa magari.

Kutokana na kupuuza sheria za usalama barabarani wananchi ambao mara nyingi wamekuwa waathirika wa vitendo hivyo vya ukiukaji wa sheria na kanuni nao wameibuka na mbinu ya kukabiliana nayo, wameshinikiza kujengwa kwa matuta katika barabara kuu ambazo zilijengwa ili kurahisisha mawasiliano.

Hakika matuta haya yamekuwa na mathara makubwa sana kwa uchumi wa taifa; moja, kila lilipojengwa tuta barabara zinaanza kuharibika hapo, haijalishi ni barabara ya ubora wa kiwango gani, ukweli huu uko dhahiri. Matokeo yake ni kwamba badala ya barabara kudumu kwa muda uliopangwa, huanza kuharibika mapema sana, hivyo kugharibu sana uchumi wa nchi.
Wamiliki wa magari nao wamejikuta wakiingia hasara kubwa katika kuendesha vyombo vya moto barabarani kwa sababu matuka hayo yamekuwa chanzo kikubwa cha kuvunjika kwa vipuri ama kuchakaa kwa haraka kwani matuta kwenye barabara ya lami ni sawa kabisa na kusema kuwa barabara husika imejaa mashimo.
Hali hii imepandisha sana gharama za kutunza vyombo hivyo, hali ambayo inakuwa mzigo mkubwa kwa wananchi kumiliki na kutumia vyombo vya moto.

Wananchi nao katika mkoroganyo huu pia wanachangia uvutujaji wa sheria za usalama barabarani, wengi wanapuuzia sheria hizi, wakiwekewa vivuko mara nyingi hawavitumii ipasavyo, wanavuka tu kienyeji barabarani bila kujali.
Wapo waliozoea barabara kiasi cha kuleta kero kubwa kwa madereva hasa sehemu zenye mkusanyiko mkubwa wa watu.

Kwa ujumla, sisi kama taifa bado hatujaelewa maana na umuhimu wa kuheshimu na kuzingatia sheria za usalama barabarani.

Mikakati ya kuhimili majanga ya ajali kama matuta inabuniwa, lakini matokeo yake yanaathiri uchumi wetu, yaani ni sawa na kusema kuwa hatua hizo zinakula kwetu kama taifa.
Tunafikiri wakati umefika sasa kwa umma kutambua kuwa kutokuheshimu sheria za usalama barabarani gharama yake ni kubwa sana, si lazima iwe hivyo kwa sababu ya vifo vya ajali tu, bali hata kugharimu fedha nyingi kutunza barabara zinazoharibiwa na matuta ya kila mahali. Tubadilike sasa.

CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom