Uchambuzi wa Bajeti ya Ujenzi na Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2023/24

ACT Wazalendo

JF-Expert Member
May 5, 2014
610
1,540
Uchambuzi wa Bajeti ya Ujenzi na Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Utangulizi.
Katika mwendelezo wa uwasilishaji, mijadala na upitishwaji wa bajeti Bungeni, Jana tarehe 22 Mei 2024, Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (Mb), aliwasilisha hotuba ya utekelezaji wa bajeti kwa mwaka uliopita na mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2022/23. Mjadala wa bajeti hii umeanza jana na leo utaitimishwa kwa Bunge kuidhinisha bajeti hiyo).

Katika mwaka wa fedha 2023/24, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi inaomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi trilioni 3.55 (3,554,783,957,000.00) kati ya fedha hizo, Shilingi trilioni 1.468 (1,468,238,449,000.00) ni kwa ajili ya Sekta ya Ujenzi na Shilingi Trilioni 2.4 (2,086,545,508,000.00) ni kwa ajili ya Sekta ya Uchukuzi. Bajeti hii ni upungufu wa Shilingi bilioni 310 Sawa asilimia 8.03
Tunafahamu kuwa Mpango na bajeti ya Wizara itaenda kusimamia masuala ya ujenzi, utengenezaji na ukarabati wa Miundombinu ya reli, barabara, bahari, maziwa na anga. Aidha kuwezesha kusimamia na kudhibiti huduma za uchukuzi na usafirishaji nchini na kusimamia taasisi zilizo chini yake.

Hivyo basi, katika kuchangia mjadala wa bajeti hii muhimu na kutimiza wajibu wa kuisimamia na kuiwajibisha Serikal, Sisi ACT Wazalendo kupitia Waziri Kuvuli wa Miundombinu ya Ujenzi, Reli na Barabara Eng. Mohammed Mtambo na Naibu Waziri Kuvuli Eng. Fidel Christopher tumefuatilia hotuba na kuichambua ili kuona kwa kiasi gani imeweza kubeba matarajio na matamanio ya wadau na wananchi kwa ujumla wake.

Kupitia uchambuzi huu tumekuja na hoja kubwa nane (8) kuhusu bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

1. Kuchelewa kukamilika na kuongezeka kwa gharama za ujenzi wa Reli ya SGR
Wizara ya ujenzi na uchukuzi kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC), inasimamia utekelezaji wa ujenzi wa reli ya kisasa yaani “Standard Gauge Railway” (SGR), inayounganisha Dar es Salaam, Mwanza, Kigoma, Katavi na nchi jirani za Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. SGR ina urefu wa kilomita 1,800, upana wa milimita 1,435.
Uchambuzi wetu wa taarifa mbalimbali za utekelezaji wa Mradi huu muhimu umebaini mambo makubwa mawili;

Mosi, kuna ucheleweshaji wa ukamilishaji wa mradi. Kipande cha kwanza na cha pili vipo vyuma ya wakati kwa zaidi ya miaka mitatu. Hali ya utekelezaji wa mradi huu kwa mujibu wa ripoti ya hali ya uchumi na utekelezaji wa bajeti wa Wizara ya Fedha kwa mwaka 2023/24 hadi kufikia Juni 2023 hakuna kipande hata kimoja kilichokamilia.

Hali halisi inaonyesha kama ifuatavyo; kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (97.65 %), Morogoro – Makutupora (91.32%), Mwanza – Isaka (19.70%) Makutupora – Tabora (3.26%);
Mfano wa hasara zilizoletwa kwa ucheleweshaji utaona kwenye kipande cha kwanza. Kwa mujibu wa mkataba wa ujenzi wa reli kwa kipande cha kwanza Dar- Moro ulitakiwa kukamilika tarehe 1 Novemba 2019.

Hata hivyo mradi huo uliongezwa muda wa kukamilika mara saba zaidi, na kuongeza siku 1,414 hadi muda wa kukamilika, sawa na miaka 3.8. Ila hadi sasa bado ujenzi haujakamilika kwa muda uliopangwa Hii imepeleke kuongezeka kwa gharama ya zaidi ya Shilingi bilioni 25 (Dola za kimarekani Milioni 11.32)

Pili, kuongezeka kwa gharama ya Ununuzi wa treni (vichwa vya treni, treni za kisasa za umeme na mabehewa ya abiria).

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ameibua hoja ya ukiukwaji wa sheria ya manunuzi na hivyo kupelekea kuongezeka kwa gharama za manunuzi. CAG anasema kuwa Gharama ya Ununuzi wa treni (vichwa vya treni, treni za kisasa za umeme na mabehewa ya abiria) iliongezeka kwa Dola za Kimarekani milioni 215 baada ya kukataliwa kwa zabuni zingine zote bila sababu ya msingi.

Tatu, kuongezeka kwa gharama za Ujenzi wa SGR kipande cha 3 na 4. Kutokana na uamuzi wa Serikali kukubaliana na masharti ya Benki ya Standard Chartered kuilazimisha TRC kuwa na zabuni bila ushindani, gharama za Ujenzi wa SGR ziliongezeka kwa Dola za Kimarekani Milioni 1.3 na 1.6 kwa kilomita moja mtawalia, sawa na nyongeza ya USD 742M kwa ujumla. Ongezeko hili la gharama lingeweza kuepukika kama kungekuwa na ushindani katika zabuni, kipande na,1, 2 na 5 kilichoshindanishwa, gharama za Ujenzi wa kilomita 1 ilikua dola za marekani milioni 4.1, 4.6 na 3.9 mtawalia. Kampuni iliyopewa zabuni ya kipande cha 3 na 4 iliweka bei ya dola za marekani milioni 5.2 na 5.5

ACT Wazalendo tunaendelea kusisitiza wito wetu kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuunda Kamati Teule ya Bunge kufanya uchunguzi wa kina wa masuala haya matatu yaliyoibuliwa na CAG katika Taarifa yake ya mwaka huu Hii ni kutokana na ukweli kuwa hoja hizi ni nzito sana na hazipaswi kusubiri utaratibu wa kawaida wa Kamati ya Bunge ya Mahesabu ya Serikali (PAC) kwani mchakato huo ni mrefu sana. Kamati hiyo ipewe hadidu rejea ambapo pamoja na mambo mengine

Mosi, Kamati iwahoji Benki ya Standard Chartered ya Uingereza kuhusu masharti ya kutulazimisha Mkandarasi wa Kujenga reli Pili, Kamati ichunguze sababu zilizopelekea TRC kuchukua njia ya ‘single source’ katika vipande namba 3 na namba 4, uzembe na ucheleweshaji wa kumalizika kwa vipande vya mradi vinavyopelekea kuongezeka kwa gharama na Tatu, Kamati ichunguze sababu za Bei ya manunuzi ya treni kuongezeka maradufu.

2. Zimwi la ushiriki wa sekta binafsi kwenye ujenzi wa reli na barabara
Ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPPs) unazidi kukuzwa kama njia ya kupata fedha zinazohitajika ili kutekeleza miradi ya maendeleo hususani ujenzi wa miundombinu ya reli na barabara. Wakereketwa na wanazi wa mtazamo huu wanadai kwamba Ubia ni njia bora ya kuziba pengo la kutotekelezwa kwa kasi kwa ujenzi wa Miundombinu kunatokana na ukosefu wa fedha za kutosha kutoa huduma muhimu ili kufikia malengo tarajiwa.

Katika mpango wa bajeti wa wizara ya ujenzi na uchukuzi 2023/24 tumeona kutawaliwa na maumuzi ya kujenga reli na barabara kwa ubia na sekta binafsi; kutafuta mwekezaji kwa ubia baina ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) kwa mradi wa reli ya Mtwara – Mbambabay na matawi yake ya Liganga na Mchuchuma na Tanga – Arusha – Musoma. Barabara ya Chalinze hadi Morogoro kujengwa kwa mfumo huo na maeneo mengine.

Ubia unapigiwa chapuo kama ni njia mbadala ya kugharamia ujenzi wa miundombinu au kutoa huduma ambazo kwa hoja kadhaa; Mosi, gharama zinazotumika na Serikali kwa uwekezaji katika miundombinu ni kubwa hivyo itachukua muda mrefu kukamilisha kwa kutegemea fedha za walipa kodi.

Pili, mfumo wa ubia unatoa nafuu kwa Mfuko Mkuu wa Serikali (Hazina) kubeba mzigo wa gharama kwa mkupuo kulipia miradi ya maendeleo na kupunguza mahitaji ya kukopa ili kuanzisha miradi ya ujenzi.

Tatu, hoja inayojengwa ni kwamba ubia wa sekta ya umma na binafsi unapotumika kwenye ujenzi wa miundombinu inapanua wigo wa muda wa kulipia kutoka papo kwa papo hadi muda mrefu zaidi (nafasi ya kupumua).
Masikitiko yetu makubwa na tahadhari tunayoitoa kwa Serikali kutokumbatia mwelekeo huu kwa kuwa hoja zinazojengwa zinajaribu kupumbaza umma kama ni njia ya kujikomboa kumbe unawapeleka utumwa kwa kuongeza mzigo na minyonyoro kwa walipa kodi. Sababu za tahadhari yetu ni kama zifuatazo;

Kwanza, Ubia (PPP) mara nyingi ni ghali zaidi kuliko mfumo wa kawaida wa ugharamiaji unaofanywa na Serikali. Hii ni kutokana na gharama ya mtaji, matarajio ya faida ya makampuni binafsi na gharama za malipo ili kujadili mikataba tata ya Ubia (PPP). Gharama ya mtaji kwa kawaida ni ghali zaidi katika miradi ya ubia kuliko miradi ya ujenzi inayofanywa na Serikali pekee yake kwa sababu Serikali hazilengi kupata faida; Pia, hata zinapokosa mtaji zinaweza kukopa pesa kwa viwango vya chini vya riba kuliko makampuni binafsi.

Pili, hoja ya kutoa nafuu ni jambo la muda mfupi, deni linatunzwa kwa siku za usoni. Tatu, miradi itakayojengwa kwa mtindo huu inakuja na tozo, makato na kodi kwa watumiaji ili kupata mapato na faida kwa aliyewekeza jambo linaloweza kuwaondoa wanachi wasioweza kumudu gharama hizo kutumia miundombinu hiyo au kuanzisha bughudha katika kutumia kwake.

Kwa uchambuzi wa jumla, Ubia wa Sekta ya Umma na binafsi katika ujenzi wa Miundombinu ni njia ya kuficha deni la taifa kwa kutumia mbinu za kihasibu zisizo wazi.

Pili, ni mbinu fiche ya ubinafsishaji wa Miundombinu ya kimkakati ambayo itatengeneza matabaka katika matumizi au kuzalisha kero/bughudha kubwa wakati wa matumizi yake (Mfano wa daraja la Kigamboni) ni ajabu sana kuona mwekelekeo huu kutazamwa na Viongozi wa Serikali na CCM kama mwarobaini wa kumaliza changamoto zinazoikabili sekta ya miundombinu.

ACT Wazalendo tunaendelea kuitaka Serikali iimarishe mfumo wa Usimamizi wa ujenzi wa reli na Barabara kwa kushughulikia ubadhirifu, uzembe na kutowalipa kwa wakandarasi.
Vilevile, tunatoa wito kwa Serikali kuzuia mianya ya upotevu wa fedha za umma zinaoelekezwa kwenye sekta ya uimarishaji wa miundoimbinu ya reli na barabara. Mwisho, Serikali iachane na mawazo ya kubinafsisha miundombinu ya kimakakati ya reli na barabara kwa madai ya juu juu yanayoweza kuongeza mzigo zaidi.

3. Uwekezaji na hasara katika uendeshaji na usimamizi wa Ndege za Shirika la ATCL
Kampuni ya ndege ya Taifa (ATCL) ina wajibu wa kusimamia uendeshaji wa ndege za Serikali kwa kukodishiwa kwa niaba ya Serikali. Tangu kufufuliwa kwa kampuni hii mwaka 2016 kuna changamoto kadhaa za uendeshaji. Ikiwemo mzigo mkubwa wa madeni ya uendeshaji, kuharibika mara kwa mara kwa injini za ndege na gharama kubwa za uendeshaji;

Kuhusu hoja ya gharama kubwa za uendeshaji na mzigo wa madeni. Katika uchambuzi wetu wa ripoti ya CAG ya mwaka 2021/22 tuliofanya April 11, 2023 tulieleza zinatokana na maamuzi mabovu yaliyofanywa na Serikali mwaka 2016 kuhusu Wakala wa Ndege za Serikali. Mosi, uamuzi wa kuipeleka TGFA kuwa chini ya Ofisi ya Rais Ikulu kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Pili, Wakala kuongezewa jukumu la kuratibu ununuzi wa ndege, kuzikodisha kwa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) na kusimamia mikataba ya ukodishwaji wa ndege hizo kwa niaba ya Serikali, mbali na jukumu lake la asili la kutoa huduma ya usafiri wa anga kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na viongozi wengine wa Kitaifa.

Tulieleza athari za uamuzi huo unathibitishwa na ripoti ya CAG, ambayo imeonyesha ATCL wanaendelea kupata hasara ya Shilingi bilioni 35 sambamba na Shirika hilo kuwa na mtaji hasi wa Shilingi bilioni 158. Tuliweka wazi kuwa hasara inayopata ATCL kwa sehemu kubwa inatokana na mfumo wa umiliki wa ndege. Mfumo uliopo sasa ATCL haimiliki ndege. Ndege zote zilizonunuliwa na Serikali kwa fedha za walipa kodi zinamilikiwa na TGFA na kukodishwa kwa ATCL. Mfumo huu unaoleta hasara kwa taifa unatokana na uamuzi wa mwaka 2016.

Hoja ya pili, ufinyu wa bajeti ya ukarabati, matengenezo na ununuzi wa ndege nzuri. Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge iliyowasilishwa jana imethibitisha kuwa injini mbili za ndege za Serikali zimeharibika (mbovu). Itakumbukwa Februari 19, 2023 Kiongozi wa Chama Ndg. Zitto Kabwe alieleza kuhusu kuwepo kwa taarifa ubovu wa ndege hizi. Mkurugenzi Mkuu wa ATCL akatoka hadharani kupinga hoja ile.

Jana Mwenyekiti wa kamati ya Miundombinu na Uchukuzi ameliambia Bunge kuwa kuna injini mbili kubwa za ndege zimeharibika, jambo hili linachochea wito wetu wa kutaka uchunguzi wa kina katika ununuzi wa ndege kuanzia ulipoanza mwaka
Aidha, hali ya upatikanaji wa fedha za bajeti kwa ajili ununuzi na matengenezo ya ndege. Katika mwaka wa Fedha 2022/2023 Bunge liliidhinisha kiasi cha Shilingi Bilioni 353 kwa ajili ya mradi wa ununuzi wa ndege lakini hadi kufikia Februari 2023 ni Shilingi Bilioni 27.07 zilipelekwa sawa na asilimia 7.7 kwa hiyo zaidi ya asilimia 92 ya Fedha hazijapelekwa, Serikali hii hii inasema inafanya Malipo ya ndege mpya Tano ambapo kati hizo ndege moja aina ya Boeing767-300F ilitarajiwa kuwasili nchini mwezi march 2023 na ndege nyengine zote nne kuwasili Baadae mwaka huu.

Hivyo basi, ACT Wazalendo tunarudia wito wetu wa kuitaka Serikali kuirejesha TGFA wizara inayohusika na uchukuzi ili kudhibiti ubadhirifu na wizi kwa kuimarisha uwazi, kwa kuwa bajeti ya wizara ina kaguliwa na ripoti yake inakuwa wazi.

Pili, tunaitaka Serikali imwagize CAG kufanya ukaguzi maalumu wa manunuzi ya ndege tangu tulipoanza kununua ndege mwaka 2016. Tatu, tunaitaka Serikali ifanye mapitio ya mikataba yote ya manunuzi ya ndege kwa lengo la kuiboresha kwenye mapungufu.
Nne, Serikali ipeleke fedha za kutosha kama ilivyoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya miradi ya maendeleo ikiwemo kununua ndege ili kusukuma maendeleo ya Sekta nyengine nchini.

4. Msongamano Bandari ya Dar es Salaam
Kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko yasiyoisha ya kuwepo kwa msongamano wa magari unaopelekea kuwepo kwa muda mrefu wa kusubiri kupakia au kupakua mizigo. Ucheleweshwaji unaosababisha na uwezo wa bandari kumudu mahitaji hayo, unapaswa kufanyiwa kazi kwa haraka.

Hususani katika kipindi hiki ambapo gharama za vitu vimekuwa juu, gharama zinazoweza kuokolewa kwa kuboresha utendaji na uwezo wa bandari zitaenda kuwasaidia wananchi kupata huduma kwa bei ya chini kuliko hivi sasa. Katika hotuba ya mwaka jana Waziri wa Ujenzi na uchukuzi Prof. Makame Mbarawa alitaja kufanya maboresho ya GAT na. 7 & 8 kulijenga, lakini katika hali ya utekelezaji bado halijakamilika, ahadi imejirudia tena kwa mwaka na kutegewa fedha kiasi cha shilingi Bilioni 7.

Sisi, ACT Wazalendo tuna mapendekezo yafutayo ili kukabiliana na changamoto za msongamo katika bandari ya Dar es Salaam.
Mosi, Wadau wote wa bandari waunganishwe kwenye mfumo wa kielektroniki unaotumiwa na bandari ili kuweza kuharakisha uondoshwaji wa mizigo bandarini kwani wakati mwingine mizigo inachelewa kutokana na wadau wengine kama Mkemia Mkuu, Shirika la Viwango Tanzania-(TBS), Wizara ya Nishati na Wizara ya Madini na wengine wengi kutokuwemo kwenye mfumo huo;

Pili, Mchakato wa kuwa na eneo Kurasini-Shimo la Udongo ambalo litatumika kuegesha magari yanayoingiza na kutoa mizigo bandarini sasa ufanyike kwa haraka ili eneo hilo lipatikane kwani mojawapo ya kero za wafanyabishara wanaotumia Bandari ya Dar es Salaam ni kutokuwa na maegesho jambo ambalo husababisha usumbufu na gharama zisizotabirika;

Tatu, Serikali kuharakisha ujenzi wa bandari za nchi kavu ili kupunguza gharama kwa wateja kusafiri mpaka Dar se salaam kwa ajili ya kutoa mizigo. Ni muda sasa tangu Serikali imeanza mipango ya kujenga bandari kavu katika maeneo ya Kwala -Pwani, Ihumwa -Dodoma, Katosho-Kigoma na Misungwi –Mwanza;
Nne, kuimarisha na kuboresha bandari ya Tanga, Lindi na Mtwara ili kupunguza msongamano Bandari ya Dar es salaam.

5. Madai na stahiki za madereva wa masafa marefu
Kwa muda mrefu madereva wa magari ya masafa marefu (Nje ya Nchi) wamekuwa na malalamiko yasiyosikilizwa kuhusu maslahi yao, mazingira ya kazi na mifumo ya sheria na utekelezaji wake katika kusimamia madereva na sekta ya usafirishaji.

Mambo yanayolalamikiwa sana yakihusisha; matamko ya mara kwa mara ya uendelezaji wa mafunzo au ujuzi wa udereva. Madereva wamekuwa ni waathirika wa kuanzishiwa operesheni maalumu za kuendeleza ujuzi kwa gharama zao bila ya kuwa na mfumo shirikishi. Mfano tarehe Machi 1, 2023 Jeshi la Polisi lilitangaza operesheni maalumu ya kukagua vyeti vya udereva kwa madereva wote hasa wa leseni za daraja C na E wafike kwenye Ofisi za makamanda wa mikoa kwa ukaguzi, Operesheni hii ilitishia kunyang’anya leseni madereva wasio na vyeti au warejee darasani jambo hili si baya lakini halikuwa shirikishi.

