Ujuzi wa miaka 38 wa kutengeneza pikipiki wamfanya aunde helikopta

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,318
33,125
Ujuzi wa miaka 38 wa kutengeneza pikipiki wamfanya aunde helikopta
Imeandikwa


07_09_gqtqxh.jpg

Helkopta hiyo yenye jina la RASOMAKA
Habari Zaidi:

AMINI usiamini, kila mwanadamu amezaliwa na kipaji chake ambacho kama akikitumia vizuri, kitamnufaisha. Hivi ndivyo fundi pikipiki, Ramadhan Said (51), mkazi wa Magomeni Makanya jijini Dar es Salaam na mzaliwa wa Singida Ipembe, yuko kwenye hatua za mwisho za kuunda helikopta.

Akizungumzia ubunifu wake, fundi Ramadhan anasema ingawa hakumaliza elimu ya sekondari, aliweza kujifunza ufundi makanika na kufaulu vizuri. " Nilifaulu na dada zangu wawili kwenda sekondari, ila niliishia kidato cha kwanza na kupelekwa kujifunza umakanika", anasema fundi Ramadhan.

Anasema kushindwa kwake kuendelea na masomo ya sekondari, kulitokana na matatizo ya kifamilia hivyo baba yake kumpeleka masomo ya ufundi. Ramadhan anasema baada ya kumaliza ufundi makanika aliajiriwa na kampuni na idara mbalimbali za ujenzi na kufanya kazi kama fundi magari, pampu za maji, pikipiki na kazi nyingine za ufundi.

Ni ujuzi huo ndio uliomfanya abuni jinsi ya kutengeneza helkopta, ambapo kwa mara ya kwanza akiwa Chunya Mbeya alitengeneza helkopta ndogo isiyo na mtu. Mafanikio ya helkopta hiyo ya kwanza aliitengeneza mwaka 1988, akiwa kwenye machimbo ya dhahabu, mara baada ya kuacha ufundi kwa muda.

Anasema wakati akifanya kazi kwenye machimbo ya madini ya dhahabu, wakati wa mapumziko, alikuwa akiutumia kutengeneza chombo hicho. "Muda wa mapumziko akili yangu ilinituma kubuni hiki chombo na nilikuwa na fomula ya utengenezaji wa helkopta", anasema fundi Ramadhan.

Helkopta ya sasa ambayo iko kwenye hatua za mwisho ya kuwekewa injini na kutengenezewa stendi ya kusimamia. Mara baada ya kukamilika, ambapo anategemea kuiwasha Desemba mwaka huu, itakuwa na uwezo wa kuruka mita 100 hadi 150 kutoka usawa wa bahari.

Helkopta hiyo ina kila kifaa kinachohitajika kwenye helkopta za kawaida, tofauti ni kwamba ametumia injini ya pikipiki. Injini hiyo ina ukubwa wa cc 750, na alianza kukusanya vifaa mwaka 2007 ambapo mwaka 2008 mwezi Februari alianza kuitengeneza. Fundi Ramadhan ambaye ni mmoja wa mafundi bora na makini wa pikipiki katika Jiji la Dar es Salaaam, kazi yake anaifanyia eneo la Kagera, Magomeni.

"Sijaacha ufundi wa pikipiki, bado naendelea kufanya, na huu wa kutengeneza helkopta naufanya siku za Jumapili", anasema Fundi Ramadhan. Vifaa anavyotumia kutengeneza helikopta hiyo vyote ni vya pikipiki, ila ameviboresha kwa ajili ya kutumika kwenye helkopta.

Anasema mara baada ya kukamilika na kufanikiwa jaribio hilo, anategemea kutengeneza nyingine kubwa kama atapewa kibali cha kufanya hivyo na mamlaka husika. Hii ya sasa inayokwenda hatua za mwisho za matengenezo ina uwezo wa kuchukua watu wawili. Gharama ambazo hadi sasa ameshatumia kutengeneza helkopta hiyo ni zaidi ya Sh milioni tatu, na hadi ikamilike itagharimu zaidi ya Sh milioni saba.

