Udanganyifu katika mitihani una historia yake

Feb 13, 2017
5
8
Udanganyifu kwenye mitihani una historia yake

Moja ya habari kubwa kila yanapotangazwa matokeo ya mitihani ya kitaifa huwa udanganyifu unaofanywa na watahiniwa, hii ni kwa darasa la nne na Saba, kwa elimu ya msingi, kidato cha pili, nne na sita kwa elimu ya sekondari na hata kwenye vyuo vya taaluma mbali mbali.

Ni takribani siku kumi zimepita tangu kutangaza matokeo ya darasa la nne na kidato cha pili, miongoni mwa habari zake kubwa ilihusu wanafunzi 206 waliofutiwa matokeo kwa sababu za udanganyifu.

Kabla ya vumbi la matokeo hayo kutulia, Jumatano ya wiki hii tena, yametangazwa matokeo ya kuhitimu elimu ya ukunga na uuguzi ambapo wahitimu 1,330 wamefutiwa matokeo kutokana na udanganyifu.

Mijadala imekuwa mingi kwa kila kada, lakini yote imejikita kwenye matokeo ya tatizo na sio kiini cha tatizo lenyewe, tu apaswa kuangalia zaidi tulipojikwaa na sio tulipoangukia.

Haya tunayoyashuhudia sasa ni matokeo ya tulichokipanda kwenye miaka ya 70 hadi 90.

Hili janga limeanzia mbali sana, kipindi cha madaraka mikoani, mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi ilisimamiwa na Mkoa, kwa maana ya Ofisi ya Afisa Elimu Mkoa (REO), walitunga, walichapisha na kusambaza.

Linapokuja suala la udhibiti wa mitihani inafahamika, kuna usiri wa kiwango cha juu sana, hivyo ni wazi chanzo cha kuvuja ilikuwa ofisi hizo hizo za mkoa ambazo ndizo zilizokuwa na jukumu la usimamizi.

Kwa kuwa wao sio walimu waliohusika kufundisha darasani, waliwatumia baadhi ya walimu kuwatayarisha watoto wao, hiyo ikawa hatua ya kwanza ya kuvuja kwa mitihani, na walengwa hapo wakiwa watoto wa viongozi ngazi za mkoa, Wilaya, marafiki na jamaa zao.

Wanasema hakuna siri ya zaidi ya mtu mmoja, walimu nao wakapata fursa ya kusaidia vijana wao, mnyororo wa wanufaika ukaongezeka.

Mwishoni mwa miaka ya 1980 kuja 90 wimbi likahamia sekondari, waliokuwepo miaka hiyo watakumbuka vijana walivyohangaika huku na kule kipindi cha mitihani ya kidato cha nne na sita, wakitumia kauli kama vile papers imevuja, ipo shule........X

Nani alivujisha mitihani wakati inasimamiwa na Baraza la Taifa la Mitihani, miongoni mwa taasisi chache zinazoaminika kuwa na usiri wa kiwango cha juu kabisa?

Mwanafunzi hana fursa ya kuiba mtihani, ni wazi yupo anayemuibia, na huyu atakuwa yule mwenye dhamana.

Wimbi likahamia vyuo vikuu kwenye kwenye miaka 2,000, na nakumbuka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kililazimika kuanzisha mtihani wa mchujo kwa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga pale, ni kipindi kilichoshuhudia wimbi la wandaaji wa thesis mitaani, Sinza ilitajwa kuwa moja ya maeneo walikopatikana hao wataalamu.

Hivyo basi, hata tunapojadili incompetence kwenye utendaji wetu, ni vema kupitia historia ya elimu yetu.

Kwa mtiririko huu, tusione ajabu watu leo hii wakiona wizi, udanganyifu na uzembe kuwa mambo ya kawaida, kwa baadhi yetu ni uzao wa huo uchafu.

Tunaondokaje kwenye huu mkwamo kama taifa?

Hili ni swali lenye kuhitaji mjadala wa kitaifa na utashi wa kisiasa!.
 
Back
Top Bottom