Pili, suala la maslahi ya madereva. Sekta ya uchukuzi (Usafirishaji) imekosa uangalizi wa karibu kutoka kwa Serikali hususani eneo la maslahi ya madereva. Madereva wengi wanafanya kazi bila mikataba ya kazi. Aidha, wanadai kupewa fedha ya kila siku (allowance) badala ya kwa mujibu wa masafa (mileage) wakiwa safarini.

Wanadai malipo ya dola 10 kwa siku wanayolipwa juu ya fedha ya TShs 700,000 ya jumla wakiwa safarini yaongezwe kwa sababu kiasi cha dola 10 wakiwa ugenini ni kidogo mno kujikimu. Wanadai usafirishaji wa mafuta, ambayo yana mtindo wa kupotea kwa mujibu wa joto (evaporating) uangaliwe upya ili isiwe madereva. Wanadai kupatiwa posho maalumu wanaposafirishaji mzigo wenye sumu. Wadai kufikiriwa upya gharama za kukimu mafuta wanazopewa ambazo ni za kiwango cha chini.

Tatu, Usalama wa madereva wawapo nje. Yapo matukio mbalimbali ya wizi, uporaji na uhalifu wanaofanyiwa maderva wawapo safarini. Madereva wengi wanaopata ajali wakiwa kazini au kufariki huwa hawalipwi au malipo kiduchu hutolewa na makampuni na kuacha familia zao katika ufukara, hii ni kwa sababu madereva wengi hawapewi mikataba bali maelewano ya juu juu. Haya na matukio mengine mengi yamekuwa yakiwakatisha tamaa madereva wengi ambao ndio wanaosukuma maendeleo ya sekta ya uchukuzi.

Kwa ujumla changamoto wanazopitia madereva wa masafa marefu zipo katika makundi haya ni

i. Mikataba, Madai na Haki na maslahi yao maeneo ya kazi.

ii. Changamoto za kiutendaji na kiutawala wawapo safarini ndani na nje ya nchi.

iii. Changamoto za kiafya na kiusalama katika ubebaji wa kemikali zenye sumu.

iv. Changamoto za kiusalama wawapo nje ya nchi

ACT Wazalendo tunaichukua sekta ndogo ya madereva kama askari wa mstari wa mbele wa kukuza uchumi wetu hasa katika biashara ya nje hivyo madai yao yanapaswa kufanyiwa kazi haraka ili kuwatia moyo na ari ya kufanya kazi.
Mosi, tunaitaka Serikali kusimamia utekelezaji wa sheria ya ajira na mahusiano kazini ya mwaka 2004 katika sekta ya usafirishaji (madereva).

Pili, tunataka Madereva wanaosafirisha nje ya nchi walipwe malipo mazuri tunapendekeza walipwe kwa Viwango vya Kimataifa kama wanavyolipwa madereva wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za kusini Afrika SADC.

Tatu, tunataka kiundwe chombo maalumu kitakacho simamia, kulinda na kutetea maslahi ya madereva (Chama cha Madereva Tanzania).

6. Mradi wa Mabasi yaendayo haraka unatekelezwa chini ya Kiwango.
Katika Hotuba yake Bungeni Waziri Prof. Makame Mbrawa (Mb) ameliambia bunge kuwa kazi za ujenzi wa barabara ya Mabasi Yaendayo Haraka Awamu ya Pili (CBD – Mbagala, Km 20.3) zimefikia asilimia 90 na ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka Awamu ya Tatu (CBD – Gongolamboto km 23.33) zimefikia asilimia 5.

Taratibu za manunuzi ya Mkandarasi wa kazi za ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka Awamu ya Nne (Ali Hassan Mwinyi – Morocco – Mwenge – Tegeta na Mwenge – Ubungo (km 30.12) zinaendelea
Ripoti ya CAG imeonyesha kuwa Ujenzi wa kipande cha CBD-mbagala haukidhi viwango kama ilivyoainishwa kwenye mkataba kati ya Msimamizi wa Mradi (TANROADS) na mkandarasi katika maeneo mbalimbali kama vile unene wa lami, viwango vya chini vya madaraja ya watembea kwa miguu Mbagala na vizuizi vya ajali vya barabara ya juu ya Kilwa na Mandela.