Hata hivyo anasema, kama angepata msaada wa kununua mkoba wa vifaa vya ufundi (tool box), ambao unagharimu Sh milioni 15, angeweza kufanya mambo makubwa zaidi. Kwa sasa helkopta hiyo iliyotengenezwa kwa mabati maalumu kutoka China, inawashangaza wananchi na mafundi wengine ambao wako kwenye eneo inakotengenezwa.

Fundi Ramadhan anasema ingawa wapo baadhi ya wanajamii wanaostaajabu ubunifu huo, lakini mkewe anamtia moyo kwa kuwa anafahamu kipaji chake. Anasema kwenye familia na ukoo wao asilimia kubwa wote wako kwenye fani za ufundi, ambapo dada yake ambaye walichaguliwa naye kujiunga na shule ya sekondari hivi sasa ni mhandisi wa maji.

"Tulichaguliwa kujiunga kidato cha kwanza na dada zangu wawili, mimi sikumaliza mwaka nikaacha shule ila dada yangu ndiye aliyemaliza na kufika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam", anasema fundi Ramadhan. Anaongeza kwamba dada yake huyo alichukua masomo ya uhandisi wa maji na hivi sasa ni Mhandisi kwenye Idara ya Maji Zanzibar.

Helkopta hiyo yenye jina la RASOMAKA, fundi Ramadhan anasema aliwaza aiite jina gani ndipo akaamua kuiita majina yake kwa kipufi. Ramadhan hakuanzia hapo ubunifu wake, kwani baada ya kufuzu masomo ya ufundi makanika mjini Singida, alichukua mafunzo kwa njia ya posta nchini Uganda kwa miaka miwili na kutunukiwa Cheti.

Hakuishia hapo, kwani ujuzi wake wa ufundi ulimfanya apate kazi kwenye Idara ya Ujenzi kama fundi magari na aliacha kazi hiyo mwaka 1975 na kwenda Shinyanga kujifunza utengenezaji wa pikipiki.

Ni umahiri wake wa kutengeneza vyombo vya moto ndio uliomfanya kampuni nyingi kumtafuta na baadhi ya kampuni alizofanya kazi ni za China zilizopo nchini. Hata hivyo ujuzi huo ulimfanya aende Burundi kwenye Kampuni ya UMP ya pikipiki aina ya Yahama na Renout ambapo alikuwa na kazi ya kutengeneza na kuunganisha pikipiki.

Kupitia ujuzi huo kama fundi pikipiki na pia mbunifu wa kutengeneza vifaa kama clachi, stata, plagi na vipuri vingine vya vyombo vya moto na kuongeza kuwa kama angewezeshwa, kupata baadhi ya mashine angekuwa mbali. Mashine ambazo kama wahisani wangemwezesha kununua, ni pamoja na mashine ya kuchonga vyuma, kutoboa, kompresa pamoja na mkoba wa vifaa vya ufundi.

Mbali na ujuzi wake wa kubuni na kutengeneza helkopta hiyo, fundi Ramadhan mwenye mke na watoto watatu, bado ni baba bora aliyewasomesha wanawe na hivi sasa wote wanajitegemea. Fundi Ramadhan, anaamini kwamba kila mwenye bidii ya kazi anafanikiwa na kwamba ili kutimiza malengo yako, ni lazima kujaribu kufanya kitu na sio kuogopa.

"Mafanikio huja taratibu, fanya kazi kwa bidii, jitume na pia timiza ndoto zako kwa kujaribu kufanya jambo badala ya kuogopa na kuanza kuwaza", anasisitiza Ramadhan. Hivyo ndivyo fundi Ramadhan anavyofanya shughuli zake kwa kujaribu kutekeleza kile ukionacho, na kwamba akifanikiwa atazungumza na mamlaka husika kumsaidia kutengeneza helkopta kubwa zaidi yenye kuchukua abiria.
http://www.habarileo.co.tz/makala/?n=2791&cat=makala
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom