Ukosefu wa dira unalipeleka Bunge letu pabaya

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,322
33,127
Hatua ya Spika wa Bunge Anna Makinda kuivunja Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini ni kifungua macho kuhusu nini hasa kinatokea bungeni, na hasa mipaka ya uzalendo na utumishi wa umma katika hatua tofauti za wabunge hasa kuanzia kipindi hiki cha awamu ya nne.

Hali hiyo imejitokeza baada ya baadhi ya wabunge kuanzisha hoja ya kutaka kung’olewa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi na Waziri Profesa Sospeter Muhongo kwa kutofuata utaratibu katika kutoa tenda ya kuingiza mafuta mazito kwa kuzalisha umeme wa IPTL. Kwa vile ‘siku

za mwizi ni arobaini,’ safari ikafahamika kabisa kuwa wako waliochukizwa na hatua hiyo ingawa ilikuwa kwa manufaa ya umma.
Waliofuatilia kilichotokea bungeni katika miezi ya hivi karibuni wanakumbuka kuwa ilikuwa ni mfululizo wa madai kama hayo ambako ilimlazimu Rais

Jakaya Kikwete kubadilisha Baraza la Mawaziri licha ya kutokuwa na imani na yaliyosemwa kuhusu baadhi yao.
Wakati ule utetezi wa mawaziri haukusikilizwa na badala yake wabunge wakafaulu katika kuwatupia lawama mawaziri, wakati ’madudu’ waliyokuwa wakizungumzia yalitokea zaidi katika mashirika ya umma na serikali za mitaa.

Kutokana na kutaka kuwa mawaziri ndiyo wawajibike kwa hilo, walioingia madarakani sasa wameyakalia kooni mashirika ya umma kuhakikisha kuwa hawafanyi wanachotaka halafu lawama zitupiwe uongozi wa juu zaidi katika wizara.

Kwa kawaida mashirika ya umma yalikuwa huru kuendesha shughuli zao, na wasimamizi wa mwisho kimsingi ni bodi na si wizara, labda pale ambapo serikali inahitajika kuridhia mahusiano fulani ambako shirika haliwezi kujitegemea, na siyo masuala ya tenda ndogo kama hiyo ya Puma Energy, na kadhalika.

Kwa miaka mingi kumekuwa na uhusiano wa kiitikadi kati ya mashirika ya umma na wabunge, ambako nia muhimu ni kuwa wasiingiliwe katika shughuli zao, na muhimu zaidi ni kuondoa kila wazo la urekebishaji wa sheria kuhusu mashirika ya umma, masuala ambayo sasa inaelekea yanarudi ‘mezani.’

Kwa mfano serikali inapata shida sana kulipa madeni ya Tanesco kwa wazalishaji umeme binafsi, na kujazia nakisi ya uendeshaji wa shirika, wakati inajijazia gharama kupitia miradi ya Pwagu na Pwaguzi, na sasa inafichuka.

Kwa mfano, Waziri Prof.Muhongo alieleza ‘dili’ za Tanesco ambazo hadi sasa hakuna mtu ambaye angeweza kuzigusa, kuuza nguzo za kupitisha umeme nchini Kenya halafu kuzinunua kutoka huko, wakati zimeuzwa na shamba la serikali ambalo kazi yake ni kuihudumia Tanesco ipate nguzo.

Halafu, wakati nguzo hizo zinatengenezwa hapa nchini watemi wa Tanesco wanachangisha shilingi milioni moja kwa mtu anayetaka kuunganishwa umeme kama kuna nguzo moja inahitajiwa, au zaidi ya laki tano bila nguzo.

Hii sasa inarekebishwa na kuanzia mapema mwakani gharama za kuunganisha umeme tayari zitashushwa kwa karibu nusu hasa kwa watumiaji wa kawaida, mijini na vijijini wasitaabike kupita kiasi.

Hadi sasa dhana ya wabunge ya ‘utawala bora’ imekuwa ni utiifu kwa mashirika ya umma na kuondoa kila wazo la kuyabinafsisha, na pia kutokuingilia wanachofanya kwa kuwa wao ndiyo wataalamu, na watendaji wizarani wanapoingilia ni kwa sababu ‘wana lao jambo,’ na ndiyo pia tulivyoambiwa wakati wa sakata la Richmond na Dowans.

Kumbe inawezekana kulikuwa na akina Eliakim Maswi na Prof.Muhongo wenye uzalendo lakini hakuna aliyejua janja ya baadhi ya wabunge wakati huo, na makundi CCM yakafanikisha mipango iliyobaki, lakini ‘za mwizi ni arobaini.’ Baadaye tukaambiwa mitambo ile ni mikuukuu, tusiinunue; sasa tunajua ni uwongo mtupu.

Hakika Bunge letu limeweka historia kwa kudhihirisha uzalendo hasa linapokuja suala la kitaifa kama hilo la mgowo wa umeme na madudu mengine yaliyotajwa bungeni kuhusu shirika letu la umeme Tanesco. Tunaamini kuwa kama alivyosema Spika Makinda, hata wale wote waliohusika katika madudu hayo watachukuliwa hatua stahiki nchi yetu isonge mbele.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

 
Back
Top Bottom