Uchambuzi wetu unaonyesha kwamba Mradi huu ni moja ya miradi inayotekelezwa kwa kiwango cha chini kabisa katika nchi yetu. Hoja alizoziibua CAG zinaonyesha wazi wazi harufu ya ubadhirifu na/au uhujumu wa Mradi. Kwa kuwa Mradi huu ni mkopo ambao utalipwa na kila Mtanzania awe wa Dar es Salaam au nje ya Dar es Salaam tuna mashaka kuwa Barabara nzima itakuwa mbovu na hata kusababisha maafa kwa watumiaji.

Mbali na kipande hiki kuwa hakijakamilika na kimejengwa chini ya kiwango tayari Serikali kupitia TANROADS wameshampa tena mkandarasi huyohuyo kipande cha CBD- Gongo la Mboto (km 23.33),
ACT Wazalendo, tunamashaka na Ubora wa mradi huu, hivyo tunaitaka TANROADS imfute kazi Mshauri wa Mradi kwa kushindwa kumsimamia mkandarasi vizuri.

Pili, TANROAD iwe macho katika kuangalia utekelezaji wa mradi huu ili kuhakikisha ubora kulingana na thamani ya fedha ambayo ni mkopo. Tunataka kuwa na mradi bora utakaohudumia watu na kupunguza adha barabarani na si kusababisha misongamano na ajali kutokana na Ubovu wa mara kwa mara.

7. Matengenezo ya vivuko nchini ni kizungumkuti.
Kufuatia ubovu wa muda mrefu wa vivuko vya kigamboni mnamo tarehe 16 Februari 2023 Serikali kupitia wakala wa ufundi umeme Tanzania [TAMESA] ilisaini mkataba wa matengenezo ya kivuko cha Mv magogoni na kampuni ya Africa Marine and General Engineering ya nchi ya Kenya. Mkataba huo wa una thamani ya shilingi Bilioni 7.5. Mchakato wa matengenezo ya kivuko hiki kimezua maswali mengi mno. Miongoni mwa mambo yaliyoibua maswali mengi ni pamoja na:

Gharama ya ukarabati wa kivuko si halisi. Imeonekana kutoendana na matengenezo yaliyotajwa kwani ukitoa engine na gearbox ambazo gharama yake haizidi bilioni 2, matengenezo mengine kama kupaka rangi kivuko na kufunga mifumo ya CCTV ni ya kawaida gharama zake haziwezi kufikia bilioni 7.5 iliyotajwa na TEMESA huku kivuko hicho kipya kilitengenezwa kwa Bilioni 8 tu.

Kuchelewa Ukarabati wa Meli ya Mv Mwongozo. Takribani miaka saba sasa tangu Mv Mwongozo kuacha kufanya kazi kwa sababu ya changamoto ya msawazo lakini Serikali ipo kimya. Sababu ya meli hiyo kutofanyiwa matengenezo mpaka sasa haijajulikana. Kukosekana kwa meli katika ziwa Tanganyika kunakwamisha shughuli za kimaendeleo kwa wakaazi wa maeneo hayo.
Aidha Ukarabati wa vivuko kama Mv Musoma, Mv Tanga, Mv Misungwi, Mv kilombero, Mv Nyerere, Mv Mara, Mv Kitunda na Mv Kyanyambasa hivi vivuko vyote havijakamilika sababu inayopelekea kucheleshwa kwa ukarabati wa vivuko hivyo haijulikani hali inayoleta shida kubwa kwa wakaazi wa maeneo hayo.

ACT Wazalendo Tunaitaka Serikali kushughulikia masuala ya utengezaji wa vivuko na meli kwa umakini na uharaka. Meli na vivuko hivyo virudi kufanya kazi ili kusaidia kuondoa adha kwa watumiaji wa vivuko hivyo.
Pili, tunaitaka Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) kuchunguza upya mchakato wa zabuni ya MV KIGAMBONI kwani kuna mashaka kwa Umma kwamba matengenezo yake yana viashiria vya rushwa na upendeleo.

Aidha tunatoa wito kwa Serikali kuwekeza vizuri kwenye kuboresha miundombinu ya vivuko na kuwachukulia hatua kali za kisheria wote wanaohujumu miundombinu. Serikali iachane na mawazo yoyote ya kubinafsisha huduma ya vivuko.

8. Ucheleweshaji wa Miradi ya Barabara maeneo ya pembezoni
Utelekezaji wa miradi ya barabara imekuwa ikichukua muda mrefu sana hasa kwa upande wa barabara za pembezoni mwa nchi. Hii ni changamoto kubwa sana. Serikali imekuwa inatengeneza matabaka katika utoaji wa huduma za msingi kwa jamii.

Yapo maeneo mengi tangu kupata uhuru bado hawajapata kushuhudia mradi wa barabara kwa kiwango cha lami lakini wakienda kwenye majiji makubwa wanakuta miradi mbalimbali inaendelea. Hii inasabisha vijiji vingi kutokuendelea na thamani ya uzalishaji mazao kutowanufaisha wazalishaji bali wachache kwa kisingizio cha usafiri.

Tunaona bajeti inatengwa kila mwaka kwa ajili ya kulipa mkandarasi au upembuzi yakinifu bila kuona barabara hizo zikikamilishwa kama mfano wa miradi hiyo ni barabara ya Soni-Bumbuli-Dindira-Kongowe (km 74) Barabara ya Mtwara-Newala-Masasi Barabara ya Likuyufusi-Mkenda (km122.50) Barabara ya Nachingwea-Liwale (km130), Nangurukuruku-Liwale (km210) Hii inaonyesha kwa kiasi gani Serikali inashindwa kufuatilia utekelezwaji wa miradi hiyo. Miaka nenda rudi barabara hazikamiliki. Wananchi wa maeneo hayo ndio wanaoteseka. Ajabu bajeti inatengwa kila mwaka lakini hakuna kinachofanyika; barabara zipo vilevile.

ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kuchukua hatua stahiki na kuhakikisha miradi hiyo inakamilika haraka iwezekanavyo ndani ya muda uliotolewa ili kuondoa mateso kwa wananchi ambao wamekuwa wakiteseka kwa muda mrefu sana na kuilalamikia Serikali juu ya barabara hizo. Serikali itengeneze barabara hizo ili kuchagiza maendeleo ya watu wanaoishi pembezoni hasa vijijini.

Hitimisho.
Katika uchambuzi wetu. Tumeona namna ucheleweshaji wa ukamilishwaji wa miradi mbalimbali unavyosababisha hasara ya kifedha na kuzorotesha hali ya upatikanaji wa huduma katika maeneo husika. Mradi wa Reli ya kisasa (SGR) kipande cha Dar es Salam hadi Morogoro umechelewa kwa miaka zaidi mitatu. Miradi mingi ya Barabara hususani za mikoa ya pembezoni imekuwa ikijirudiarudia kila mwaka kwenye bajeti ya wizara bila kukamilika. Mfano tulizozieleza Barabara za Pangani-Dar; Nanguruku- Liwale-Nachingwea- Mangaka kuitaka kwa uchache.

Aidha, changamoto za uwezo na ufanisi wa bandari ya Dar es Salaam kimekuwa kilio cha muda mrefu. Pia, tumeona mwelekeo mpya unaodhaniwa kama mwarobaini wa upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo namna utakavyoligharimu taifa. Kilio na madai ya madereva bado hayajashughulikiwa. Kila mwaka waziri mwenye dhamana haonyeshi nia kumaliza kero zao.

Mwisho, hoja zilizoibuliwa na CAG kwenye uendeshaji na Usimamizi wa shirika la ndege Tanzania (ATCL) ni muhimu sana Serikali kusikiliza ushauri wetu tulioutoa ili kuiwezesha wizara kusimamia kwa ufanisi. Lazima shirika lirejeshewe wajibu wake wa kimanunuzi na umiliki wa ndege zote inazozisimamia.

Imetolewa na;
Eng.Mohamed Juma Mtambo
Twitter @MtamboMJ_1
Waziri Kivuli wa Miundombinu, Barabara na Reli
ACT Wazalendo.
23 Mei, 2023
 
Back
Top Bottom